Mkanganyiko wa takwimu, mauzo ya ufuta yakipaa

Dar es Salaam. Wakati bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2024/25, ikionyesha kuwa mauzo ya zao la ufuta yalifikia zaidi ya Sh1.25 trilioni kwa kipindi cha mwaka 2022/23, taarifa ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) inaonesha mauzo yalikuwa Sh715.6 bilioni kwa mwaka 2023.

Licha ya kuwa takwimu hizo ni za vipindi tofauti lakini vinavyoingiliana, tofauti yake ni kubwa, jambo linaloweka ugumu wa kujua uhalisia ni upi, hata hivyo zote zinaonyesha ongezeko la mauzo ya zao hilo ambalo hivi karibuni limeweka rekodi ya kuuzwa kwa Sh4,500 mkoani Songwe.

Kwa mujibu wa Tantrade, mauzo ya ufuta yamekuwa yakipanda na kushuka ambapo mwaka 2019 yalifikia Sh492.66 bilioni, huku yakishuka kidogo mwaka 2020 (Sh487.31 bilioni) na mwaka 2021 (Sh444.82 bilioni), lakini yalianza kupanda mwaka 2022 hadi kufikia Sh504.08 bilioni.

Taarifa hiyo inaonyesha ufuta umekuwa ukiuzwa zaidi katika nchi za China, Japan, Uholanzi, Marekani, Korea na Israel.

Loading...

Loading…

Hata hivyo, kwa upande wa Wizara ya Kilimo, takwimu hizo, mauzo ya ufuta yamepita mauzo ya chai, kahawa, mkonge, kakao, tumbaku, pamba na pareto ambayo kwa pamoja yamefikisha zaidi ya Sh1.25 trilioni.

Ufuta ni zao la mafuta linalolimwa katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Katavi, Mbeya, Manyara na Morogoro, Pwani, Dodoma, Hata hivyo, asilimia 75 ya uzalishaji wa zao hilo unafanyika mikoa ya kusini.

Pamoja na mkanganyiko huo, bado zao la ufuta limeonekana kupaa sokoni, likipita zao mojamoja miongoni mwa mazao ya asili ya biashara ambayo ni chai, kahawa, mkonge, kakao, tumbaku, pamba na pareto.

Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Profesa Aurelia Kamuzora anashauri kuwapo kwa njia inayoweza kuchochea uzalishaji wa ufuta, ikiwemo kuainisha maeneo yanayofaa kwa ajili ya kilicho cha zao hilo.

“Ni fursa kubwa kwa nchi kama maeneo haya yataainishwa na uzalishaji kufanyika, pia wakulima wawezeshwe zaidi katika kulima zao hilo,” anasema Profesa Kamuzora.

Kuhusu kuongezeka kwa thamani ya mauzo ya ufuta, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alipotafutwa kwa simu hakupokea na hata alipotumiwa ujumbe, hakujibu.

Hata hivyo, akisoma hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo, Waziri Bashe alisema wizara yake imeendelea kuimarisha uzalishaji wa zao la ufuta kwa kusambaza mbegu bora za ufuta tani 24 kwa wakulima katika mikoa ya Lindi (tani 10), Mtwara (tani 10), Ruvuma (tani 2) na Pwani (tani 2).

“Vilevile, Wizara kupitia TARI imezalisha mbegu za msingi za ufuta tani 0.3 ambazo zitatumika kuzalisha tani 60 za mbegu zilizothibitishwa. Aidha, mafunzo ya kilimo bora cha zao la ufuta kwa wakulima 65 na maofisa ugani 62 yametolewa kwa wakulima katika Mkoa wa Mtwara,” alisema.

Katika eneo la mazao ya mafuta, alisema uzalishaji umefikia tani 2.14 milioni ikilinganishwa na tani 1.7 milioni mwaka 2021/2022, sawa na ongezeko la asilimia 25.8 ya lengo la tani 3.03 milioni.

“Kwa mfano, uzalishaji wa alizeti umeongezeka kutoka tani 425,653.1 msimu wa 2021/2022 hadi tani 1.13 milioni msimu wa 2022/2023, sawa na ongezeko la asilimia 166 na ufuta umeongezeka kutoka tani 79,170.43 msimu wa 2021/2022 hadi tani 266,694 mwaka 2022/2023 sawa na ongezeko la asilimia 237.2.”

Alisema tija ya zao la ufuta imeongezeka kutoka tani 1.49 kwa hekta hadi tani 1.6 kwa hekta, sawa na asilimia 0.64 ya uwezekano wa tija ya kuzalisha tani 2.5 kwa hekta.

Kwa mwaka 2024/2025 Serikali itahamasisha wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta, yakiwemo alizeti, chikichi, karanga na ufuta kutoka tani zaidi ya 2.14 milioni mwaka 2022/2023 hadi kufikia tani 2.2 milioni.

Mingine ni TARI kuzalisha mbegu za ufuta tani 108, ambapo kati ya hizo, tani tatu ni mbegu za awali na mbegu za msingi tani tano na mbegu zilizothibitishwa tani 100.

“TARI kutoa mafunzo ya kilimo bora cha zao la ufuta kwa wakulima 2,000 na maofisa ugani 500 na kuandaa mashamba ya mfano 105 katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Songwe, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro, Manyara, Dodoma, Singida, Tabora na Mbeya.

“Wizara itaendelea na majadiliano na Wizara ya Fedha kuweka kodi kwenye mafuta yanayotoka nje ya nchi ili kulinda viwanda vya ndani na wakulima,” anasema.

Zao lingine linalokuja kwa kasi ni mahindi, ambayo yameonekana yameongezeka mara tano katika kipindi cha mwaka 2020/2021 na mwaka 2022/2023.

Katika mwaka wa fedha ulioishia 2022/2023, mauzo ya mahindi yalifikia Sh628.958 bilioni, yakiongezeka kutoka Sh124.253 bilioni mwaka 2020/21.

Katika mwaka 2022/2023 Sh1.252 bilioni zilipatikana katika mauzo ya chai, kahawa, mkonge, tumbaku, pamba, pareto na kakao.

Pia mauzo hayo ni zaidi ya yale yaliyopatikana katika uuzaji wa bidhaa nyingine 28 ambapo ndani yake inajumlisha matunda, mbogamboga na mazao.

Kwa ujumla wake katika bidhaa hizo 28, jumla ya Sh1.183 trilioni ziliingizwa katika mwaka 2022/2023.

Mmoja wa wafanyabiashara wa mahindi aliyezungumza na Mwananchi, John Julius anasema urahisi iliowekwa kwa sasa katika ufikiaji wa masoko ya nje ni moja ya sababu ya mauzo hayo kuongezeka.

“Sasa hivi tunahamasishwa kuuza mazao nje ili tupate bei nzuri, hii inafanya tunakuwa huru kuuza mazao yetu kwa bei ya ushindani katika masoko ambayo tunaona yatatulipa sisi,” anasema Julius.

Mohammed Mwekya, ambaye pia ni mfanyabiashara alisema uwepo wa soko huru linalomwezesha mfanyabiashara kufikia fursa zinazopatikana katika nchi mbalimbali kunawafanya kujifunza vitu vingi na kujua ushindani uliopo, tofauti na kuwafungia wafanyabiashara katika eneo moja.

Licha ya fursa hizo, anataka kuendelea kurahisisha upatikanaji wa vibali kwa ajili ya kusafirisha mazao nchi mbalimbali, ili waweze kufikia fursa hizo kirahisi.

“Pia maelewano kati ya nchi na nchi ni muhimu ili kuondoa shida wanayoweza kukutana nayo wafanyabiashara mipakani, licha ya kuwa na vibali vyote, ni muhimu majadiliano yanayokuwa yakifanyika yaendelee kuleta matunda kama ilivyo sasa,” anasema Mwekya.

Akizungumza na Mwananchi, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli anasema uwepo wa mahitaji ya chakula katika nchi za karibu na Tanzania ndiyo sababu ya kuwapo kwa mauzo hayo, hasa katika mahindi.

“Mauzo yamekuwa yakitegemeana na soko, uzalishaji utakaokuwapo katika eneo husika ndio utakaoamua soko likoje, ndiyo maana tumeshuhudia ongezeko hilo, hasa katika mahindi,” anasema Mweli.

Alisema kilichoonekana katika mwaka wa fedha 2022/2023 huenda kikashuhudiwa tena katika mwaka wa fedha unaofuatia kutokana na baadhi ya nchi tayari kuonyesha nia ya kununua chakula Tanzania.

“Tayari mwaka huu pia tunatarajia kuuza zaidi katika nchi za Malawi na Zambia ambazo zimeshaonyesha nia ya kununua chakula kutoka Tanzania,” anasema Mweli, huku akitaja baadhi ya nchi kuwa ni Malawi na Zambia.

Akizungumzia mkanganyiko wa takwimu kati ya Wizara ya Kilimo na Tantrade, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema wameshaiona changamoto hiyo na wanaifanyia kazi.

“Sisi huwa tunachukua takwimu za mazao Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wizara ya Kilimo huwa wanaangalia vibali walivyotoa.

Tutuba anasema “Kwa mfano mfanyabiashara ameomba kibali cha kununua mchele tani 1,000, lakini akikusanya anapata tani 900 akatoa kwenda kuuza nje, TRA watarekodi hiyo.

“Au wakati mwingine, ananunua tani 1,000, lakini anauza nusu na nusu nyingine anaweka ghalani, labda amekosa wateja, TRA watarekodi mauzo ya nje mpakani, lakini Wizara ya Kilimo watarekodi kibali walichotoa,” alisema.

Alisema kutokana na changamoto hiyo, wameunda timu ya kuweka uwiano wa takwimu.

“Tuliliona hilo hata kwenye mauzo ya korosho, nikawaita tukazungumza. Kwa hiyo tumeunda timu ya kuangalia ili kuweka uwiano,” alisema.

Akifafanua zaidi, Tutuba alisema baadhi ya wafanyabiashara huongeza thamani ya mazao yao kutokana na gharama walizotumia wakati wa kununua.

“Kwa mfano mtu amenunua tani 1,000 ya mchele, anajumuisha gharama za wabebaji na usafiri, halafu akifika mpakani anaeleza gharama za ununuzi tofauti na zile za kununulia,” alisema.

Kuhusu sababu za zao la ufuta kutokuonekana kwenye taarifa za BoT, Tutuba alisema ni kwa sababu ya mfumo uliopo ambao umeshaweka namba maalumu (GFS codes) za mazao ya asili ya biashara.

“Yale mazao yalishawekwa tangu zamani ili kulinganisha nchi na nchi nyingine zinazozalisha, hivyo likiibuka zao lingine haliwezi kuingizwa, sanasana litachukuliwa kuwa ni zao linaloliwa ndani.

“Kwa mfano maharage, tunalima kwa wingi lakini hayamo, hata mbaazi tumekuwa tukiuza India, ni mabadilishano tu,” alisema.

Related Posts