WATAFITI WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA, KANUNI ZA KUFANYA TAFITI ZA AFYA

Na WAF – Dar Es Salaam

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka watafiti wote nchini kuzingatia sheria na kanuni za tafiti za Afya ikiwemo kupata kibali kutoka NIMR pamoja na kuzingatia maslahi ya Taifa.

Waziri Ummy ametoa agizo hilo leo Mei 16, 2024 wakati akifunga kongamano la 32 la Kisanyansi lililofanyika kwa Siku Tatu katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalim Julius Kambarage Nyerere Jijini Dar Es Salaam.

“Fanyeni tafiti zenu kwa uthibitisho wa Kisayansi na tuzione, zisibakie kwenye makaratasi, watumieni waandishi wa habari kutoa taafira zenu za tafiti ili zijulikane na ziweze kufanyiwa kazi.” Amesema Waziri Ummy

Aidha, Waziri Ummy amesema Sekta ya Afya itaendelea kuwekeza katika tafiti za Kisayansi lengo likiwa ni kuiwezesha Serikali kutunga sera pamoja na kufanya mabadiliko ya sera mbalimbali zinazohusu masuala ya Afya.

Amesema, Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga fedha kiasi cha Tsh: Bilioni 3.5 kwa ajili ya kuiwezesha NIMR kufanya tafiti mbalimbali za Kisayansi ili Serikali iweze kupata ushahidi wa Kisayansi katika kufanya maamuzi pamoja na kuboresha huduma za Afya.

“Umuhimu wa tafiti za Kisayansi zinaiwezesha Serikali kufanya maamuzi ambayo yana uthibitisho wa Kisayansi ikiwemo uamuzi uliofanywa wa kutoa dozi moja ya chanjo ya HPV kwa ajili ya kuwakinga wasichana kupata Virusi vya Saratani ya Mlango wa Kizazi.” Amesema Waziri Ummy

Amesema, awali Chanjo hizo zilikua zinatolewa kwa dozi mbili lakini baada ya tafiti za Kisayansi ambazo Serikali imejiridhisha sasa inatolewa dozi moja kwa wasichana wenye umri kuanzia mika 9-14 ambayo inatuwezesha kuokoa fedha.

Kwa upande wake Prof. Abood ameiomba Serikali kuendelea kuwekeze fedha kwenye Taasisi ya Utafiti ya Taifa (NIMR) ili kurahisisha ufamyaji wa tafiti mbalimbali katika Sekta ya Afya.

Related Posts