Mamlaka nchini Ukraine zimesema watu 17 wamejeruhiwa katika shambulizi la anga la Urusi katika miji ya kusini mwa Ukraine ya Mykolaiv na Kherson huku shambulizi lingine la anga likiwaua watu wawili katika mji wa Dnipro. Wakati vita hivyo vikizidi kuchukua mkondo mpya Rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine ameahirisha safari zake zote za nje ili kupambana na hali mbaya ya vita inayoendelea kuzorota nchini humo.
Soma zaidi. Marekani yatangaza kitita kipya cha msaada kwa Ukraine
Urusi imeendeleza mashambulizi yake nchini Ukraine mapema hii leo kwa kushambulia miji kadha ya kusini mwa nchi hiyo.
Katika taarifa iliyotolewa na gavana wa mji wa Kherson kupitia mtandao wa Telegram ni kwamba watu 17 wamejeruhiwa kufuatia mashambulizi ya anga ya Urusi yaliyolenga makaazi ya watu na majengo ingawa jeshi la Urusi limepiga kuwa lililenga maeneo ya makaazi ya watu.
Kando na shambulio hilo, Urusi pia imefanya shambulizi lingine la anga katika mji wa Mykolaiv ambapo wahudumau wa huduma za dharura wamesema kwamba takriban watu 6 walijeruhiwa.
Marekani kutoa msaada zaidi kwa Ukraine
Kwa upande mwingine Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken ambaye yuko ziarani nchini Ukraine amesema Ukraine inaweza kuamua yenyewe iwapo itaamua kuyashambulia maeneo ya Urusi na kwamba Marekani haitoshiriki kwa maamuzi hayo ikiwa Ukraine itafanya hivyo.
Soma zaidi. Ukraine yaondoa vikosi vyake maeneo kadhaa ya uwanja wa vita
Waziri huyo pia ameongeza kuwa Marekani itaiongezea Ukraine dola bilioni 2 za kimarekani kwa ajili ya ufadhili wa kijeshi.
“Tutatoa dola bilioni 2 za ziada katika ufadhili wa kijeshi wa kigeni kwa Ukraine. Na tutaiweka hii pamoja katika mfuko wa kwanza wa aina yake wa biashara ya ulinzi, mpango huu una vipengele vitatu. Moja, ni kutoa silaha leo. Kwa hivyo hii itakuwa ni kuisaidia Ukraine katika kupata silaha hizo , mbili, ni kuzingatia vilevile katika jambo ambalo Dmytro(Kuleba) alilizungumzia hivi punde kwamba kuwekeza katika msingi wa viwanda vya ulinzi wa Ukraine, na kusaidia kuimarisha hata zaidi uwezo wake wa kuzalisha kile inachohitaji kwa ajili yake yenyewe, lakini pia kuiwezesha Ukraine kujipatia silaha na kuzalisha kwa ajili ya wengine” amesema Blinken.
Kwa sasa mzozo kati ya Ukraine na Urusi unazidi kuchukua sura mpya kila uchao na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amelazimika kusitisha safari zake za nje ili kuitupia macho hali ya kiusalama ambayo inazidi kuzorota nchini humo kufuatia mkururo wa mashambulizi ya Urusi.
Soma zaidi. Putin aunga mkono mpango wa China wa kuutatua mzozo nchini Ukraine
Katika mji wa kharkiv nchini Ukraine takriban watu 8,000 wamehamishwa wiki hii kutokana na mashambulizi ya Urusi, wengi wao wakiwa ni watoto, wazee na walemavu.
Hata hivyo, Rais wa Urusi Rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye yuko ziarani nchini China akigusia suala la vita vya nchi yake na Ukraine mbele ya waandishi wa habari amesema nchi yake iko tayari kwa mazungumzo na Ukraine ikiwa pande zote mbili zitazingatiua maslahi ya pande zote mbili.