Dar es Salaam. Ubalozi wa India nchini umekutana kwa mazungumzo na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (Pura) kupata taarifa kuhusu vitalu vya utafutaji mafuta na gesi asilia.
Mazungumzo hayo yamefanyika jana Mei 15, 2024 katika ofisi za Pura na kuhudhuriwa na Katibu wa Pili wa Balozi wa India nchini Tanzania (Masuala ya Biashara), Narender Kumar na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Pura, Danstan Asanga.
Kumar amesema baada ya kusikia mpango wa Serikali wa kunadi vitalu vya mafuta na gesi asilia kupitia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2024/25, ubalozi wa India nchini Tanzania umeona ni vyema kukutana na mamlaka husika kufahamu kwa mapana kuhusu suala hilo ili kutoa taarifa kamili kwa kampuni na wadau katika Taifa hilo.
“Ni matumaini yetu kuwa kampuni kutoka India zitavutiwa na taarifa hii ndiyo sababu tumeamua kutafuta taarifa zaidi zitakazowasaidia kufanya maamuzi ya kushiriki na hatimaye kuwekeza katika shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini Tanzania,” amesema.
Akizungumzia duru ya tano ya kunadi vitalu, Asanga amesema Pura kwa niaba ya Serikali imeendelea na maandalizi.
Amesema tayari wamekamilisha maandalizi ya mkataba kuhusu uzalishaji na ugawanaji wa mapato ambao umewasilishwa Wizara ya Nishati kwa hatua zaidi.
Kazi zingine zilizofanyika amesema ni uwekaji wa mipaka ya vitalu vitakavyoingizwa katika mnada baada ya kupata ridhaa ya Wizara ya Nishati na maandalizi ya vifurushi vya data za petroli.
Asanga ameema mapitio ya Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 yanaendelea ili kuangalia vifungu vinavyohitaji maboresho na kwamba, Pura inashiriki kwenye mapitio hayo.
Amesema kazi ya kunadi vitalu itafanyika baada ya kukamilika kwa maandalizi ya msingi, ikiwamo mapitio ya Sheria ya Petroli 2015 na kuwa mpango wa Serikali ni kuzindua duru hiyo mwaka huu.
Pande hizo pia zimejadili kuhusu uwezekano wa kuanzisha mashirikiano baina ya mamlaka za udhibiti wa utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia kwa upande wa Tanzania na India.
Mbali ya hayo, wamejadili uwezekano wa kushirikiana katika programu za kujenga uwezo kwa watumishi katika masuala ya mafuta na gesi asilia kupitia ufadhili wa Serikali ya India.