Rais wa Urusi afanya ziara nchini China – DW – 16.05.2024

Wakati wa ziara ya Putin nchini China, Xi amemuhakikishia kiongozi huyo wa Urusi kuhusu ushirikiano wa karibu.

Vyombo vya habari nchiniChina, vimeripoti kuwa Xi amemwambia Putin kwamba kuimarika kwa uhusiano kati ya mataifa hayo mawili kunachangia katika amani, utulivu na ustawi wa kanda hiyo pamoja na ulimwengu kwa ujumla.

Xi asema mahusiano kati ya China na Urusi yameimarika

Vyombo hivyo vya habari pia vimeripoti kuwa kiongozi huyo wa China hakutaja kuhusu vita vya Urusi nchini Ukraine wakati wa hotuba yake ya ufunguzi lakini amesema kwamba mahusiano kati ya Urusi na China yameimarika na kuhimili jaribio la mabadiliko ya mazingira ya kimataifa.

Soma pia:Putin aishukuru China kwa ‘mipango’ ya amani ya Ukraine

Ziara hiyo rasmi ya Putin nchini China, inakuja wakati ambapo vikosi vya nchi yake vinaendeleza mashambulizi katika eneo la Kharkiv, kaskazini mashariki mwa Ukraine yalioanza wiki iliyopita, huu ukiwa uvamizi muhimu zaidi wa mpakani tangu kuzuka kwa vita kamili vya Urusi nchini humo.

Putin asema atamjulisha Xi kuhusu hali nchini Ukraine

Putin amesema kuwa atamjulisha kiongozi huyo wa China kwa undani zaidi kuhusu hali nchini Ukraine na kushukuru kwa muingilio wa China na washirika wake wengine katika kudhibiti hali hiyo.

Rais huyo wa Urusi ameongeza kusema wawili hao wamepanga mazungumzo zaidi ya sera za kigeni katika mkutano usio rasmi baadaye hii leo.

Maafisa wa uokoaji wazima moto kufuatia shambulio la Urusi mjini Kharkiv nchini Ukraine mnamo Mei 14, 2024. Urusi ilianzisha mashambulizi ya anga kwenye makazi ya watu katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Maafisa wa uokoaji wazima moto kufuatia shambulio la kombora la Urusi mjini Kharkiv, UkrainePicha: Anadolu/picture alliance

Kabla ya kutoa kauli zao, viongozi hao wawili walitia saini taarifa ya pamoja kuhusu kuimarisha ushirikiano wa kina na wa kimkakati kati ya mataifa hayo mawili katika kuadhimisha miaka 75 ya uhusiano wao wa kidiplomasia.

Xi amesema China na Urusi zitaendelea kushikilia msimamo wa kutokuwa na miungano na pia kutolumbana.

Putin asema ni muhimu kufanya kazi katika kujenga mfumo thabiti na wa kutegemeana katika eneo la Asia-Pasifiki

Kwa upande wake, Putin amesema wanaona ni muhimu kufanya kazi katika kujenga mfumo thabiti na wa kutegemeana katika eneo la Asia-Pasifiki ambapo hakuna nafasi ya miungano ya kijeshi na kisiasa iliyofungamana.

Wakati huo huo,Xi amesema yeye na Rais Putin wanakubaliana kwamba wanapaswa kuzingatia masuala yenye maslahi kwa mataifa hayo mawili, kujikuza na kuimarisha ushirikiano wa kimaslahi, na pia kuwezesha mafanikio ya kila mmoja.

Urusi inaitegemea zaidi China kiuchumi

Mkutano wa leo ulikuwa thibitisho lingine la urafiki usiokuwa na mipaka kati ya mataifa hayo mawili, waliokubaliana mnamo mwaka 2022, kabla ya Urusi kuanzisha uvamizi wake kamili nchini Ukraine.

Tangu wakati huo, Urusi imekuwa ikiitegemea zaidi China kiuchumi wakati ambapo vikwazo vya mataifa yamagharibi vimekatiza ufikiaji wake wa sehemu kubwa ya mfumo wa biashara ya kimataifa.

 

Related Posts