KATI ya sapraizi ambazo mashabiki wa Simba wanaweza kukumbana nazo wiki chache zijazo ni kung’oka kwa wakongwe wa kikosi hicho akiwemo Shomari Kapombe ambaye piga ua amekuwa hakosekani kwenye kikosi cha kwanza.
Kapombe ambaye ameitumikia Simba kwa nyakati tofauti akianza 2011 hadi 2013 kisha akarudi tena Julai 2017 mpaka sasa, anaondolewa kutokana na kile kilichoelezwa ni umri kuwa mkubwa kwani ana miaka 32 pia uwepo wa Israel Mwenda huku mipango mingine ni kusajili beki wa kigeni.
Uamuzi huo ni katika kuhakikisha msimu ujao Simba wanarudisha utawala wao uliopotea kwa misimu mitatu ndani ya Ligi Kuu Bara ambapo imeshuhudiwa Yanga ikitawala.
Simba iliyobeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara 22 ikizidiwa na Yanga mara nane, kabla ya kuwa vibaya ilitawala ligi hiyo kwa misimu minne mfululizo 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021 wakati ambao Yanga ilishindwa kutoboa.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinabainisha kwamba Kapombe anayemudu kucheza nafasi ya beki wa kulia na kiungo, safari yake ndani ya klabu hiyo inafikia tamati mwisho wa msimu huu.
“Katika kuijenga Simba mpya kuna mambo yanakwenda kufanyika ikiwemo kuimarisha kikosi kwa kuwaondoa wachezaji wakongwe baadhi wanaoonekana kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara akiwemo Kapombe kwani uongozi unaona wanatumia gharama kubwa kuwauguza halafu mchango kwa timu ni mdogo,” kilisema chanzo hicho.
“Kapombe kinachomgharimu ni namna anavyosumbuliwa sana na majeraha kwani akiumia kurudi uwanjani inamchukua muda mrefu na ukiangalia tunaye Israel Mwenda anayefanya vizuri kama anakosekana yeye.
“Mipango ya uongozi ni kumbakisha Mwenda kwani imeonekana hatuwezi kubaki nao wote kwa pamoja kwa sababu msimu ujao lazima aje beki wa kulia kutoka nje, hivyo mmoja atatupisha na ndiyo Kapombe. Hata hivyo pia David Kameta ‘Duchu’ yupo na anaweza kucheza nafasi hiyo lakini Duchu na Mwenda wote bado vijana wanahitaji mtu mwingine kwenye nafasi yao ndiyo maana atasajiliwa beki mzoefu wa kimataifa.”
Kapombe alijiunga na Simba Julai 2017 akitokea Azam FC, kisha Julai 2023 akaongeza mwingine wa kuendelea kuichezea Simba hadi Juni 30, 2025 hivyo amebakiwa na mwaka mmoja katika mkataba wake wa sasa.
Beki huyo msimu huu katika ligi kuu amecheza mechi 20 akitumia dakika 1,584 huku akitoa asisti nne, hana bao, amebeba Ngao ya Jamii baada ya Simba kuifunga Yanga katika mchezo wa fainali uliochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga katika ufunguzi wa msimu.
Kwa muda wote ambao amecheza Simba, Kapombe amebeba mataji matano ya Ligi Kuu Bara katika msimu wa 2011–12, 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021.
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba Simba wameshashtukia kwamba Henock Inonga ameshamalizana na FAR Rabat ya Morocco lakini kwavile wana mkataba nae wataminya dili hilo na watamuachia aende timu nyingine yoyote kwavile wamebonyezwa kwamba kuna dili zingine kama mbili zinakuja.
Habari zinasema kwamba Simba wameamua kufanya umafia huohuo kimyakimya kwavile wanaamini kwamba staa huyo hajitumi makusudi na amesusia mazoezi na kuondoka kwenda Ufaransa bila kuaga.
Straika raia wa Gambia, Pa Omar Jobe pamoja na Aishi Manula wataondolewa pia mwishoni mwa msimu kupisha sura nyingine, Mwanaspoti limeambiwa. Jobe alijiunga na Simba katika usajili wa dirisha dogo msimu huu ambapo bado ana mkataba na timu hiyo hadi 2026. Habari zinasema kwamba Manula atarejea zake Azam ambao mara kadhaa wamekuwa wakionyesha nia ya kuwa nae wakiamini kwamba atawabeba kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao japo kwa mechi chache kwani wamekuwa wakihangaika na eneo hilo kwa muda mrefu.
Mbali na Azam, Manula ambaye thamani yake imeonekana kushuka Simba baada ya kusimama langoni walipofungwa mabao 5-1 kwenye ligi, kipa huyo anahusishwa pia na Ihefu. “Jobe hajaonyesha kiwango uongozi unafikiria kumtoa kwa mkopo nafasi yake apatikane mchezaji mwingine wa kigeni.” Mbali na Jobe aliyejiunga na timu hiyo akitokea FC Zhenis Astana ya Kazakhstani, sababu kubwa inayomtoa pia Manula ni kile kilichoelezwa majeraha ya nyama za paja aliyonayo kwa sasa akiwa anaendelea kujiuguza akiwa nje ya uwanja kwa muda mrefu.
“Kinachofanyika ni kupambana kumbakisha Ayoub Lakred, yeye ana ofa amezipata, viongozi hawapo tayari kumuachia kwa namna yoyote ile ndiyo maana wanaendelea kumshawishi abaki kwa sababu akiondoka kumpata kipa mwingine wa kiwango chake itakuwa kazi kubwa,” kilisema chanzo hicho.
Wachezaji wengine walio kwenye nafasi ya kukatwa mwishoni mwa msimu huu kwa sababu mbalimbali ni Clatous Chama na Saidi Ntibazonkiza.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kwa sasa hawaangalii chochote zaidi ya kupigania kumaliza ligi ili kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kisha baada ya hapo ndiyo masuala ya kuboresha kikosi yatafuatia kwa kufahamika nani anatoka na nani anaingia.
“Bado tuna mechi nne za kucheza katika ligi, akili na mawazo yetu ni kuhakikisha hizi mechi tunazimaliza vizuri ili tuwe kwenye nafasi ya kuiwakilisha nchi katika Ligi ya Mabingwa kwani ndiyo michuano tunayostahili zaidi,” alisema Ally.
“Baada ya kukamilisha hili jambo, ndipo hayo masuala ya usajili katika kujenga kikosi utakuwa muda muafaka wa kuzungumzia lakini sio kwa sasa.”
Simba kwa sasa ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 57 baada ya kucheza mechi 26 imeachwa pointi tatu na Azam iliyocheza mechi 27, leo Ijumaa itapambana na Dodoma Jiji. Simba inapambana kumaliza ligi nafasi ya pili ili kupata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao nafasi ambayo Azam pia inaitaka.