Mpole, Ninja wasaka nafasi za CAF

WATANZANIA wanaochezea soka Ligi Kuu ya DR Congo, mshambuliaji George Mpole (FC Lupopo) na beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ (Lubumbashi Sport), wamezungumzia namna kazi ilivyo ngumu kuelekea kumaliza msimu huu wa 2023/24.

Mpole timu yake inaonekana kuwa na nafasi ya kucheza michuano ya CAF kwani ipo nafasi ya tatu, huku TP Mazembe ikiwa inaongoza ligi, lakini ni tofauti kwa Ninja ambaye timu yake ipo nafasi ya nane kati ya zile nane ambazo zinasaka ubingwa wa nchi hiyo.

Ligi hiyo kwa sasa inachezwa kwa kanda mbili, Lumbumbashi inawakilishwa na TP Mazembe, FC Lupopo, Lubumbashi Sport na Don Bosco.
Wakati Ukanda wa Kinshasa ni As Vita, Maniema, AF Congo na Douphine Noir, ambapo Jumamosi ya wiki hii, zitakutana FC Lupopo anayochezea Mpole na Lubumbashi Sport anayochezea Ninja.

Ninja aliyejiunga na klabu hiyo Agosti 2023 akitokea Yanga, amezungumzia hilo akisema: “Siioni nafasi ya timu yangu kupata nafasi ya kushiriki michuano ya CAF mwakani, ngoja tuone katika mechi mbili zilizosalia tutavuna kitu gani na Jumamosi tunacheza dhidi ya FC Lupopo anayoichezea Mpole, utakuwa mchezo mgumu.”

Kwa upande wa Mpole alisema: “Naiona nafasi ya kushiriki michuano ya CAF ingawa bado hatujamaliza mechi maana inaoongoza ni TP Mazembe.”

Amezungumzia mechi yao dhidi ya Lubumbashi Sport anayoichezea Ninja kwamba hautakuwa mchezo rahisi ila wakishinda watazidi kujiweka kwenye nafasi nzuri.

“Ukiona timu zilizoingia kucheza hatua za kanda kusaka bingwa wa nchi zinakuwa na ushindani mkali haijalishi ipo nafasi ya ngapi, hivyo natarajia utakuwa mchezo mgumu na ushindani,” amesema.

FC Lupopo msimu uliopita ilishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini ikawa ngumu kwa Mpole kucheza kwani kabla hajajiunga nayo alikuwa ameishacheza michuano hiyo akiwa na Geita Gold.

Mpole aliyejiunga na timu hiyo baada ya kutoka kuchukua Tuzo ya Ufungaji Bora ya Ligi Kuu Bara akifunga mabao 17 msimu wa 2021/22, alisema: “Natamani uwe msimu ambao utakuwa wa mafanikio kwangu baada ya msimu ulioisha ligi ya ndani kufutwa.”

Related Posts