Ousman Sonko wa Gambia afungwa miaka 20 jela – DW – 15.05.2024

Mahakama ya Uhalifu ya Shirikisho la Uswizi hii leo imemhukumu aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani wa Gambia Ousman Sonko kifungo cha miaka 20 jela kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu aliotenda chini ya utawala wa dikteta wa zamani wa nchi hiyo Yahya Jammeh. Uamuzi huo wa kihistoria umeagiza Sonko afukuzwe Uswizi kwa miaka 12 mara tu baada ya kukamilisha kifungo, na alipe fidia kwa raia. 

Taarifa ya mahakama imeeleza kwamba “imempata Ousman Sonko na hatia ya makosa mengi ya mauaji ya kukusudia, makosa mengi ya utesaji na hatia ya kutoa kifungo cha uwongo, makosa ambayo ni ukiukaji dhidi ya haki za binadamu.”ousman sonko

Soma zaidiVikao vya kusikiliza unyama wa Jammeh vyatimiza mwaka 

Mahakama yampata Ousman Sonko na hatia

Mahakama imeeleza kwamba, “Sonko alifanya uhalifu huu kama sehemu ya mashambulizi ya kimfumo dhidi ya raia. Katika uamuzi wake, mahakama imeamua kwamba, pamoja na kumpa Ousman Sonko hukumu ya kifungo cha miaka 20 jela, atafukuzwa kutoka Uswizi kwa miaka 12 mara baada ya kukamilisha kifungo hicho, na vilevile lazima alipe fidia kwa raia walalamishi “kwa maumivu yasiyo ya kimwili na mateso waliyopata”.

Hata hivyo mahakama imemuondolea mashtaka ya ubakaji. Sonko, mwenye umri wa miaka 55, na mshirika wa karibu wa Jammeh, amepatikana na hatia ya msururu wa makosa aliyoyatenda kati ya mwaka 2000 na 2016. Aliachishwa kazi mwaka 2016 baadaya kuhudumu kama waziri wa usalama wa ndani.

Gambia Banjul | Rais Yahya Jammeh
Rais Yahya Jammeh – 29.11.2016 Afisa wa Gambia akizungumza na Rais Yahya Jammeh wakati wa mkutano wake wa mwisho mjini Banjul, GambiaPicha: Jerome Delay/AP Photo/picture alliance

Sonko anaweza kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.Waziri wa zamani wa utawala wa Jammeh kupandishwa kizimbani Usisi

Alihukumiwa chini ya kanuni ya mamlaka ya ulimwengu, ambayo inaruhusu nchi kushtaki madai ya uhalifu dhidi ya ubinadamu, uhalifu wa kivita, na mauaji ya kimbari bila kujali ni wapi yalitendeka.

Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na uwasilishaji wa kesi katika mahakama za kimataifa, Trial International – liliwasilisha malalamiko na kusababisha kukamatwa kwa Sonko — na limesema kuwa yeye ndiye afisa wa ngazi ya juu zaidi kuwahi kuhukumiwa barani Ulaya kwa uhalifu wa kimataifa chini ya kanuni ya mamlaka ya ulimwengu.

Soma zaidi Gambia yaunda jopo la wataalamu kuchunguza jaribio la mapinduzi la wiki iliopita

Ujumbe mzito wa viongozi wanaokiuka haki za binadamu

Mkurugenzi mtendaji wa Trial International Philip Grant amesema uamuzi huo unatuma “ujumbe mzito dhidi ya tamaduni ya kutokujali (impunity)”. Amesema kupitia ukurasa wake wa X kwamba, “Wahalifu wa ngazi ya Waziri sasa wanaweza kufikiwa na haki,”.

Sonko alikanusha mashtaka na kuwashutumu walalamishi kwa kusema uwongo huku akilaani kifungo chake cha miaka saba kabla ya kesi, kifungo ambacho anasema kilihusisha kifungo cha upweke.

Sonko alikosana na Rais wa zamani wa Gambia Yahya Jammeh katika miezi ya mwisho ya utawala wake uliotajwa kama wa ukandamizaji. Jammeh aliyeongoza kwa miaka 22 alilazimika kukimbilia uhamishoni Equatorial Guinea mwezi Januari 2017 baada ya kushindwa katika uchaguzi wa Urais. Mwezi huo huo, Sonko alikamatwa Uswizi alikokuwa akitafuta hifadhi.

Reed Brody, mwendesha mashtaka ya uhalifu wa kivita anayehudhuria kesi hiyo ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba, “kutiwa hatiani kwa Ousman Sonko, mmoja wa nguzo za Utawala wa kikatili wa Yahya Jammeh, ni hatua muhimu katika safari ndefu ya kutafuta haki kwa waathiriwa wa Jammeh,”

Mwendesha mashtaka wa umma wa Uswizi alikuwa ametafuta kiwango cha juu zaidi cha adhabu ambacho ni kifungo cha maisha.

 

Related Posts