JKT yaongeza mahanga kwa vijana

Kigoma. Jumla ya vijana 14,100 watapatiwa nafasi katika mahanga 141 yaliyojengwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kurekebisha mahanga ili waweze kuchukua vijana wengi zaidi.

Itakumbukwa wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya JKT, Rais Samia aliitaka Wizara ya Ulinzi kuandaa mpango mkakati wa kurekebisha makambi yote sambamba na kuongeza mahanga yatakayokuwa yanatumiwa na vijana wanaojiunga na JKT.

Akizungumza na Mwananchi Digital baada ya ukaguzi wa ujenzi wa mahanga hayo katika vikosi vya Mkoa wa Kigoma, Mwenyekiti wa Kamati ya Kimkakati ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema ujenzi huo umefanyika kwa kipindi cha miaka mitatu.

“Kwa muda wa miaka mitatu imeweza kuongeza uwezo wa kuchukua vijana 14,100 kwa kujenga mahanga 141,” amesema Brigedia Jenerali Mabena.

Ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha za maendeleo kwa ajili ya kuhakikisha miundombinu na majengo yanajengwa ili kuwezesha kuchukua vijana wengi wa Kitanzania kwa mujibu wa sheria na wale wa kujitolea.

Amesema tangu kurejeshwa kwa mafunzo ya lazima, Serikali imeongeza uwezo wa kuchukua vijana kutoka 5,000 hadi 50,000 kwa wakati mmoja.

Ametoa mfano wa Kikosi cha Kanembwa kilichoko Wilaya ya Kakongo Mkoani Kigoma, ambacho awali kilikuwa na uwezo wa kuchukua vijana 1,000 lakini hivi sasa kina uwezo wa kuchukua vijana kati ya 4,000 hadi 5,000.

Brigedia Jenerali Mabena amesema wanaendelea kukiongezea uwezo kwa maana ya kuongeza mahanga, vyoo na miundombinu mingine ili iweze kuchukua vijana wengi zaidi.

Amesema katika mwaka wa fedha 2023/24, kikosi hicho kilipewa Sh1.6 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa mahanga ambapo kinajenga mahanga saba ambayo yataongeza uwezo wa kuchukua vijana 700.

Naye Mkurugenzi wa Fedha wa JKT, Eveline Kibisa amesema wametembelea miradi inayoendeshwa vikosini na wameona majengo yamejengwa vizuri na yana thamani kulingana na fedha ambazo wamewapatia.

“Tunaishukuru Serikali na katika miaka hii mitatu ya fedha wameweza kutupatia fedha za kutosha na katika kila kikosi tumeweza uwezo mkubwa wa kuongeza idadi ya vijana,” amesema.

Amewaomba wakuu wa vikosi kusimamia vyema fedha wanazoziomba Serikali na kwamba itakavyoona kuna matumizi mazuri ya fedha watapata moyo wa kuendelea kuwasaidia kujenga mahanga zaidi.

Kamanda wa Kikosi cha 824 KJ, Luteni Kanali Mantage Nkombe, amesema katika kikosi hicho wamepata fedha kwa ajili ya ujenzi wa mahanga saba.

“Tumeona ni mafanikio kwani tunaweza kuongeza idadi ya vijana wanaojiunga na Jeshi letu la kujenga Taifa. Tunaendelea za kutekeleza tukitii maelekezo kutoka ngazi za juu kwanza kuhakikisha kuwa yanakamilika kwa muda,”amesema.

Pia amesema maagizo hayo watayatekeleza kwa  kuhakikisha thamani ya fedha inazingatiwa kwa kujengwa katika viwango bora.

Naye wa vijana wa kujitolea katika kikosi cha Jeshi 825 Mtabila hicho, Amina Singano ameshukuru Serikali kwa kujenga majengo 15 ambapo kati ya hayo matano ni ya wasichana na 10 kwa wanaume.

Related Posts