Serengeti. Wakazi wa Kijiji cha Kenyamonta kilichopo Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita 10 kufuata huduma ya afya katika kijiji jirani cha Iramba kutokana na kijiji chao kutokuwa na kituo cha afya.
Kutokana na hali hiyo, wakazi hao wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo vifo vya mama na watoto pamoja na wazee, huku baadhi ya kina mama wakilazimika kujifungulia njiani kabla ya kufika kwenye zahanati hiyo ya Iramba.
Hayo yamebainishwa leo Mei 16, 2024 na baadhi ya wakazi wa kijiji hicho walipokuwa wakipokea msaada wa mabati kwa ajili ya kuezekea jengo la zahanati kutoka Benki ya Biashara ya Taifa (TCB).
“Mimi ni bodaboda na wiki iliyopita kuna mzee alifia njiani nikiwa nimembeba yeye na ndugu yake, tukiwa tunamkimbiza hospitalini Iramba, maana yake ni kwamba kama hapa tungekuwa na zahanati labda yule mzee asingefariki, angewahi na kupatiwa matibabu,” amesema Dismas Ngoko, mkazi wa kijiji cha Kenyamonta.
Ngoko amesema mbali na kushuhudia kifo cha mzee huyo, pia amewahi kushuhudia kina mama wawili wakijifungulia njiani kwa nyakati tofauti baada ya kushindwa kufika katika zahanati ya kijiji jirani kutokana na umbali kutoka kijijini kwao.
Amesema kutokana na hali hiyo, kijiji chao kinahitaji kuwa na kituo cha afya ili wananchi wapate huduma hiyo muhimu kwa ukaribu na uhakika zaidi.
“Baadhi ya kina mama wanashindwa kufika hospitalini kwa wakati kwa sababu suala la uchungu halina muda maalumu, ni kitu cha kushtukiza, mfano ukiumwa uchungu usiku kwa kweli inakuwa ni vigumu sana kujifungulia hospitali maana kule huwezi kwenda kwa mguu, lazima utafute usafiri,” amesema Nyambura Mbusi.
Amesema mbali na kujifungua, pia mama wajawazito wanashindwa kuhudhuria kliniki kipindi chote cha ujauzito kutokana na umbali huo.
Amesema tofauti na umbali, pia gharama za usafiri zipo juu, hivyo wanashindwa na kuamua kutumia dawa za kienyeji muda wote wa ujauzito.
“Hapa wajawazito wengi wanajifungulia nyumbani na baadhi yao wanafariki au wanapoteza watoto kwa sababu inakuwa ni vigumu sana kufika kwa wakati kutokana na changamoto za umbali na gharama,” amesema Ghati Tumbe
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Getene Sanchawa amesema kutokana na adha wanayoipata wakazi wa kijiji hicho, serikali ya kijiji ilikuja na wazo la mradi wa ujenzi wa zahanati ili kusogeza huduma karibu na wanachi.
“Tunaiomba Serikali itushike mkono kwani mradi wetu unaendelea vizuri hadi sasa,pia itenge kabisa bajeti ya kuajiri watumishi isije ikatokea tunakamilisha jengo kisha tunaendelea kukosa huduma kwa sababu ya kukosa watumishi,” amesema.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji wa Kijiji cha Kenyamonta, Venance Lewanga amesema mradi huo ulioanza kutekelezwa mwezi Mei nwaka jana hadi sasa umefikia asilimia 54 za utekelezaji wake na unatarajiwa kukamilika Mwezi Juni mwaka huu.
Amesema hadi kukamilika mradi unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh181.7 milioni ambapo utahusisha ujenzi wa majengo ya wagonjwa wa nje, kujifungulia akinamama, huduma ya afya ya uzazi na mtoto pamoja na kichomea taka.
“Pia kutakuwa na choo kwaajili ya watumishi pamoja na wagonjwa sambamba na shimo la kuhifadhia kondo la nyuma,” amasema
Amesema mradi utakapokamilika unatarajiwa kuhudumia wakazi zaidi ya 3,000 kutoka katika kaya 638 kijijini hapo pamoja na maeneo jirani ambapo hadi sasa mradi huo umetumia zaidi ya Sh54.3 fedha ambayo imetokana na vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na wahisani na nguvu za wananchi.
Meneja wa TCB tawi la Bunda, Samuel Charles amesema benki hiyo imetoa msaada wa mabati 300 yenye thamani ya zaidi ya Sh27.3 milioni kwaajili ya kuezeka jengo la zahanti kijijini hapo.
Amesema msaada huo unatokana na sera ya benki hiyo ya kutoa sehemu ya faida inayopatikana kila mwaka kwaajili ya kusaidia miradi ya maendeleo katika jamii.
“Pia tunafanya hivi kwa kutambua umuhimu wa afya bora katika jamii na afya bora ni pamoja na huduma bora za afya na za uhakika hivyo kutokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo kijijini hapa tumeona kuwa na sisi tunawajibika kwa namna fulani katika utatuzi wa changamoto hiyo,” amesema.