AKILI ZA KIJIWENI: Mudathir hajahitaji kubebwa na uzawa

MCHEZO wa soka ni wa kitimu lakini hilo halipaswi kuwa kigezo cha mchezaji binafsi kubweteka au kusubiria kupata nafasi kwa huruma.

Yaani sio kwa sababu ni mchezo wa kitimu, basi mchezaji apewe tu nafasi ya kucheza kwa vile tu timu imesajili idadi fulani ya wachezaji hata kama haonyeshi kama anastahili kupewa hiyo nafasi.

Mara kwa mara kwenye ligi yetu kumekuwa na malalamiko uwepo wa wachezaji wa kigeni umekuwa ukichangia kunyima nafasi ya kucheza wachezaji wazawa na wengine kudiriki kusema wanaporomoshwa viwango vyao.

Hili hutokea zaidi katika timu kubwa hapa nchini ambazo huwa zinasajili idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni na kikanuni, timu inaruhusiwa kuwa nao wasiozidi 12.

Lakini wapo wachezaji wazawa ambao hawajataka kuingia katika mtego wa kusubiri huruma ya umma ili wapate nafasi ya kucheza kwenye timu zao na badala yake wameamua kupambana hadi kushawishi mabenchi ya ufundi ya timu zao.

Mfano wa wachezaji hao ni kiungo wa Yanga, Mudathir Yahya ambaye pamoja na uwepo wa wachezaji wa kigeni amekuwa tegemeo kubwa la timu hiyo licha ya uwepo wa wachezaji wa kigeni ambao wanacheza katika nafasi yake.

Mara nyingi msimu huu ameifungia mabao muhimu timu yake ambayo yameamua matokeo ya Yanga, pia amekuwa akipiga pasi za mwisho ambazo wenzake wamekuwa wakizitumia kufunga mabao.

Mudathir hajataka kuingia katika mtego wa kuona hapangwi kwa sababu kwenye timu yake wapo wageni bali ameamua kupambana katika viwanja vya mazoezi na vile vya mechi ili awe na ubora ambao leo unamzalia matunda.

Anachokifanya Mudathir Yahya kinazidi kufuta ile dhana, kinachorudisha nyuma wachezaji wazawa ni uwepo wa wageni bali ni kiwango chao binafsi cha juhudi za kusaka mafanikio yao.

Wazawa wavuje jasho kupigania nafasi hakuna kinachoshindikana kama anavyoonyesha Mudathir Yahya.

Related Posts