Mbangula naye anajishangaa | Mwanaspoti

WAKATI wadau na mashabiki wakijiuliza kasi ya straika wa Tanzania Prisons, Samson Mbangula kupungua, mwenyewe amesema naye anashangaa kwanini hafungi tangu alipoifunga Simba.

Mbangula alikuwa na muendelezo mzuri wa kufunga mabao lakini tangu amefunga mabao mawili dhidi ya Simba, Machi 6 mwaka huu wakati Tanzania Prisons iliposhinda 2-1, hajaingia tena wavuni.

Staa huyo ambaye ni Askari Magereza ni miongoni mwa wachezaji wazawa wenye idadi kubwa ya mabao akifunga nane. Kinara ni Stephane Aziz Ki na Feisal Salum ambao kila mmoja amefunga 15. Hapo katikati wapo Wazir Junior (12), Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya na Marouf Tchakei ambao kila mmoja anayo tisa.

Mbangula alisema kama wanavyoshangaa wadau kutofunga kwake, hata mwenyewe anashangaa licha ya juhudi anazofanya awapo uwanjani lakini kulifikia lango imeendelea kuwa ngumu.

Alisema pamoja na ukame wa mabao alionao, lakini anaendelea kupambana kwani hajakata tamaa, badala yake anajifua kuhakikisha michezo mitatu iliyobaki anafanya kweli.

“Kwa mechi za sasa kila timu inajipambania kufikia malengo, kuna wanaokwepa kushuka daraja, vita ya nafasi nne za juu na wanaohitaji kuwa salama, lakini sijakata tamaa.”

“Zaidi naendelea kujiandaa na michezo iliyobaki ili nizidi idadi ya mabao niliyonayo, najua kazi si nyepesi sana kutokana na mabeki nao kuwa na mipango yao ila naamini nitafanya vizuri,” alisema Mbangula.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ahmad Ally alisema kwa sasa wanajiandaa na mchezo ujao dhidi ya Mashujaa, Mei 20 ambao ni muhimu sana kwao.

“Tumesota sana bila ushindi tangu mechi na Simba, sasa Mashujaa ndio watakata kiu yetu ya muda mrefu, tunajua mechi itakuwa ngumu ila hatuna namna” alisema Kocha huyo.

Prisons yenyewe imekuwa haina mwendelezo mzuri kwa siku za karibuni tangu ilipoifunga Simba Machi 6 kwani baada ya hapo imecheza mechi nane bila ushindi. Matokeo ya mechi hizo yapo hivi; Mtibwa 2-1 Tanzania Prisons, JKT Tanzania 1-1 Tanzania Prisons, Tanzania Prisons 1-1 KMC, Geita Gold 0-0 Tanzania Prisons, Tanzania Prisons 0-0 Kagera Sugar, Coastal Union 0-0 Tanzania Prisons, Dodoma Jiji 0-0 Tanzania Prisons na Tanzania Prisons 0-1 Ihefu.

Licha ya ukame huo wa mabao, lakini unaweza kusema huu ndiyo msimu bora zaidi kwa Mbangula ndani ya Ligi Kuu Bara kutokana na kufunga mabao hayo nane yakiwa ni mengi zaidi kwenye misimu mitano iliyopita kwani msimu uliopita alimaliza ligi akiwa na mabao sita, huku msimu wa 2021/22 akifunga moja wakati 2020/21 akutupia mawili. Msimu wa 2019/20 nao alifanya vizuri akifunga mabao saba.

Related Posts