Mikoa sita vinara wizi wa mtandaoni hii hapa

Dodoma. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, ametaja mikoa sita yenye matukio mengi ya wizi wa kimtandao.

Nape ameitaja mikoa hiyo bungeni leo Mei 16, 2024 alipowasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25. Ameliomba Bunge kuidhinisha Sh180.92 bilioni.

Nape amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeendelea kudhibiti uhalifu mtandaoni kwa kuchukua hatua mbalimbali.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, akizungumza bungeni jijini Dodoma leo.

Amezitaja hatua hizo ni pamoja na kusimamisha usajili kwa mawakala wanaotembea kwa mikoa iliyoripotiwa kuwa na idadi kubwa ya matukio ya wizi wa kimtandao ambayo ni Rukwa, Morogoro, Dar es Salaam, Tabora, Songwe na Mwanza.

Amesema TCRA inaendelea kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi na wadau wengine kuhakikisha inakabiliana na tatizo la uhalifu wa kimtandao.

“Zoezi hili ni endelevu na linalenga kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kuwalinda watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini,” amesema.

Amesema Serikali kupitia TCRA imeendelea kuboresha na kusimamia uendeshaji wa mfumo unaosimamia na kudhibiti huduma za mawasiliano ya simu nchini (CMS).

Waziri Nape amesema mfumo huo umeiwezesha TCRA kubaini simu za ulaghai na zile za mitandao ya kijamii (OTT by- pass fraud) kwa kutumia njia za kisasa.

Amesema katika kipindi cha Julai 2023 hadi Aprili, 2024, TCRA imeendelea kubaini mawasiliano ya simu za ulaghai zinazoingia nchini.

Nape amesema katika kipindi hicho, simu za ulaghai 767 zilibainika na hatua stahiki zilichukuliwa.

Kuhusu kufungia laini za simu, Nape amesema namba tambulishi zilizofungiwa ni 95,194 ambazo ziliripotiwa kupotea, kuibwa au kuhusika katika matukio ya kihalifu.

Amesema hilo limewezesha kupunguza matukio ya wizi na kusaidia upatikanaji wa vifaa vya mawasiliano vyenye ubora kwenye soko.

Waziri Nape amesema sekta ya mawasiliano imeendelea kukua akieleza hadi Aprili, 2024 kulikuwa na laini za simu milioni 72.5.

“Idadi hii ya laini za simu inahusisha zinazotumiwa na watu na zinazotumiwa kwa ajili ya mawasiliano kati ya mashine kwa mashine (M2M),” amesema.

Related Posts