Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amesema hakujawahi kuwa na hati ya kusafiria kutoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam wala mkoa wowote bali kilichokuwepo ni hati maalumu.
Masauni amesema hayo akijibu hoja ya mbunge wa Konde, Mohamed Said Issa ambaye alitaka utaratibu wa kutumia hati ya kusafiria kwa mtu anayeingia Zanzibar urejeshwe.
Akijibu hoja zilizotolewa na wabunge waliochangia bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/25 bungeni leo Mei 15, 2024, Masauni amesema wabunge na wananchi wafahamu utambulisho wa nchi ni mali ya wananchi wenyewe.
Amesema hati ya kusafiria ni utambulisho kuwa mtu ni raia wa nchi gani. Amesema Katiba katika ibara ya 17 inatoa uhuru wa Mtanzania kutoka eneo moja kwenda lingine.
Masauni amesema Mtanzania ana haki ya kwenda popote, ndiyo maana hatutumii hati ya kusafiria kwa ajili ya mzunguko au matembezi ya ndani ya nchi.
“Mbunge anapotoa hoja hati ya kusafiria irudishwe ni kukosa uelewa tu, hakujawahi kuwa na hati za kusafiria, kilichokuwapo ni matumizi ya hati maalumu kwa ajili ya masuala ya usalama na hadi leo bado zinatumika. Tofauti ni mabadiliko ya wakati tu,” amesema.
Waziri Masauni amesema hadi leo mtu anapotaka kusafiri kutoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam au Dar es Salaam kwenda mikoa mingine anahitajika kutoa Kitambulisho cha Taifa (Nida).
Amesema hiyo haina maana kuwa ni hati ya kusafiria bali ni kwa ajili ya usalama.
“Nataka ieleweke si sawa kujenga taswira au kuhamasisha Watanzania kuwa ndani ya nchi moja kuna matumizi ya pasipoti kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine Tanzania. Ni nchi moja na wananchi ni wamoja,” amesema.
Mbali na hilo, Masauni amesema Serikali ina mpango wa kuliimarisha na kulifanya Jeshi la Polisi liwe la kisasa kwa kuanza kutumia njia ya mifumo. Amesema ipo mifumo zaidi ya 22.
Amesema katika kutekeleza maoni ya Tume ya Haki Jinai, Jeshi la Polisi limetayarisha mfumo ambao umesaidia kuondoa changamoto ya muda mrefu ya watu kubambikiwa kesi.
Amesema mfumo huo unasaidia kuhakikisha mtu yeyote anayetoa taarifa katika kituo cha polisi, taarifa zake zinasomeka kwa wadau wote wa haki jinai.
Masauni amesema mfumo huo ambao umefungwa na wataalamu wa ndani ya jeshi hilo, unatumika katika vituo 23. Lengo ni kuufunga katika vituo vyote.
Kuhusu madeni, Masauni amesema mwaka huu zimetolewa Sh15 bilioni kupunguza madeni ya Jeshi la Polisi yanayofikia Sh77 bilioni.
Masauni amesema ni imani yake malengo ya Rais ya kuhakikisha anaongeza mshahara, posho, haki na stahiki za askari yatafikiwa.
“Hoja ambayo imekuwa ikiwagusa kwa muda mrefu waheshimiwa wabunge ya kuangalia kikokotoo kwa maana ya pensheni, Rais ameshalitolea maelekezo na yenyewe inaenda kupewa suluhisho,” amesema.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo amesema Serikali imetenga Sh1 bilioni katika mwaka 2024/25 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kisasa vya upekuzi katika magereza matano nchini.
Amesema vifaa hivyo vitafungwa katika magereza matano ya Karanga mkoani Kilimanjaro, Maweni (Tanga), Lilungu (Mtwara), Uyui (Tabora) na Ruanda (Mbeya).
Bunge limepitisha bajeti ya Sh1.7 trilioni kwa ajili ya Wizara ya Mambo ya Ndani Nchi kwa mwaka 2024/25.