Wanaodaiwa kumlawiti mtoto wa miaka mitatu mbaroni Arusha

Arusha. Watu ambao idadi yao haikutajwa wanaotuhumiwa kumlawiti mtoto wa miaka mitatu katika Kata ya Muriet, jijini Arusha wamekamatwa.

 Kukamatwa kwao kunatokana na agizo la Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda alilolitoa mwishoni mwa wiki wakati akihitimisha siku tatu za kliniki ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Makonda alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Arusha na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha kufuatilia suala hilo.

Alitoa maagizo hayo baada ya mama wa mtoto huyo, kulalamika kuwa watuhumiwa anaodai waliomlawiti mtoto wake waliakamatwa na Polisi na baadaye waliachiwa bila kufikishwa mahakamani.

“Askari wote waliokupa kauli ambazo siyo nzuri nijue majina yao, OCD hakikisha ulinzi wa huyu dada na mganga mkuu wa mkoa nakuagiza, fuatilia kote huyu mama alikopita na mtoto wake akapimwa, nataka hiyo ripoti na atafutiwe dawa ili apone,” alielekeza Makonda.

Mama huyo alisema hajui kwa nini watu hao waliachiwa ilhali mwanawe hali yake inazidi kuwa mbaya, akidai hivi sasa anajisaidia damu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 15, 2024 ofisini kwake, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerewa amesema baada ya kufuatilia, tayari wanaodaiwa kutekeleza jambo hilo wamekatamatwa na Jeshi la Polisi (bila kutaja idadi yao).

“Katika kliniki ile kulikuwa na maelekezo  mbalimbali, moja ni la kuwakamata watu wote wanaodaiwa kumlawiti mtoto wa miaka mitatu, tumewabaini na tumewakamata tayari, hatua za kisheria zinaendelea na mtoto anaendelea na matibabu,” amesema Mtahengerwa.

Amesema kliniki hiyo iliyoanza kufanyika Mei 8 hadi 10, 2024, ilipokea malalamiko mengi na jana walianza kuyafanyia kazi.

Amesema kati ya mashauri 54, mashauri 37 yamepatiwa ufumbuzi na mengine wanaendelea kuyafanyia kazi.

Akiwa katika baraza la wazi la kusikiliza mashauri ambayo hayajapatiwa ufumbuzi katika kliniki ya Makonda, Witness Simon, mama wa mtoto huyo alitoa kilio chake mbele ya Makonda akidai baada ya mwanawe kulatiwa alienda Kituo cha Polisi Muriet kuchukua fomu namba tatu ya polisi (PF3).

Akaenda Kituo cha Afya Muriet na baadaye Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru na kote walithibitisha kuwa mwanawe kalawitiwa zaidi ya mara mbili, lakini polisi hawajawahi kufuatilia kesi yake zaidi ya kumfukuza na kumgombeza akienda kuulizia.

“Hata walivyokamatwa watuhumiwa walilala ndani siku moja wakaachiwa, wakanifuata nyumbani kwangu wakaniambia kama sina nyota ya kutembea na askari nitabaki sana, mtoto wangu ana miaka mitatu namfunga pampesi anajisaidia damu,” alidai mama huyo.

Alidai hata siku ya kwanza alipoenda kwenye kliniki hiyo alitishiwa kuuawa na watu asiowafahamu na alipoenda dawati la jinsia la Polisi kuonana na askari wanaotoka Kituo cha Muriert, walimpatia nauli wakamwambia arudi kituoni suala lake litafanyiwa kazi.

“Nikaenda wakaniambia kila siku ni kurudi hapa, unarudi kutafuta nini, nikawaambia mtoto wangu bado anaumwa wakaniambia ndiyo uje kusumbua watu hapa, hujielewi wewe nikaondoka. Hata RB yangu walininyang’anya,” alidai mama huyo.

Related Posts