UWEZO wa kupiga mashuti ya mbali, anaoonyesha winga wa Simba, Edwin Balua, nyuma ya pazia anafanya zoezi la kupiga mipira nje ya 18 ya uwanja kabla ya mechi.
Katika stori za hapa na pale alizopiga na Mwanaspoti, Balua amesema akiwa mazoezini anapenda kufunga kwa kupiga mashuti ya mbali, jambo linalomjengea kujiamini wakati wa mechi, kutokuogopa kufunga akiwa mbali.
“Unajua hakuna kinachoshindikana chini ya jua, kitu unachokifanyia mazoezi mara kwa mara inakuwa rahisi kukifanya bila uoga wakati wa kuipambania timu, kwani mabao ya kufungia mbali inakuwa ni kushitukiza,” amesema.
Kabla ya kujiunga na Simba kwa usajili wa dirisha dogo, Balua aliyowahi kuifunga timu hiyo bao la nje ya 18, ulikuwa mpira wa kutengwa shuti lake likamshinda kipa Ally Salim, ilikuwa Oktoba 5, 2023, Uwanja wa Azam Complex.
Balua kwa sasa anamiliki mabao manne, mawili akitoka nayo Prisons akiifunga Simba, Mtibwa na aliyofunga akiwa na Wanamsimbazi ni dhidi ya Namungo lilikuwa shuti la mbali na Tabora United.