Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia mkazi wa Kijiji cha Malya Tarafa ya Ibindo wilayani Kwimba mkoani humo, Fabian Pauline (32) kwa tuhuma za kumuua mtoto wake, Alvin Fabian (3) kwa kipigo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa, mtuhumiwa alitekeleza tukio hilo Mei 9 mwaka huu baada ya kumshambulia mtoto wake kwa kutumia fimbo na kumsababishia majeraha maeneo mbalimbali ya mwili wake, yaliyomsababishia kifo.
Kamanda Mutafungwa akizungumza leo Mei 15, 2024 na waandishi wa habari, amesema mtuhumiwa alifikia uamuzi huo baada ya kumkuta mtoto huyo amejisaidia haja kubwa na kujipaka maeneo mbalimbali ya mwili wake.
“Tukio hili lilitokea Mei 9, mwaka huu Saa 10:00 alasiri katika kijiji na kata ya Malya Tarafa ya Ibindo Wilaya ya Kwimba,” amedai Mutafungwa.
Amesema mwili wa marehemu baada ya kufanyiwa uchunguzi umekabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za maziko na upelelezi wa tukio hilo unaendelea, utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
Katika tukio lingine, Mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, Aman Manyama (31) amekutwa amefariki baada ya kudaiwa kujinyonga juu ya mti wa mwembe kwa kutumia kamba ya kuanikia nguo.
Mwili wa Aman ambaye ni mfanyabiashara, ulikutwa ukining’inia juu ya mti huo uliopo mbele ya nyumba ya babu yake anayeishi Mtaa wa Isenga ‘B’, Ilemela mkoani Mwanza jana Jumanne Mei 14, 2024.
Mutafungwa amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba chanzo cha kifo cha marehemu ni msongo wa mawazo kwa marehemu ambaye anadaiwa kuwa na maradhi ya muda mrefu.
“Aman alikuwa anasumbuliwa na maradhi mbalimbali na kulazwa katika Hospitali ya rufaa ya Kanda ya Bugando Mei 12, 2024 ambapo ilipofika Mei 13, mwaka huu aliruhusiwa kutoka katika hospitalini baada ya kupata nafuu. Kesho yake akakutwa amejinyonga nje ya nyumba hiyo,” amesema Mutafungwa.
Wakati huo, Jeshi hilo linamshikilia Mkazi wa Kijiji cha Kigungumule wilayani Magu mkoani Mwanza, Ezron Macheya (47) kwa tuhuma za kumjeruhi mtoto wake wa kike (8), akimtuhumu kuwa ana tabia ya kuzurura mitaani na kuchelewa kurudi nyumbani.
Macheya anadaiwa kutenda ukatili kwa mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza jana Mei 14, 2024.
Anadaiwa alimchapa kwa kutumia ubapa wa panga, fimbo na mkanda wa suruali maeneo mbalimbali ya mwili wake.
“Mtoto huyo, amepata michubuko sehemu mbalimbali za mwili wake na amepelekwa Kituo cha Afya Kisesa na mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani,” amesema Mutafungwa.
Kamanda huyo ameitaka jamii kuepuka tabia ya kutoa adhabu nzito kwa watoto, jambo linaloweza kugeuka na kuwa ukatili na wahusika hawatafumbiwa macho.