Wanafunzi 194 Momba wapewa mimba ndani ya mwezi mmoja

Songwe. Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo ameagiza kukamatwa ndani ya siku 21 kwa wanaume waliohusika kuwapa mimba wanafunzi 194 wa shule za msingi na sekondari katika Wilaya ya Momba mkoani Songwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. 

Chongolo ameyasema hayo leo Mei 16, 2024 wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo akikagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi kupitia mikutano ya hadhara.

Wakati Chongolo akieleza hayo, ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania ya mwaka 2022 inaonyesha Songwe kuwa mkoa unaoongoza kwa mimba za utotoni ikiwa na asilimia 45.

Mikoa mingine ni Ruvuma (asilimia 37) Katavi (asilimia 34), Mara (asilimia 31) na Rukwa (asilimia 30). Hata hivyo, ripoti hiyo inabainisha kupungua kwa mimba za utotoni kutoka asilimia 27 mwaka 2015/2016 hadi kufikia asilimia 22 mwaka 2022.

Ongezeko la mimba za utotoni limerekodiwa katika mikoa ya Dar ambayo mwaka 2025/2016 ilikuwa kwa asilimia 11.9 ripoti imeonyesha mwaka 2022 kiwango kimefikia asilimia 18.1, Njombe kutoka asilimia 19.7 hadi silimia 25.5 na Ruvuma kutoka asilimia 32 hadi asilimia 37.

Akiwa kwenye ziara yake, Chongolo ameeleza kusikitishwa na takwimu mbaya za wanafunzi 194 katika halmashauri ya Wilaya ya Momba kupewa ujauzito ndani ya mwezi mmoja, huku akiliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha ndani ya siku 21 linawakamata wahusika wote ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Amesema mkoa wa Songwe ni miongoni mwa mikoa mitano nchini inayoongoza kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia, ubakaji, ulawiti, mimba na ndoa za utotoni, hivyo ni jukumu la wote kuhakikisha wanasimama kidete kupiga vita tabia hizo.

“Wilaya ya Momba ina shule za msingi 103 na shule za sekondari 17, cha kushangaza ndani ya mwezi mmoja watoto 194 wamepewa ujauzito, Hii ni hatari kubwa, tunatakiwa tushirikiane kuhakikisha tunatokomeza mimba za utotoni,” amesema Chongolo.

Chongolo amewaagiza maofisa watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha wanawafichua wanaume wanaoharibu maisha ya watoto na kutoa taarifa kwenye uongozi wa wilaya ili hatua zaidi za kisheria zichukuliwe.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoani Songwe, Augustino Senga amesema wapo katika mikakati ya kuwasaka waliowapa mimba wanafunzi hao na kwamba maagizo ya mkuu wa mkoa ameyapokea na atahakikisha wahusika wanatiwa hatiani.

“Mimi nina mwezi mmoja na nusu toka niletwe mkoani hapa, nimekuta baadhi ya matukio ya aina hii yametokea, naahidi wahusika wote hawataachwa salama, nawasihi ndugu zangu waacheni watoto wasome, msijiingize kwenye matukio hayo,” amesema Kamanda Senga.

Mkuu wa Wilaya ya Momba, Kenan Kihongosi amemhakisha mkuu wa mkoa huo kwamba atatekeleza maagizo aliyompa ndani ya siku 21, na wahusika wote watasakwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ili iwe mfano kwa wengine.

Mkazi wa kijiji cha Chiwanda wilayani Momba, Ester Nakawale amesema viongozi wa vijiji wamekuwa wakimaliza kesi kienyeji na kupelekea kushamiri kwa kesi kuendelea kwani hakuna hatua zozote zinazochukuliwa kwa wahusika.

Naye Juma Simpasa amesema chanzo cha mimba hizo ni baadhi ya wazazi kutokuwa na nia ya kuwaendeleza watoto wao kimasomo, hivyo ili kukomesha tatizo hili, lazima sheria kwa wahusika iongezwe makali ikiwa ni pamoja na kifungo cha miaka 60 jela, tabia hiyo itakoma.

Related Posts