‘WANANCHI ACHENI KUNUNUA DAWA ZINAZOTEMBEZWA MIKONONI,KATIKA MABASI KWANI NI HATARI KWA AFYA’

Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Iringa

MKUU wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba amewataka wananchi waaache mara moja kununua dawa zinazotembezwa mikononi ikiwa ni pamoja na katika vyombo vya usafiri(mabasi) kinyume cha sheria kwani mara zote dawa hizo huwa ni duni na bandia.

Pia amesema Serikali haitamwonea huruma mtu yeyote atakayepatikana na dawa bandia kwa kigezo kuwa hakujua kuwa ni bandia wakati huo huo akiwa amesababisha madhara kwa wagonjwa.

Akizungumza wakati akifungua kikao kazi kilichoandaliwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba(TMDA)kwa Wahariri wa vyombo vya habari, Serukamba amesema hivi karibuni mamlaka hiyo imetoa taarifa kwa umma kuhusu uwepo wa dawa hizo bandia ambazo ni hatari kwa afya za wananchi.

“Hivyo niwaombe wahariri muendelee kutumia vyombo vyenu kuwaelimisha wananchi kuhusu suala hili hususani kuwalimisha wananchi waache kununua dawa zinazotembezwa mikononi ikiwa pamoja na katika vyombo vya usafiri.Serikali haitamwonea huruma mtu yeyote atakayepatikana na dawa bandia,”amesema.

Amefafanua Mamlaka hiyo haiwezi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi bila ushirikiano wa vyombo vya habari , hivyo ni imani yake kuwa kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na kushirikishana wananchi wataelewa matatizo yaliyopo katika jamii yanayohusu usalama na ubora wa bidhaa zinazodhibitiwa na TMDA.

“Hivyo kuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba sura 219 inatekelezwa na wadau wote kwa ufanisi.Tunafahamu tofauti na bidhaa nyingine dawa, vifaa tiba na bidhaa nyeti na zenye madhara makubwa ya kiafya ikiwa hazikudhibitiwa ipasavyo na yanaweza kusababisha ulemavu…

“Kupoteza maisha na hivyo kudhoofisha uchumi wa nchi.Kwahiyo bidhaa hizo zinahitaji kudhibitiwa kwa utaratibu wa namna ya pekee, lengo likiwa ni kuzuia madhara kwa watumiaji katika kufikia lengo hilo bidhaa hizo zinahitaji kuhakikiwa usalama, ubora na ufanisi kabla ya kuruhusiwa kutumika, kazi ambayo inasimamiwa na TMDA,”amesema.

Kwa upande wake Dk.Yonah Mwalwisi ambaye ni Mkurugenzi wa Dawa kutoka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba(TMDA) alipokuwa akitoa mada katika kikao kazi hicho amesema

makadirio ya Shirika la Afya Duniani(WHO) yanaonesha bidhaa tiba moja kati ya 10 zinazozunguka katika soko , basi itakuwa bandia.

Akieleza zaidi alipokuwa akitoa mada kuhusu bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi bandia na hatua zinazochukuliwa katika kudhibiti dawa hizo, Dk.Mwalwisi amesema changamoto ya dawa duni na bandia iko duniani kote.

“Kwa Tanzania sisi tuko chini ya asilimia moja yaani tuko asilimia 0.2 lakini nchi nyingi duniani zinakabaliwa na changamoto hiyo kwa kiwango kikubwa, kwetu tumefanikiwa kudhibiti kutokana na hatua ambazo zinachukuliwa na TMDA,”amesema.

Amefafanua thamani ya bidhaa za dawa bandia zimefikia Dola za Marekani bilioni 30.5 na hiyo inatokana na uwepo wa bidhaa bandia nyingi na ndivyo inavyozungumzwa.

“Tunapozungumzia uwepo wa dawa bandia hapa nchini tunazungumzwa tofauti sana lakini ukiangalia takwimu zinatuonesha tofauti, tuko chini ukilinganisha na wengine.

“Suala la bidhaa bandia na la duniani kote , sio la Tanzania peke yake .Hakuna nchi ambayo iko salama katika bidhaa duni na bandia,”amesema na kusisitiza kwa Tanzania TMDA imekuwa na mifumo thabiti ya kudhibiti changamoto hiyo na wamefanikiwa.

Ametumia nafasi hiyo kufafanua kuwa uwepo wa dawa bandia na duni duniani kumesababisha kuripotiwa kwa vifo akitolea mfano matumizi ya viua vijasumu inachangia vifo vikiwemo vya watoto waliokuwa wanasumbuliwa na kifua cha kubana ambao walipoteza maisha baada ya kutumia dawa hizo.

Akeieleza zaidi amesema kuwa udhibiti uingizaji bidhaa bandia na duni umeifanya Tanzania kuwa salama .“Hakuna bidhaa tiba inayoingia nchini bila kupata kibali kutoka TMDA.”







Related Posts