Mwenyekiti wa Chadema, Fremaan Mbowe amesema Tanzania haijanufaika na miaka 30 ya demokrasia kutokana na mifumo iliyopo kukinufaisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachoamini fikra zake ndizo sahihi katika kuongoza nchi. Anaripoti Salehe Mohamed, Zanzibar… (endelea).
Mbowe ametoa kauli hiyo leo Alhamis katika mkutano wa demokrasia kwa mwaka 2024 unaofanyika katika Hotel ya Golden Tulip, ambapo amesema kuwa Watanzania walitarajia mfumo wa vyama vingi ungeleta mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali.
Amesema tatizo lililopo hivi sasa ni CCM kuamini inahodhi fikra za Watanzania badala ya kuruhusu fikra tofauti kutoka kwenye vyama vya wapinzani na wengine kuboresha maeneo mbalimbali.
“Mwaka 2015 tulikuwa na uchaguzi uliosababisha wapinzani wengi kuingia madarakani lakini baada ya uchaguzi tulikuwa tunaongoza halimashauri 47 na tuliamini tungeweza kutekeleza mipango na sera zetu lakini CCM walikwenda kufanya mabadiliko ya sheria na kupoka mamlaka za halimashauri katika utekelezaji wa shughuli zake” amesema.
Mbowe amesema kuwa mazingira yaliyowekwa na CCM yalifanya utekelezaji wa kazi kwenye maeneo yaliyokuwa yakiongozwa na upinzani hali ilikuwa ngumu zaidi jambo ambalo linaonyesha chama hicho tawala kinaizungumzia demokrasia kwa maneno na si vitendo.
“Sisi tunaamini sera za majimbo ili chama chochote kitakachoingia madarakai kitakuwa na uwezo wa kutekeleza sera na ilani zake katika eneo inaloliongoza badala ya ilivyo hivi sasa wakishinda wapinzani wanatekeleza sera na ilani ya CCM” amesema.
Mbowe amesema jambo la msingi linalopaswa kufanywa hivi sasa ni Taifa kutengeneza maridhiano ya kitaifa ili kupata Katiba inayotibu majeraha na kutibu changamoto za uchaguzi, kero za muungano na itakayohakikisha haki kwa makundi yote.
“Kama tunatafuta suluhisho tuanzie hapo, mwaka 2022 wakati natoka jela kwa kesi ya ugaidi nilikutana na Rais Samia Suluhu Hassan na aliniambia kuwa kama Taifa tuna tatizo la kutoaminiana tukakubaliana tumalize tofauti yetu. Tulikuwa tunakinzana kwa sababu ya kutoaminiana. Sasa tuondoke huko” amesema.
“Nilimuambia Rais Samia kuwa ni lazima wakubwa watambue kuna wadogo na kuwaheshimu kwa mawazo, fikra na matendo si kwa maneno. Ushirikiano unahitaji kuaminiana na kufikia maendeleo tuliyotarajia” amesema.
Mbowe amesema jambo lingine linalopaswa kuangaliwa kwa kina ni namna nchi inavyopata viongozi wake.
“Namna tunavyowapata viongozi wetu ndiyo tatizo, wapiga kura wanachagua wanayemtaka, mifumo inaamua vinginevyo kwa utashi wa CCM. Viongozi wetu hawana kibali cha Mungu katika kutawala” amesema.
“Leo Tume ya Uchaguzi imetangaza kuanza kuandikisha wapigakura. Process ya uchaguzi ni lazima kwanza iwatambue wapiga kura na kuhakikisha wapigakura badala ya kuanza kutangaza tarehe ya kuanza kuandikishwa watu wapya, vyama vya upinzani vinaingia katika uchaguzi wakati hawakushirikishwa kuanzia katika hatua ya kwanza ya kuhakikisha mambo yanakuwa mazuri” amesema.
Mbowe pia amesema kuwa CCM hawawezi kukwepa lawama wa kinachotokea hivi sasa kwa sababu hawaoni ulazima wa kusikiliza mawazo ya wengine na kuyafanyia kazi kwa masilahi kwa Taifa.
Naye Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Dorothy amesema wananchi wanajua wanataka nini na walitoa mapendekezo juu ya Katiba wanayoitaka lakini CCM hawakuwa na utashi kwa kuwa hawakufanya kile kilichohitajika na wananchi.
“CCM wamehodhi kila kitu, lakini tunachokifanya sasa katika demokrasia ni kudanganyana hata sheria iliyopatikana kuhusu Tume Huru ni kudanganyana. Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika miezi michache ijayo lakini Tamisemi ndiyo watausimamia. Hii si sawa na tulikubaliana tofauti,” amesema.
Amesema kudharauliwa na kupuuzwa kwa madai ya wananchi, mchakato wa Katiba hakuwezi kuifikisha nchi katika maendeleo na demokrasia iliyokusudiwa.
“Hii si sawa, tukifanya mabadiliko madogo kwa hila hatutaweza kupiga hatua katika maendeleo, mifumo inatuvusha kwa imani lakini si kwa kuiboresha kwa matendo yetu. Mifumo bado hatujaiandaa vizuri ya kutuletea kile tunachokitarajia. CCM wakubali kurekebisha mambo kwa vitendo si maneno matupu” amesema.