Namna Zimbabwe inavyohaha na uhaba mkubwa wa chakula

Hali ya chakula nchini Zimbabwe inaripotiwa kuwa mbaya.

Kulingana na ripoti kutoka Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP), takribani watu milioni tano, ambao ni karibu theluthi moja ya watu wote milioni 16 wa Zimbabwe, wanahitaji msaada wa chakula.

Wazimbabwe milioni 2.5 wanakabilia na hatari ya kufa njaa, na wengine milioni 5.5 wako katika hatari ya kuwa katika hali kama hiyo siku za usoni.

Uhaba wa chakula umesababishwa na ukame kutokana na El Nino.

El Nino ni mzunguko wa matukio ya joto na baridi yanayotokea kando mwa Ikweta katika Bahari ya Pasifiki, husababisha ongezeko la joto la uso wa bahari katika Pasifiki.

Kipindi cha joto cha tukio hili, kinachojulikana El Nino Southern Oscillation (ENSO), kinasababisha hali ya ukame. ENSO huunda hali ya joto na kavu ambayo ina athari kwa mazao ya chakula.

Zimbabwe ni moja ya nchi katika ukanda wa kilimo ambayo mara kwa mara imekumbwa na athari mbaya za El Nino tangu mwaka 1982.

Matukio ya El Nino yamekuwa yakijirudia kwa njia isiyo ya kawaida, yakijitokeza kila baada ya miaka miwili hadi sita.

Kwa mfano, Februari 2016, Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe alitangaza ‘Hali ya maafa’ kutokana na ukame uliosababishwa na El Nino, ambao uliacha watu milioni 2.44 wakihangaika kwa kukosa chakula.

Shirika la Taifa la Anga za Juu na Bahari (NOAA) lilitabiri tukio kubwa la El Nino kutokea kati ya Oktoba 2023 na Machi mwaka huu.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) limetoa ombi la msaada wa dharura wa Dola za Marekani milioni 84.9 unaolenga kuwasaidia watoto na wanawake walioathirika na janga la El Nino nchini Zimbabwe.

Hali ya uhaba wa chakula inaathiri haki ya watoto kupata elimu na kulindwa. Kuna upungufu wa majisafi na salama, pia lishe duni na vyote vinaongeza hatari ya utapiamlo na magonjwa ya kuhara miongoni mwa watoto.

Mbali ya El Nino, mambo mengi yanahusika kama vile sera za ardhi, mabadiliko ya tabianchi, uwekezaji mdogo katika kilimo na migogoro ya kiuchumi.

Sera za ardhi nchini Zimbabwe zimekuwa moja ya sababu zinazochangia uhaba wa chakula.

Baadhi ya sera hizo zimesababisha athari mbaya katika kilimo na uwezo wa nchi kujitosheleza kwa chakula.

Julai 2000, Serikali ya Zimbabwe chini ya Rais Mugabe ilianzisha mpango wa mageuzi ya ardhi ya haraka ambao ulilenga kugawa ardhi ya kilimo kutoka kwa wamiliki wa Kizungu na kuwapa wananchi wa Waafrika.

Hata hivyo, utekelezaji wa mageuzi haya ulifanyika kwa njia isiyo ya mpangilio na mara nyingi ilihusisha uvamizi wa mali na ukosefu wa taratibu za kisheria. Hii ilifanya mashamba mengi kutolimwa au kulimwa bila ufanisi.

Mageuzi hayo yalisababisha kuporomoka uzalishaji wa kilimo kwa sababu wamiliki wapya wa ardhi mara nyingi hawakuwa na ujuzi au rasilimali za kutosha kufanya kilimo cha kibiashara.

Kutokana na wasiwasi wa usalama wa umiliki wa ardhi na mazingira duni ya biashara, wawekezaji wa ndani na wa kimataifa wamepunguza uwekezaji katika kilimo.

Hali hii imeleta athari kwa miundombinu ya kilimo, upatikanaji wa pembejeo na teknolojia ya kilimo, na kusababisha uzalishaji duni wa chakula.

Katika hili, suluhisho la kudumu linaweza kuhusisha marekebisho ya sera za ardhi ili kuhakikisha usimamizi bora na kuongeza uwezo wa nchi wa kuzalisha chakula.

Mbali na sera za ardhi, sababu nyingine ni mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa na athari kubwa kwa uhaba wa chakula nchini Zimbabwe, kama ilivyo katika maeneo mengine ya dunia.

Hali ya hewa inayoendelea kubadilika imeleta changamoto za kipekee kwa kilimo na usalama wa chakula. Sehemu ya mabadiliko ya tabianchi ni ukame ambao umesababisha upungufu mkubwa wa mvua, kuongezeka kwa joto, na hali ya ukame wa muda mrefu.

Hali hii imesababisha upungufu wa maji kwa mazao na mifugo, hivyo kusababisha upungufu mkubwa wa chakula.

Mbali na ukame, mabadiliko ya tabianchi pia yanaweza kusababisha mafuriko makubwa. Mafuriko yanaweza kusababisha uharibifu mkubwa kwa mazao, miundombinu ya kilimo na mifumo ya kuhifadhi chakula.

Mabadiliko ya tabianchi yamesababisha mabadiliko katika misimu ya kilimo, kama vile mwanzo wa mvua au mvua za muda mfupi. Hii imeharibu ratiba ya kupanda na kuvuna mazao.

Hata hivyo, ipo sababu nyingine inayochangia tatizo la uhaba wa chakula.

Sarafu ya Zimbabwe inahusiana na uhaba wa chakula nchini humo. Hii ni kwa sababu hali ya uchumi inaathiri upatikanaji wa chakula na uwezo wa watu kukinunua.

Kuporomoka kwa thamani ya sarafu kumeathiri uwezo wa wananchi kununua chakula na inaweza kuathiri masoko ya ndani ya chakula.

Wakati wa mporomoko wa thamani ya sarafu bei za bidhaa hupanda, ikiwa ni pamoja na mbolea, mbegu na dawa za kilimo.

Katika kukabiliana na hilo, Aprili, 2024 Benki Kuu ya Zimbabwe (RBZ) ilizindua sarafu mpya iliyopewa jina la ‘Dhahabu ya Zimbabwe’ (ZiG).

Lengo la ZiG ni kujenga imani na kurejesha utulivu katika mfumo wa fedha wa Zimbabwe.

Hata hivyo, ufanisi wa ZiG katika kukabiliana na hali mbaya ya uchumi ni suala linalokosolewa na wachambuzi na wadau wa kiuchumi. Ingawa hatua kama hizi zinaweza kusaidia kudhibiti mfumuko wa bei na kurejesha imani katika sarafu.

Changamoto nyingi za kiuchumi nchini Zimbabwe zinahitaji ufumbuzi wa kina zaidi kuliko tu kuzindua sarafu mpya.

Kuhusu uhaba wa chakula, ZiG pekee haiwezi kutatua tatizo hilo moja kwa moja. Kama ilivyoelezwa, hali ya chakula nchini Zimbabwe inahusiana na masuala mengi, ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa kilimo, miundombinu, sera za kilimo, mabadiliko ya tabianchi, na hata masuala ya kijamii na kiuchumi.

Kwa hiyo, ili kukabiliana na uhaba wa chakula, Serikali ya Zimbabwe inahitaji kuchukua hatua za kina zinazolenga kuboresha uzalishaji wa kilimo, kuboresha miundombinu, kusaidia wakulima kupata pembejeo za kilimo, kukuza teknolojia ya kilimo na kuboresha mifumo ya biashara na usambazaji wa chakula.

Serikali ya Zimbabwe sasa inachukua hatua kadhaa kuelekea malengo hayo, lakini bado kuna changamoto nyingi katika utekelezaji na athari zake.

Related Posts