Wanajeshi watano wa Israel wajeruhiwa kwa kugongwa kwa gari

Israel. Wanajeshi watano wa Jeshi la Israel (IDF), wamejeruhiwa baada ya kugongwa na gari eneo la Haifa.

Tukio hilo lililotokea asubuhi ya leo Mei 16, 2024 linachunguzwa kubaini iwapo ni ajali ya kawaida au shambulio dhidi ya askari hao.

Askari hao wamegongwa jirani ya kambi ya kijeshi walipokuwa wamesimama kando mwa barabara katika Mtaa wa Moshe Dayan, ulioko Haifa.

Tukio hilo limeripotiwa na tovuti za Times of Israel, Ynet na Jerusalem Post.

Taarifa zinaeleza tukio hilo lina mwelekeo wa kuwa ajali ya kawaida lakini uchunguzi unafanyika kubaini iwapo ni shambulio lililopangwa.

Polisi inamshikilia dereva wa gari hilo na inaelezwa uchunguzi umeanza.

Watoa huduma ya afya wanasema wanajeshi hao wamepelekwa kwa matibabu katika kituo cha tiba cha Rambam.

Kwa mujibu wa taarifa askari mmoja amejeruhiwa kichwani na miguuni. Wengine wanne inaelezwa hawakupata madhara makubwa.

Katika hatua nyingine, imeripotiwa wanajeshi watano wa IDF wameuawa na wengine saba kujeruhiwa usiku wa jana Mei 15, 2024 Kaskazini mwa Gaza baada ya makombora kufyatuka kwenye kifaru.

Uchunguzi wa awali wa IDF unaonyesha kifaru hicho kinachofanya kazi pamoja na askari wa miamvuli katika kambi ya Jabaliya kilifyatua makombora mawili kwenye jengo ambalo askari walikuwa wamekusanyika usiku.

Askari hao inaelezwa kimakosa walidhaniwa kuwa ni kikosi cha adui hivyo kushambuliwa kwa makombora hayo.

Kwa mujibu wa takwiku za IDF, kati ya askari 278 wa Israel waliokufa katika mapigano kwenye Ukanda wa Gaza katika mapambano dhidi ya Hamas yaliyoanza Oktoba, mwaka jana, 49 wamekufa kwa kushambuliwa kimakosa na askari wenzao.

Inaelezwa matukio hayo hutokea kutokana na changamoto ya mawasiliano miongoni mwa vikosi na wakati mwingine ni kutokana na uchovu wa askari au kutokuzingatiwa kwa kanuni.

Askari wengine 1,712 wemejeruhiwa kati ya hao, 338 wamejeruhiwa kwa kiasi kikubwa, huku wengine 566 kwa kiasi cha kati na 808 majereha yao ni ya kiwango kidogo.

Imeandikwa na Sute Kamwelwe kwa msaada wa mtandao

Related Posts