Zelensky amesema aliyevamia mkoa huo wa Kharkiv ataangamizwa kwa namna yoyote na kwa kutumia rasilimali zilizopo, huku akisifu ufanisi wa vikosi vyake na kusisitiza kuwa wanaendeleza pia mapambano katika mji wa Kupyansk, katika mkoa wa Donetsk na pia katika mji wa Vovchansk karibu na mpaka wa Urusi.
Rais Zelensky ambaye amelazimika kuahirisha safari zake zote za nje kutokana na vita hivyo kushika kasi, na ambapo wiki hii alitarajiwa kufanya ziara katika mataifa ya Ureno na Uhispania amesisitiza kuwa ikiwa Ukraine itawezeshwa kikamilifu, ni wazi kwamba watamshinda adui.
Soma pia: Urusi yaendeleza mashambulizi zaidi kwa Ukraine
Katika ujumbe wake wa video ambao amekuwa akiutoa kila usiku, Zelensky amesema: “Dunia ina nguvu, ina silaha, ina uwezo wa kuilazimisha Urusi kurejea kwenye amani, amani ya haki. Ni lazima hatua zote zichukuliwe ili kuhakikisha kwamba uvamizi wa Moscow na jaribio lake la kuzidisha mashambulizi vinakomeshwa.”
Uingereza yazitolea wito nchi washirika wa Ukraine
Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Grant Shapps amesema washirika wa Ukraine wamekuwa “wakipuuzia” matukio ya vita na kwamba mafanikio inayoyapata Urusi huko Kharkiv ni lazima yachukuliwe kama “wito unaoashiria hatari” kwa kuwa jeshi la Moscow limesonga mbele katika maeneo ya kaskazini-mashariki kutokana na ukosefu wa silaha na wanajeshi wa kutosha nchini Ukraine.
Soma pia: Marekani yatangaza kitita kipya cha msaada kwa Ukraine
Katika siku za karibuni, Urusi imekuwa ikizidisha mashambulizi yake katika maeneo ya kusini na kaskazini-mashariki mwa Ukraine. Katika mji huo wa kharkiv karibu watu 8,000 wamehamishwa wiki hii kutokana na mashambulizi ya Urusi.
Hayo yanajiri wakati Rais wa Urusi Vladimir Putin amewasili China leo Alhamisi kukutana na mwenzake Xi Jinping akitafuta uungwaji mkono zaidi kutoka Beijing katika juhudi zake za vita nchini Ukraine lakini pia kufufua uchumi wake unaokabiliwa na vikwazo vya nchi za Magharibi.
(Vyanzo: Mashirika)