Wanasiasa hawasaidii mchakato wa Katiba mpya

Seneta wa jimbo la Busia, nchini Kenya, Okiya Okoiti Andrew amesema Tanzania haiwezi kupata Katiba mpya kwa kuwategemea wanasiasa pekee bali kila mwananchi anapaswa kushiriki kikamilifu kuidai. Anaripoti Salehe Mohamed, Zanzibar … (endelea).

Kauli hiyo ameitoa leo Alhamisi katika mkutano wa demokrasia wa mwaka 2024 unaofanyika katika hoteli ya Golden Tulip Zanzibar, ambapo amesema Kenya walifanikiwa kupata Katiba iliyopo hivi sasa kutokana na asasi za kiraia kwa kushirikiana na wananchi kuwa mstari wa mbele kuidai.

Amesema kuwa kama Watanzania wasipokuwa mstari wa mbele kudai Katiba wasitegemee wataipata kwa kuwa wanasiasa wanafanya mambo yenye masilahi kwao.

“Nimewasikia hapa kuwa mnawategemea wanasiasa kushinikiza Katiba mpya, nawaambieni ukweli hamtafanikiwa kwa kuwa wanasiasa ni sawa na askari jela na nyinyi (wananchi) ni sawa na wafungwa mnaotaka kuvunja jela muwe huru. Kamwe askari jela hawatakubali mfanye hivyo,” amesema.

Amesema kuwa Kenya kama kiongozi akileta masihara atapata wakati mgumu hivyo ni vema raia kuwa wakali juu ya mambo wanayoyaona hayaendi sawa.

“Wananchi teteeni uhuru na mambo yenu, wanasiasa, wanasiasa wanapigania nani awe askari jela. Wakitofautiana baada ya uchaguzi wanaweza kukaa pamoja na kugawana madaraka. Hawa hawakubali jela ivunjwe nanyi msipokuwa makini kung’amua jambo hilo mtaendelea kuwa ndani ya jela kama wananchi,” amesema.

“Mkitegemea wanasiasa hamuwezi kupiga hatua, mkitegemea maandamano ya wanasiasa na wawe mstari wa mbele katika kupanga vita mtadanganyana,” amesema.

“Mkitaka kushinda hii vita, mnapaswa kujiunga pamoja na kutetea masilahi yenu. Asasi za kiraia zinapaswa kusonga mbele kudai Katiba” amesema.

Hata hivyo, Okiya amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika mchakato wa Katiba mpya ambao ulikwama mwaka 2014 na kinachotakiwa kufanyika hivi sasa ni kuangalie kile kilichopatikana wakati ule kinaweza kutumikaje.

“Msitarajie kupata kikubwa bila kuthamini kidogo kilichopatikana, ninyi mlishapiga hatua lakini naona kama mnataka kukipoteza badala ya kuking’ang’ania, nendeni mahakamani mkahakikishe mabadiliko mliyokusudia yanatokea,” amesema.

Amesema kuwa wanasiasa hawapendi Katiba nzuri kwa kuwa wanapenda kuiba kura ili waendelee kuwepo madarakani.

“Wanasiasa wanataka mifumo ambayo ni rahisi kwao kucheza na kura zilizopigwa ili wabaki madarakani, ni lazima tuwe na mifumo imara ya Katiba ambayo haitachezewa. Katiba bora itazuia hila za kupoka madaraka” amesema.

Amesema kuwa Katiba mpya haitawaletea chakula wananchi bali itawazuia watu wanaowaibia kura wala kuwanyang’anya chakula walichonacho.

Katiba inazuia watu kunywang’anywa haki zao, inawafanya watu wawe huru na kuamulia mambo yao sambamba na kutekeleza haki za binadamu.

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga amesema kuwa ni lazima kuwapo kwa muunganiko wa makundi mbalimbali katika kudai Katiba mpya.

“Wanasiasa wanapopoka mchakato wa Katiba maana yake hatuwezi kupiga hatua, yeye huangalia masilahi yake kwanza na si vinginevyo. Tushirikiane na wanasiasa lakini tusiwaachie mchakato huu” amesema.

Saed Kubenea

Naye Saed Kubenea, amesema kuwa Tanzania ilikwama katika mchakato wa Katiba mpya kuanzia siku inazinduliwa na jambo hilo lilisababishwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

“Tume ya mabadiliko ya Katiba ilizuiwa kutoa ufafanuzi kwa wajumbe wa Bunge Maalum kwa nini walipendekeza hoja fulani, kimsingi mkwamo ulikuwa mkubwa,” amesema.

Related Posts