Dk Bagonza ataja kasoro za demokrasia

Unguja. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza amezitaja kasoro 10 za mfumo wa kidemokrasia nchini,  huku akisema kukosekana kwa demokrasia ni hatari kwa Taifa na mtu mmoja mmoja.

 Mbali na kasoro hizo, kiongozi huyo wa kiroho amesema licha ya nia njema ya Rais Samia Suluhu Hassan kutengeneza ‘4R’ lakini zinashindwa kuendelea badala yake zimekwama, akitaja wanaomzunguka kiongozi huyo kuwa kikwazo.

 Wakati akitaja mambo hayo, wadau wa siasa na demokrasia wamepigilia msumari kuonyesha mkwamo huo, wakitaja suluhu ya mambo hayo ni kuwa na Katiba mpya lakini maoni yao yanapuuzwa.

 Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Zanzibar, Dk Muhamed Dimwa amesema chama hicho kipo mstari wa mbele kujenga maridhiano lakini Katiba mpya sio kipaumbele cha wananchi.

 Hayo yalijiri jana Zanzibar katika Jukwaa la Demokrasia Tanzania 2024 kuelekea demokrasia jumuishi na shirikishi. Wadau mbalimbali wa demokrasia walishiriki jukwaa hilo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

 Katika mada yake kuhusu demokrasia ya maendeleo: Ukatiba na Ujumuishi, Dk Bagonza amesema mfumo wa demokrasia uliopo unaruhusu mtu kupiga kura lakini si kuchagua, unawezesha wanaochaguliwa kuwa juu ya wanaochagua kuliko kinyume chake.

 “Unaruhusu mtu kutoa mawazo yake lakini si kumhakikishia ulinzi ndani au nje ya chama chake, unaruhusu udikteta wa mtu au kundi moja uliofichwa ndani ya chama,” amesema.

 Pia, amesema unaruhusu wenye fedha kuwa na uamuzi juu ya wasio na fedha na unawanyima haki watu wasio na vyama kutawaliwa na wenye vyama, unawanyima wananchi kuwawajibisha watawala lakini mfumo unawapa uhuru wananchi kuwasumbua kwa kuwaomba fadhila binafsi.

 Ametaja kasoro nyingine, unaimarisha utulivu unaoitwa amani na kuruhusu wachache kuchezea utawala wa sheria (rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma), huku ukishindwa kutoa uhuru wa mihimili yote kujitegemea bali mhimili mmoja usiojitegemea kutawala mihimili isiyojitegemea zaidi.

 Amesema umeimarisha mashaka ya kudumu kwa makundi yote, watawala, watawaliwa, wanasiasa na wasio wanasiasa, wanaounga mkono Muungano na wanaoupinga, wanaotaka chama kimoja na wanaotaka vingi; mashabiki wa udikteta wa maendeleo na wale wa uhuru usio na maendeleo. 

 Amesema hicho ndicho chazo cha kujisimika kwa tabaka tawala ambalo halioni usalama nje ya madaraka.

 Katika maelezo yake, Dk Bagonza amesema:“Rais Samia amejitahidi sana kuonyesha njia ya kutuondoa katika mkwamo wa kidemokrasia lakini nina kila sababu kusema mawazo yake yametekwa na watu nisiowajua, wanaojaribu ama kuyapotosha au kuyatumia kuchelewesha ili mkwamo huu uendelee na baadaye waje kumlaumu Rais Samia.”

 “Kimsingi, hakuna kundi hata moja lina uhakika na usalama wake wa kudumu katikati ya mkwamo huu. Ni sawa na kufuga chatu kwenye chupa. Itapasuka na kuleta sintofahamu,” amesema. 

 Amesema kukosekana kwa demokrasia na maendeleo ni hatari kwa kila mtu na ndiyo maana kila mahali pasipo na demokrasia ya kweli, wajanja wachache huficha mali zao na familia zao nje ya nchi.

‘’Natamani uongozi uliopo utuepushe na zimwi hili linaloweza kutugeuka na kutumeza,’’ ameeleza. 

 Amesema msingi wa mfumo uliopo wa kisiasa na kidemokrasia unategemea sana hekima ya mtu binafsi kuliko mfumo.

‘’Si wakati wote tuna uhakika wa kuwa na viongozi wenye hekima hiyo. Kosa dogo la kuchagua linaweza kututumbukiza katika giza nene na tusijue namna ya kutoka,’’ amesema.

Kiongozi huyo wa dini amesema Rais Samia alipoingia madarakani aliasisi falsafa ya R4 yaani Maridhiano, Mabadiliko, Ustahimilivu na Kujenga Upya.

Samia aliyekuwa makamu wa Rais kuanzia Novemba 5, 2015, aliapishwa kuwa Rais Machi 19, 2021, baada ya kifo cha Rais John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021, katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya moyo.

 “Ukichunguza kwa makini matofali haya manne yanayojenga falsafa ya Rais Samia, huwezi kuacha kuona kuwa kuna kitu kilikwenda mrama katika maisha ya kisiasa ya Taifa hili,” amesema.

 Hata hivyo, amesema kauli hiyo ikichukuliwa kama kauli mbiu ya kisiasa litakuwa halitendewi haki Taifa na yanayoweza kutokea mbeleni. 

“Ujasiri huu wa Rais Samia, ni toba ya kiungwana inayohitaji kufanyiwa kazi kwa umakini uliojaa uzalendo. Hata hivyo, falsafa zake zimekwamishwa na watu nisio wajua,” amesema Dk Bagonza.

Baadhi ya washiriki wa jukwaa hilo

 Kiongozi huyo wa kiroho ambaye ni mjuvi wa maneno alisema: “Ukiangalia tumehimili mipasuko ipi? Mbona U-Tanganyika, Uzanzibari, Uzanzibara, udini, uchawa na uchama, vinaongezeka badala kupungua?”

 “Tumebadili nini? Mbona badala ya kubadili sheria tumebadili maneno na majina tu? Tunajenga nini? Mbona tunakusanya kuni za kuchomana? mbona tunajenga Tanganyika isiyo na Tanzania na Zanzibar isiyo na Tanzania? 

Mbona Tanzania inapwaya mbona ione mabomu ndipo iimarike? mimi naamini, kujenga wakati mwingine hujumuisha kubomoa hata kama si kila kubomoa kunajenga,” amesema Bagonza

Walichosema Lipumba, Mbowe

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba amesema utafiti uliofanywa na taasisi ya Freedom House ya nchini Marekani tangu mwaka 2006, demokrasia Tanzania na duniani kote imeshuka kwa asilimia 66 na mwaka 2021 Tanzania imeshuka mpaka asilimia 34.

 Profesa Lipumba ambaye ni mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD),  amesema mwaka 2022 walikuwa na mkutano wa TCD kuhusu namna  sheria vyama vya siasa inavyoweza kubadilishwa na Tume huru ya uchaguzi.

 Kadhalika, amesema Agosti 2023 walifanya mkutano mwingine, wakapendekeza kuwa wanahitaji kuwa na katiba mpya lakini iwapo inawezekana isipatikane kabla ya uchaguzi basi yafanyike marekebisho madogo ili matokeo ya Rais yapingwe mahakamani.

 Kwa mujibu wa Profesa Lipumba,  Serikali ilipeleka miswada bungeni lakini mabadiliko madogo ya Katiba hayakufanyika hivyo kama kupuuza maoni yao.

 “Wajumbe wote wa Tume wameshateuliwa na Katiba ya sasa inasema mjumbe wa Tume hawezi kuondolewa mpaka amalize kipindi cha miaka mitano hivyo mpaka mwaka 2026 ndio watamaliza muda wao,” amesema. 

 Hata hivyo, amesema hawana sababu ya kukata tamaa ili mambo hayo yafanyiwe marekebisho kwani demokrasia ni kitu muhimu.

“Kama hakuna demokrasia sio tu wapinzani wanaoathirika lakini hata wanachama wa chama tawala wanathirika,” amesema.

 Naye Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe,  amesema jambo linalohitajika katika nchi ni kuwa na katiba inayotibu majeraha hayo.

 Amesema wakati Rais Samia akianzisha 4R waliona kama jambo jema lakini limebaki, hawazingatii hivyo ipo haja mkuu huyo wa nchi chama chake kukubali mawazo mbadala na kuzingatia maoni yanayotolewa.

 “Kwamwe huwezi kutofautisha demokrasia na maendeleo, lakini kwa zaidi ya miaka 30 tangu kupata mfumo wa vyama vingi kama taifa halijapata faida ya vyama vingi kwasababu mfumo wenyewe hauruhusu,” amesema

Amesema uwepo vyama vya siasa ni namna bora kupeleka mambo mbele yapo maeneo vyama hivyo vinaweza kukubaliana lakini na maeneo mengine vikapingana ila kikubwa ni kuwa na fikra tofauti

 “Tatizo kubwa la nchi yetu tunakuwa na chama kimoja ambacho kinaamini kinahodhi fikra zote ambazo kinaweza kupeleka taifa hili mbele,” alisema Mbowe.

 Alisema mawazo yanayowasilishwa na makundi mbalimbali lakini hayapewi heshima kama inavyotakiwa kwasababu ya mfumo uliopo.

 Kuhusu Rais Samia kuwa na nia njema lakini anaangushwa na wanaomzunguka, Mbowe amesema kinachotakiwa ni kuwa na sheria na katiba badala ya kutegemea hisani ya mtu kwa hiyo hata Samia hawezi kuondoka kwenye lawama hizo kwani ndio kiongozi wa chama tawala.

 “Hatuwezi kugusia masuala ya demokrasia bila kugusia masuala ya katiba na uchaguzi, kwahiyo msingi mkuu ni kuwa na katiba mpya haya yote yatakwisha,” alisema Mbowe.

 Amesema Katiba imebeba mambo muhimu haki za watu na masuala ya uchaguzi hivyo ipo haja ya kuendelea kuangalia bila kuchoka.

CCM: Tupo mstari wa mbele

Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar, Dk Muhamed Dimwa,  amesema chama hicho kipo mstari wa mbele katika maridhiano na kuleta mabadiliko,  na kwamba jambo hilo linafanyika katika serikali zote zinazoongozwa na chama hicho.

 Hata hivyo, amesema masuala ya mabadiliko ya katiba yana michakato zake huku akisema kwamba suala la katiba mpya sio mpya sio kwamba itatatua matatizo yote ya wananchi na kwamba wananchi kwa sasa kipaumbele chao sio Katiba mpya bali wanataka maendeleo.

 Kuhusu 4R za Samia amesema hawawezi kuzijenga ikiwa watatiliana hofu na mashaka,  bali wanatakiwa kushikamana na kuwa na umoja wa kitaifa ili kujenga R4 kwa mustakabali wa Taifa.

 “Tusiwe na hofu, tushikamane twende mbele tunapotaka kufika, Katiba siyo ya vyama ni ya wananchi, na katiba sio suluhiso bali maendeleo na utulivu wa wananchi,” amesema.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Doroth Semu,  amesema kutokana na 4R za Rais Samia waliona kama kuna mwelekeo lakini matokeo yake wanapuuza maoni ya wananchi.

 “Hizi 4R za Rais Samia kuna vitu vinapuuzwa, kwa sababu kinachpendekezwa kinapuuzwa hakifanyiki kukamilika kwahiyo inakuwa shida kidogo,” amesema.

Alitolea mfano mabadiliko ya uchaguzi wa serikali za mitaa badala ya kusimamiwa na Tamisemi, walitaka badala yake usimamiwe na Tume Huru ya Tiafa ya Uchaguzi,  lakini imebaki miezi minne hakuna sheria iliyopelekwa bungeni kubadilisha.

 “Unaona huku ni kupuuzwa kwa makusidi mambo ambayo tumeshakubaliana lakini hayatekelezwi badala yake tunaendelea hivyo hivyo,” amesema.

Related Posts