WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kutekeleza miradi yote ikiwemo ya kimkakati kwa ajili ya kuhudumia jamii.
Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa Wizara ya Fedha itaendelea kupeleka fedha katika kila wizara ili miradi yote iliyoratibiwa na wizara hizo ikiwemo ya kilimo ziweze kukamilisha kazi zote zilizopangwa katika mwaka huu wa fedha.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Mei 16, 2024) wakati akijibu swali la Mbunge wa Hai, Mhe. Saashisha Mafue katika kipindi cha maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma. Mbunge huyo alitaka kufahamu Serikali imejipangaje katika kukamilisha miradi iliyopangwa kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha.
“Serikali inaendelea kutekeleza bajeti, nikuhakikishie Mheshimiwa Naibu Spika kuwa Wizara zote zilizoomba fedha na kupitishwa na bunge lako tukufu, fedha hizo zitatolewana kwenda kwenye wizara husika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi yote.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu amesisitiza watumishi wote wa umma wenye madai ya stahiki mbalimbali wanalipwa kwa wakati ili kuwaondolea kadhia zote zitakazowapunguzia morali ya kufanya kazi.
Mheshimiwa Majaliwa ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Kunti Majala aliyehoji nini kauli ya Serikali ya kuhakikisha inaondoa kadhia kubwa iliyoko kwa watumishi nchini.
Waziri Mkuu amesema Serikali imewasisitiza Wakuu wa idara waendelee kufanya uhakiki wa madeni ya watumishi wa umma na kuratibu vizuri ulipaji wake. “Jitihada zote hizi ni kuhakikisha kwamba watumishi hawavunjiki moyo katika kufanya kazi kwa kudai stahiki zao kwa muda mrefu.” Pia Waziri Mkuu amesema kazi ya kulipa wastafu inaendelea vizuri na kwa wale ambao bado watalipwa.