Ukisambaza picha za ajali Mbeya kukiona cha moto

Mbeya. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya, linakusudia kutumia sheria dhidi ya wananchi wanaokimbilia kupiga picha za matukio ya ajali na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii, jambo linalozua taharuki katika jamii.

Hatua hiyo imekuja kufuatia tabia ya baadhi ya wananchi kuanza kupiga picha na kuzisambaza mitandaoni pindi ajali zinapotokea, badala ya kusaidia uokoaji wa majeruhi kwenye ajali hizo.

Kauli hiyo imetolewa na leo Alhamisi Mei 16, 2024 na Ofisa Habari wa jeshi hilo mkoa wa Mbeya, Ester Kinyaga wakati akitoa elimu ya kukabiliana na majanga ya moto na uokoaji kwa askari wa Jeshi la Polisi.

“Tabia hiyo imeota mizizi sana katika mkoa wa Mbeya, matukio mengi ya ajali yamekuwa yakiripotiwa kwa tasfiri tofauti na kuzua taharuki kwa jamii ikiwepo taarifa za vifo,” amesema Kinyaga.

Ofisa huyo amesema wameweka mikakati ya kutumia sheria za kuwakamata na kuwachukulia hatua ili jamii irejee kwenye misingi, taratibu na kanuni za nchi.

Wakati huohuo, amewataka askari wa Jeshi la Polisi kuzingatia elimu ya masuala ya uokoaji ili kuongeza ushirikiano pindi yanapojitokeza matukio mbalimbali yanahitaji msaada.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, amesema kwa sasa wamekuja na utaratibu mwingine wa kuwapima askari wake kwa kufanya mitihani mara baada ya kuhitimu mafunzo mbalimbali yanayotolewa ikiwepo elimu ya majanga ya moto.

“Kwa sasa kuna utaratibu kila askari anayeripoti kutoka chuo, wanapopangiwa mikoani wanaingia darasani na kupata elimu nyingine na kuwapima uelewa kwa vitendo na mitihani.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi jijini wamesema matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii yamekuwa yakizua taharuki kubwa pindi yanapojitokeza majanga ikiwepo ajali za barabarani.

Naye Tabu Aloyce amesema Serikali imechelewa kutumia sheria hizo, ufike wakati zitumike ili wananchi wawe na hofu ya usambazaji wa picha zisizostahili na kuzua taharuki.

Related Posts