Kinzumbi Yanga, Musonda Mazembe dili lipo hivi!

MABOSI wa TP Mazembe wakiongozwa na CEO, Frederic Kitengie wiki hii wametua Makao Makuu ya Yanga yaliyopo Jangwani jijini Dar es Salaam kwa masuala mawili makubwa, kwanza kubadilishana uzoefu na lingine kujenga urafiki.

Kuna dili linakwenda kufanyika mwishoni mwa msimu huu. Taarifa ilizozipata Mwanaspoti ni kwamba, Yanga na TP Mazembe wameanza kujadili namna ya kubadilishana wachezaji huku kila upande ukitoa mapendekezo yao.

“Yanga kwa muda mrefu wanamfukuzia Philippe Kinzumbi, basi TP Mazembe wamekubali kumuachia kwa sharti la wao kupewa Kennedy Musonda.

“Inavyoonekana makubaliano hayo yatafikia pazuri na msimu ujao mkamuona Kinzumbi akiwa na jezi ya Yanga,”kilidokeza chanzo chetu ndani ya Yanga.

TP Mazembe ambao ni mabingwa mara mbili wa Kombe la Shirikisho Afrika walilobeba 2016 na 2017, wameona ndani ya Yanga kuna mali, hivyo wamekubaliana kubadilishana vifaa.

Kinzumbi na Musonda kila mmoja katika timu yake amekuwa akicheza akitokea pembeni.

Ndani ya Yanga, Musonda raia wa Zambia aliyejiunga na timu hiyo  Januari 2023, mkataba wake unatarajia kumalizika mwaka 2025 huku ikionekana hana nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha Kocha Miguel Gamondi.

Yanga inatafuta winga mwingine mwenye kasi kuelekea msimu ujao ili kuimarisha eneo lao la ushambuliaji hivyo wanaamini Kinzumbi ndiye mtu sahihi na wanaweza kumpata kirahisi kutokana na urafiki wa klabu hizo mbili.

Ikumbukwe kwamba, hivi karibuni Rais wa Yanga, Hersi Said alisafiri kwenda DR Congo kukutana na viongozi wa TP Mazembe kabla ya kuwaalika waje Dar kujenga zaidi urafiki wao ambao unaonekana unakwenda kuzaa matunda makubwa.

Huyu ni raia wa DR Congo mwenye umri wa miaka 25, amekuwa akiwindwa na Yanga tangu dirisha kubwa msimu huu lakini dili lake halikukamilika.

Winga huyo anayetumia zaidi mguu wa kushoto amekuwa ndani ya TP Mazembe tangu mwaka 2020 ambapo Yanga inamuhitaji ili kuongeza kasi katika eneo lao la ushambuliaji.

Endapo Yanga itampata winga huyo, kikosi chao kitakuwa na machaguo mengi zaidi kwenye eneo hilo kutokana na sasa uwepo wa Maxi Nzengeli ambaye wakati mwingine anatumika kupanda na kushuka. Mwingine ni Augustine Okrah ingawa kuna wakati hata Clement Mzize anacheza kutokea pembeni japo ana uwezo wa kucheza mshambuliaji wa kati. Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amesema ujio wa viongozi hao wa TP Mazembe una faida kubwa sana ambapo siku si nyingi Wananchi watafurahi.

“Katika ushirikiano wetu na TP Mazembe kuna mengi mazuri yanakuja, hivyo tusiwe na haraka,”alisema

Related Posts