Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetengeneza mfumo unaozifuatilia mashine za kutoa risiti za kielektroniki (EFD) ikisema ndio mwarobaini wa wafanyabiashara wanaokwepa kutumia mashine hizo.
Kupitia mfumo huo, utendaji wa mashine zote za EFD zitafuatiliwa na pale itakapoonekana kuna kusuasua kwenye utoaji wa risiti, mfanyabiashara anayemiliki mashine husika atatafutwa na hatua za kisheria zitafuata dhidi yake.
Kwa muda mrefu Serikali imekuwa na kilio kwa wafanyabiashara wanaokwepa kodi kwa kuacha kutoa risiti za bidhaa au huduma wanazotoa na wengine hutoa risiti pungufu.
Hatua hiyo inatajwa kuinyima mapato ya Serikali yatokanayo na kodi, hivyo kurudisha nyuma jitihada za ukusanyaji kodi na ukuaji wa uchumi.
Aprili 10, 2024, akihutubia Baraza la Eid El Fitr, Rais Samia Suluhu Hassan alionyesha masikitiko yake dhidi ya wafanyabiashara wanaojihuisha na vitendo vya ukwepaji kodi ilhali Serikali ilijitenga na kodi za dhuluma ili kutoa fursa nzuri kwao kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.
Rais Samia alisema wakati Serikali yake inaingia madarakani Machi 19, 2021 haikutaka kujihusisha na kodi za dhuluma lakini sasa dhuluma hiyo inafanywa na wafanyabiashara kwa kuzuia mapato ya Serikali.
“Nilipomwapisha Kamishna wa kodi nilimwambia nenda kakusanye kodi, tunazihitaji kwa ajili ya maendelo lakini kodi za dhuluma hapana. Nilisema hivyo kwa kutambua kwamba Serikali inahitaji mapato yatokanayo na kodi ili kutimiza majukumu yake ikiwemo kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kijamii.
Kwa mtazamo huo, leo Jumatano, Mei 14, 2024, Mkurugenzi wa Tafiti na sera wa TRA, Ephrahim Mdee amesema mamlaka hiyo kwa ushirikiano na taasisi ya Uingereza ya International Growth Centre (IGC), wameandaa mfumo wa kufuatuilia utoaji wa risiti siku hadi siku.
“Hii dashboard inatuwezesha kufuatilia mashine moja moja, kwahiyo tunafahamu idadi ya risiti zinazotoka katika kila mashine kwa siku na kama hazitoki tunafuatilia kwa nini. Hii inatupa uwezo wa kutumia sheria tulizonazo za kodi kwa ajili ya kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya wale ambao hawatumii mashine za usahihi.
“Wapo ambao tumeshawafikia na wametozwa faini lakini lengo letu sio hilo, tunachotaka ni mashine zitumike kwa usahihi na hiari hivyo tunaendelea kuelimisha wananchi waachane na vitendo hivi vya ukwepaji kodi, ukiuza toa risiti na ukinunua dai risiti,” amesema Mdee.
Akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Khamis Livembe amesema wafanyabiashara wanaoendesha shughuli zao kihalali hawana sababu ya kukwepa kodi kwa sababu wanatambua umuhimu wa kodi katika kukuza uchumi na kuendesha Taifa.
“Kodi ni msingi wa maendeleo ya nchi, kama mfanyabiashara hana konakona hawezi kukwepa kodi, hao wanaokwepa ni wezi kama wezi wengine, hivyo hatua stahiki zinapaswa kuchukuliwa dhidi yao,” amesema Livende.
Mkurugenzi Mtendaji wa IGC, Profesa Jonathan Leape amesema ufuatiliaji huo unalenga kuisaidia TRA na Tanzania kwa ujumla kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili yatumike katika maendeleo ya nchi.
Mazingira mazuri ya biashara
Akitoa msimamo wa Serikali, Kamishna wa Fedha za nje wa Wizara ya Fedha, Rished Bade amesema itaendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara na rahisi ya ulipaji na ukusanyaji kodi.
“Utafiti huu unaiwezesha TRA kuweka vizuri mifumo yake ya kodi, kuweka sheria za kodi ambazo zitalinda mapato ya Serikali na kufanya urahisi kwa wananchi bila kuwa na uhuni wowote wa kukwepa kodi,” amesema Bade.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru amesema ushirikiano baina ya TRA na IGC utaleta tija kubwa hasa katika kipindi hiki ambacho nchi ipo katika uandajii wa dira mpya ya Taifa ambayo utekelezaji wake utahitaji fedha.
Mkutano huo uliwakutanisha watafiti wa masuala ya kodi kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki wakiwemo wa Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (Repoa)
Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Dk Donald Mmari alisema wataalamu katika nchi hizo watashirikishana uzoefu wa maeneo muhimu katika ukusanyaji wa kodi, kutanua wigo wa walipa kodi na kuboresha ubunifu katika usimamizi wa kodi.
“Hakuna namna nchi hizi zinaweza kukua au kutatua changamoto zake za msingi bila kuwa na ukusanyaji wa kodi unaokidhi. Katika nchi nyingi za Afrika ukusanyaji wa mapato uko chini ya asilimia 16, Tanzania ikiwa na kiwango cha ukusanyaji cha asilimia 11.8,” alisema Dk Mmari.