Dodoma. Serikali imesema uhalifu mtandaoni umeendelea kupungua kutokana na hatua zinazochukuliwa kukabiliana nao.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema hayo bungeni leo Mei 15, 2024 akijibu swali la Mbunge wa Buhigwe, Kavejuru Felix.
Mbunge huyo amehoji Serikali ina mikakati gani ya kukomesha wizi wa mtandaoni.
Akijibu swali hilo, Nape amesema Serikali imechukua hatua kadhaa kuweka mazingira salama kwa wananchi, hususani kwenye mitandao.
Amesema mwaka 2015, Serikali ilitunga Sheria ya Makosa ya Mitandao na Sheria ya Miamala ya Kielektroniki kwa lengo la kutambua miamala inayofanyika kimtandao, lakini pia kutambua kisheria makosa yanayofanyika kwenye mitandao ili kuchukua hatua stahiki yanapobainika.
Waziri Nape amesema katika kujenga mazingira salama ya kisheria, Serikali imetunga Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022, ambayo lengo lake ni kuweka utaratibu wa kuhakikisha wakusanya taarifa wote wanafuata misingi ya kulinda taarifa za mwananchi.
Amesema Serikali ilianzisha Kitengo cha Uhalifu wa Mitandao chini ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa makosa ya mitandao, ukiwemo wizi wa aina yoyote kwenye mtandao na kuandaa majalada ya kufungua mashtaka kwa kusaidiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
Amesema katika hatua nyingine, Serikali kwa kushirikiana na watoa huduma wa simu za mkononi imeanzisha mfumo kupitia namba 15040 wa kupokea na kuzifungia namba ambazo zimeripotiwa na kuthibitika kutuma ujumbe au kupiga simu za utapeli.
“Baada ya kuthibitisha namba kufanya vitendo hivyo, namba husika hufungiwa, Kitambulisho cha Taifa (Nida) kilichotumiwa kusajili namba husika kufungiwa kusajili na kifaa kilichotumika (simu) pia kufungiwa ili kisifanye kazi,” amesema.
Amesema Serikali itaendelea kuongeza jitihada za kuelimisha umma, namna nzuri ya kutumia Tehama kuendelea kudhibiti matukio ya utapeli na wizi wa kimtandao kupitia simu za mkononi.
Katika swali la nyongeza, Felix amesema pamoja na majibu hayo, bado wizi mtandaoni unaendelea, hivyo kuhoji ni nini kauli ya Serikali?
“Kwa kuwa laini zote zilisajiliwa na TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania) na Polisi inaruhusiwa kwenda kuchukua taarifa zozote za laini zilizotumika katika uhalifu kule TCRA, ni nini kilichofanya wasikamatwe,” ameuliza.
Waziri Nape amesema kazi ya kuwakamata wahalifu ni ya Jeshi la Polisi na kwamba TCRA inawezesha Polisi kupata taarifa za wahalifu.
Hata hivyo, amesema kazi ya kufungia laini za simu zilizofanya uhalifu ni ya TCRA kwa kushirikiana na watoa huduma.
“Taarifa zinaonyesha uhalifu wa mtandaoni unaendelea kupungua,” amesema.
Amesema Septemba mwaka 2023 kulikuwa na laini za uhalifu 23,328 lakini Desemba mwaka 2023 laini hizo za uhalifu zilifikia 21,000.
Nape amesema Machi mwaka 2024, laini za uhalifu zilikuwa 17,318.
Amesema walipoanza uhakiki zilikuwa laini za simu zaidi ya milioni tisa lakini walivyozihakiki walifunga laini zaidi ya laki tisa, hivyo inaonyesha uhalifu unapungua.
Amewataka wananchi inapotokea tatizo kama hilo, wafuate utaratibu wa kuripoti ili hatua zichukuliwe.
Amesema Jeshi la Polisi limeendelea kufanya kazi nzuri ya kuwakamata wahalifu na kuwapeleka mahakamani, na hivi karibuni wameanza kuwatangaza.
Amewahakikishia wabunge kuwa usalama mtandaoni unaendelea kuimarika kwa sababu Tanzania inaenda katika uchumi wa kidijitali.