Serikali kuzihamisha kaya 1,712 KIA ifikapo Juni

Hai. Serikali imesema shughuli ya kuzihamisha kaya 1,712 za wilaya za Arumeru mkoani Arusha na Hai mkoani Kilimanjaro, zinazodaiwa kuvamia ardhi ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) itakamilika Juni 2024.

Kaya zinazopaswa kuondoka katika upande wa wilaya ya Hai ni 1,061 zilizopo viijiji vya Tindigani, Mtakuja, Chemka na Sanya Station, huku upande wa Wilaya ya Arumeru zikiwa ni kaya 651 ikijumlisha vijiji vya Malula, Kaloleni, Samaria na Majengo Kati, ambazo zitalipwa jumla ya fidia ya Sh11.3 bilioni.

Kati ya kaya 1,712 zilizopaswa kuhama, hadi sasa, kaya 46 bado hazijapokea malipo ya fidia kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kesi mbili za mirathi, kukosa akaunti za benki na kutofautiana kwa majina yaliyopo kwenye akaunti za benki.

Akizungumzia mchakato wa kuwaondoa wananchi katika eneo hilo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema baada ya Serikali kufanya tathmini, zilitolewa zaidi ya Sh11.3 bilioni kwa ajili ya kulipia maendelezo yaliyofanywa na wananchi hao kwenye eneo hilo la KIA ambalo ni la Serikali.

“Uthamini ulianza Novemba 17, 2022, idadi ya watathiminiwa kwa wilaya hizo mbili ni kaya 1,061 kwa wilaya ya Hai na 651 kwa wilaya Arumeru na Sh11.3 bilioni zitalipwa kwa waliohamishwa,” amesema Matinyi.

Amesema hadi kufikia Mei 14, 2024, wananchi 46 ndiyo walikuwa hawajapokea malipo yao.

“Serikali ingependa kumaliza jambo hili ifikapo Juni 2024 na muda ambao tumetarajia kusafisha mapagale (nyumba zilizoachwa) na kuweka maeneo katika hali yake inayostahili itakuwa imefikia mwisho wiki ijayo, lakini hatuwezi kulazimisha Mahakama kumaliza kesi za mirathi, zitaisha kwa wakati wake na haki itatendeka.

“Shughuli imefanyika vizuri na kwa amani, nimefika hapa kuja kuona ukweli kuhusu kinachozungumzwa na kuona eneo ambalo wananchi wanahama. Hadi sasa tulichokiona ni kwamba wananchi wameondoka kwa hiari yao baada ya kulipwa fedha za maendelezo waliyofanya,” amesema Matinyi.

Amesema wananchi wote waliohamishwa katika eneo, wamepelekwa katika vijiji na vitongoji jirani ikiwemo kitongoji cha Bonza, kilichopo Kijiji cha Tindigani.

“Eneo hili linabakia kuwa ni la uwanja wa ndege na wananchi wanaenda kuishi katika maeneo mengine ambao watafanya shughuli za maendeleo vizuri. Naishukuru Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini kwa kufanya kazi hii kwa weledi na kwa umakini mkubwa,” amesema.

Akitoa historia ya eneo hilo, amesema lilianza kumilikiwa na Serikali mwaka 1969 na wakati huo lilikuwa pori Tengefu la Sanya Lelatema, likiwa ni eneo lenye kilomita za mraba 800.

“Wakati huo Serikali ilitenga eneo la kilomita 110 kutoka 800 mahsusi kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huu wa ndege wa Kilimanjaro na baadaye eneo hilo lilipimwa rasmi mwaka 1989 kwa ramani namba E5255/18 na kusajiliwa na kupewa namba 231264 na hati ilipotoka lilianza kumilikiwa likiwa na hati namba 22270.

“Kati ya mwaka 2007 na 2010, wananchi wa jamii ya wafugaji kutoka wilaya hizo mbili walianza kuingia katika eneo hilo kuweka makazi na kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya eneo hilo, ikiwemo kilimo na na kuathiri shughuli za uendeshaji, hasa katika kipindi cha kiangazi.

Katika kipindi hicho, amesema vumbi kubwa hutimka katika eneo ambalo ni kame kutokana na majani mengi kuwa yametumika kama malisho na hivyo kuathiri uono wa marubani, kiasi cha ndege wakati mwingine kushindwa kutua na kulazimika kwenda kutua katika viwanja jirani,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Amiri Mkalipa amesema zaidi ya asilimia 95 ya wananchi wanaopaswa kupisha eneo hilo la uwanja wa ndege wa KIA wameshaondoka baada ya kulipwa fidia.

 “Kama Serikali tunaendeleza juhudi za kufanya wapate fedha zao kwa wakati, hakuna mwananchi yeyote wa Hai aliyelazimishwa kuondoka, wamekubali wenyewe kuondoka kwa amani,” amesema.

Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Tindigani, Nepapa Mollel ameishukuru Serikali kwa kuwapa muda wa kuondoka katika eneo hilo huku akiiomba kuwaboreshea miundombinu ya umeme na maji huko wanakohamia.

“Sisi hatubishani na Serikali, kikubwa tunachoomba ni huko tunakokwenda tuboreshewe huduma mbalimbali za maji, afya na malisho ya mifugo yetu, tupo vizuri na Serikali na tunaamini itatekeleza,” amesema.

Related Posts