Dar es Salaam. Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania PLC imeutangazia umma na wateja wake kurejesha huduma za kimtandao kikamilifu, ikieleza walioshindwa kutumia huduma ya intaneti watarejeshewa vifurushi vyao.
Kwa muda wa siku nne mfululizo nchini watumiaji wa huduma za mtandao walipata changamoto kutokana na kupungua ubora wa intaneti kulikosababishwa na kukatika nyaya za mkongo wa mawasiliano chini ya bahari.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 15, 2024, Vodacom imesema:
“Tunaelewa tukio hili limeleta usumbufu, tunaomba radhi kwa hilo. Kwa sababu hii, wateja wote walioshindwa kutumia huduma ya intaneti watarejeshewa vifurushi vyao. Tunaendelea kufuatilia kwa karibu na kuhakikisha unapata huduma bora na kasi ya juu kabisa.”
Vodacom imesema katika dhamira yake endelevu ya kuwawezesha watu kupitia mtandao huo, wateja ambao walikuwa na vifurushi ambavyo havikutumika watarejeshewa.
Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire amesema, “sisi tutoe shukrani zetu kwa watoa huduma walioshirikiana nasi kurejesha huduma.”
Amesema kampuni hiyo bado inajitolea kutoa muunganisho wa kuaminika na usiokatizwa kwa wateja wake.
“Juhudi zinazoendelea zimewekwa ili kudumisha viwango vya juu zaidi vya huduma na ubora unaotakiwa,” amesema.
Mapema leo bungeni, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema hali ya upatikanaji wa mtandao wa intaneti nchini ilikuwa imefikia zaidi ya asilimia 80 na kuwa hadi mchana wa leo huduma zingerejea kwa kiwango cha kuridhisha.
Nape ameyasema hayo wakati akitoa maelezo kuhusu mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Makete, Festo Sanga aliyekuwa akitaka maelezo kuhusu nafasi za ajira ajira za Jeshi la Polisi ambazo uombaji wake umetatizwa na kukosekana kwa intaneti.
Pamoja na majibu ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad yusuf Masauni kuwa wameongeza siku tano kuanzia kesho kukabiliana na hali hiyo, Nape:
“Tulikuwa tukipitia changamoto kubwa ya upatikanaji wa mtandao, hivi tunavyozungumza upatikanaji upo zaidi ya asilimia 80, tunategemea leo (Mei 15, 2024) kufikia mchana tutakuwa tuko katika hali nzuri” amesema Nape.
Tangu Jumapili Mei 12, 2024 Tanzania na nchi nyingine kadhaa, zilipata tatizo la kukatika kwa mtandao intaneti kutokana na hitilafu iliyotokea kwenye mkonga wa mawasiliano uliopo baharini, hali iliyoathiri shughuli nyingi zinazohitaji mtandao huo.