Dar es Salaam. Wadau wa kilimo, uvuvi na ufugaji wamesema hatua ya Serikali ya kuendelea kuzifungamanisha taasisi za fedha na sekta hizo ni hatua nzuri.
Lakini wametoa angalizo kuwa fursa hizo ziwaguse wakulima, wafugaji wakubwa na wadogo badala ya kuwaangalia zaidi wakubwa.
Walieleza hayo jana wakati wakitoa maoni yao kuhusu hatua ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), kuingia makubaliano na benki ya Exim ya kutoa mkopo Sh30 bilioni wenye masharti nafuu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kwa miaka mitano. Exim ni taasisi ya 17 kuingia makubaliano hayo na TADB.
Mdau wa kilimo, Lucas Malembo alisema hatua ya taasisi za fedha kuongezeka katika utoaji wa mikopo katika sekta hizo ni jambo jema kwa kuwa imekuwa na changamoto ya kutoaminika kwa sababu ya shughuli hiyo kutegemea zaidi hali ya msimu husika.
“Tunahitaji kulima kila wakati sio kwa msimu tena, lakini tutafikia ndoto hiyo endapo tutakuwa na teknolojia bora ya kuwezesha kilimo cha umwagiliaji.”
“Ili kuleta ufanisi katika sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi, Serikali ije na sera itakayowasaidia kukopesheka kwa urahisi kwa kuweka dhamana mashamba yao,” alisema Malembo.
Mwenyekiti wa chama wafugaji Tanzania, Mrida Malocha alisema, “changamoto kubwa iliyopo hii mikopo ikitoka tunasikia tu, maana kuna maeneo taasisi hizi za fedha hazipo, kwa hiyo wanaonufaika ni wale wakubwa tu, lengo hili jema ambalo nahisi lina mkono wa Serikali litakuwa na tija iwapo mikopo hii itafika hadi ngazi ya chini, kuliko ilivyo sasa ni kama inatolewa kwa ajili ya wakubwa,” alisema Malocha.
Naye, Mwenyekiti wa wavuvi kanda ya Ziwa Victoria, alisema, “angalizo langu katika utoaji wa mikopo hii, iende kwa walengwa mahsusi ili kuleta tija kwa wavuvi wetu, lakini ikienda kinyume cha hapo, tutaishia kusikia inakwenda kwa wavuvi au wakulima ila wenyewe haiwafikii.”
Awali akisaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege alisema wamekubaliana na Exim kutoa mikopo kwenye sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi ili kuwafikia wakulima wengi zaidi.
“Leo tumesaini makubaliano ya kuwapatia dhamana Exim ili kutoa mikopo katika sekta ya kilimo, kwa sababu huko nyuma kulikuwa na dhana ya sekta ya kilimo ni hatarishi, ndio maana taasisi za kifedha zinashindwa kutoa mikopo.
“Tunapowapa dhamana hii maana wanakwenda kwa Mtanzania yeyote iwe Tanzania bara au Zanzibar anapata mikopo hasa vijana na wanawake ambao hawana dhamana.
Serikali imetupa fedha ili kuwadhamini watu wa sekta hizi kukopesheka na benki,” alisema Nyabundege.
Mkurugenzi wa Fedha wa Exim, Shani Kinswaga alisema ushirikiano huo utakuwa na tija kubwa kimaendeleo kwa wajasiriamali wadogo, vijana, wanawake na makundi mbalimbali ya wafanyabiashara wanaokosa fursa ya fedha kwa vigezo vya dhamana.
“Ushirikiano huu utaongeza wigo wa upatikanaji wa mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kwa njia rahisi hasa waliopo katika ngazi za chini ikiwamo vijijini. Mikopo hii yenye masharti nafuu itawawezesha kupiga hatua kutoka katika kilimo kujikimu kwenda kilimo biashara,” alisema Kinswaga.