Taarifa ya jeshi laUkraine imeeleza kuwa kutokana na mapigano makali, limeamua kuwahamishia wanajeshi wake katika maeneo ya Lukyantsi na Vovchansk ili kunusuru maisha ya askari wa Ukraine na pia kuepuka askari wake kujeruhiwa katika mapigano hayo mapya yanayoendelea katika eneo la Kharkiv.
Ukraine inayokabiliwa na ukosefu wa silaha na askari wa kutosha, inajaribu kuzuia mapambano zaidi kutoka upande wa Urusi.
Soma Zaidi: Putin aunga mkono mpango wa China wa kuutatua mzozo nchini Ukraine
Wakati huo huo Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema mfumo wake wa ulinzi wa anga umefanikiwa kuyadungua makombora 10 yaliyorushwa na Ukraine. Wizara hiyo ya ulinzi ya Urusi imeserma makombora ya Marekani yalililenga eneo la Crimea mapema leo wakati ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa MarekaniAntony Blinken alipokuwa akizuru Kyiv.
Gavana wa mji wa Belgorod Vuacheslav Gladkov, amesema watu wawili wamejeruhiwa katika kijiji cha Dubovoye baada ya nyumba yao kuteketea kutokana na kushambuliwa kwa roketi.
Mashambulizi hayo ya Ukraine yanafanyika wakati ambapo wanajeshi wa Urusiwakiendeleza mashambulizi katika jimbo la kaskazini-mashariki mwa Ukraine yaliyoanza wiki iliyopita, mashambulizi hayo ni makubwa tangu Urusi ilipoivamia Ukraine miaka miwili iliyopita.
Urusi pia imesema imeufunga kwa muda uwanja mkubwa wa ndege karibu na mji wa Kazan, ulio kilomita 1,000 kutoka Ukraine, baada ya eneo hilo kulengwa na ndege isiyo na rubani ya Ukraine.
Soma Zaidi: Ujerumani na nchi za Nordic zaahidi kuendelea kuiunga mkono Ukraine
Vikosi vya Ukraine katika wiki za hivi karibuni vimeongeza mashambulizi ya angani katika maeneo ya mpakani kati ya Ukraine na Urusi lakini pia wameweza kushambulia maeneo yaliyo ndani kabisa ya ardhi ya Urusi.
Kutokana na mapigano mapya nchini Ukraine Rais Volodymyr Zelenskiy ameahirisha ziara yake katika nchi za Uhispania na Ureno. Mfalme Felipe wa Uhispania alipanga kufanya dhifa ya chakula kwa heshima ya rais Zelenskiy tarehe 17 Mei.
Zelenskiy pia alitarajiwa kusaini mkataba wa pande mbili wa makubaliano ya ushirikiano wa usalama na Waziri Mkuu wa Ureno Pedro Sanchez kufuatia tamko la pamoja la NATO lililotolewa mwaka jana.
Soma Zaidi: Blinken: Msaada wa kijeshi kwa Ukraine utawasili hivi karibuni
Mengineyo ni pamoja na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi Maria Zakharova ameuonya Umoja wa Ulaya hii leo Jumatano kwamba iwapo kambi hiyo itaviwekea vikwazo vyombo vya habari vya Urusi basi waandishi wa habari wa Magharibi walio nchini Urusi nao watakabiliwa na majibu ya haraka, yaliyo makali kutoka kwa serikali ya Urusi.
Vyanzo: DPA/AP/AFP/RTRE