Kilimanjaro. Wahenga waliwahi kusema mtaka nyingi nasaba, hupata mingi misiba, ndiyo ujumbe unaoendana na kilichomkuta Emmanuel Steven baada ya Mahakama ya Rufani kuikataa rufaa yake na kubariki kifungo cha maisha jela alichohukumiwa kwa kumbaka mtoto wa miaka sita.
Mbali na Jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo, Shaban Lila, Lugano Mwandambo na Lucia Kairo kubariki kifungo hicho cha maisha, lakini limebariki pia hukumu iliyomtaka kumlipa mtoto mwathirika fidia ya Sh1 milioni.
Baada ya kukamatwa kwa kosa hilo alilolitenda Oktoba 6, 2019, wazazi wa mbakaji huyo waliomba suala hilo limalizwe nyumbani na wakawa tayari kulipa fidia ya Sh700,000, lakini mama wa mtoto aliyebakwa aliwagomea.
Kutokana na msimamo huo wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, mbakaji huyo sasa amefika mwisho wa hatua ya rufaa kwa sababu mahakama hiyo ndio ya mwisho katika masuala ya rufaa na hii ina maana moja tu, atakufa akiwa gerezani.
Huruma pekee anayoweza kuipata mbakaji huyo aliyekuwa mkazi wa eneo la Tubuyu Wilaya ya Morogoro kama atapata msamaha wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ana mamlaka ya kikatiba ya kufanya hivyo.
Madaraka ya Rais ya kumsamehe mtu yeyote aliyepatikana na hatia ya kosa lolote, yamo katika ibara ya 15 (1) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2005.
Tukio la ubakaji lilivyokuwa
Mama wa mtoto huyo alikuwa amepanga katika nyumba moja na mama wa mrufani (mbakaji) pamoja na wapangaji wengine, wakati mbakaji huyo akiwa amepanga chumba katika nyumba nyingine umbali wa mita 200.
Asubuhi ya siku ya tukio, mama wa mtoto ambaye ni mfanyabiashara, alienda kwenye biashara zake na kuwaacha nyumbani watoto wake wawili, aliyebakwa pamoja na kaka yake, na wapangaji wengine.
Aliporudi nyumbani saa 10:00 alasiri, alikuta watoto wake wamechafuka, akaamua kuwaogesha lakini alipokuwa anamwagia maji mtoto wake wa kike, aligoma akisema ana maumivu sehemu za siri.
Maelezo hayo yalimfanya mama amchunguze akabaini sehemu zake za siri zimevilia damu iliyoganda kama mtu aliyekatwa na kiwembe na alipomdadisi ndipo akatoboa siri ya kubakwa na Emmanuel.
Alieleza kuwa Emmanuel alimwita aende kwenye chumba chake, alimfuata na alipoingia akafunga mlango kwa ndani na kumvua nguo na yeye akavua kisha akatoa uume wake na kuuingiza katika sehemu zake za siri na kumuumiza.
Baada ya kumbaka, alimpa penseli na kichongeo kama zawadi na kumtaka asije hata siku moja kumweleza mama yake juu ya kile alichomfanyia, na penseli na kichongeo hicho kilipokelewa mahakamani kama kielelezo.
Kutokana na maelezo hayo, wapangaji waliokuwepo walimfuata Emmanuel chumbani kwake kumuuliza juu ya suala hilo.
Mama wa mtoto alimsikia akikiri kufanya kitendo hicho na hata alipofuatwa na baba wa mtoto na kuulizwa, hakubadili maelezo yake alikiri kubaka.
Taarifa ilitolewa Polisi na mtoto alipewa fomu namba 3 (PF 3), alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro, daktari alithibitisha mtoto huyo kubakwa na kuumizwa vibaya ndipo mrufani alipokamatwa na Polisi.
Wazazi walivyotaka mambo yaishe
Kulingana na ushahidi wa mama wa mtoto ambao jopo la majaji hao liliunukuu kama ulivyo katika mwenendo wa kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Morogoro, kulikuwepo na jitihada za wazazi wa kijana huyo kutaka ‘walimalize’ kindugu.
Kwa mujibu wa ushahidi huo, baada ya mtoto wao kukamatwa, wazazi wa mbakaji huyo walimfuata mama wa mtoto na kutoa ofa ya Sh700,000 ili akubali walimalize jambo hilo nyumbani, lakini mama wa mtoto alikataa.
Ushahidi wa mama huyo uliungwa mkono na shahidi wa tatu na wa tano ambao ni ndugu wa baba wa mtoto aliyebakwa, ambao nao walisema waliombwa na baba mzazi wa mbakaji kulimaliza jambo hilo kinyumbani bila kufika mahakamani.
Mashahidi hao walisema kulifanyika vikao viwili, kimoja kilifanyika Oktoba 7, 2019 na kingine kikafanyika Oktoba 9,2019 sio tu kwamba mrufani alikitumia kukiri kutenda kosa la kumbaka mtoto huyo, pia alikitumia kuomba msamaha.
Lakini Ushahidi unaonyesha harakati hizo za wazazi wa mrufani hazikumshawishi mama wa mtoto akubali jambo hilo liishie nyumbani badala yake alikomaa hadi kuhakikisha haki ya mwanaye inapatikana.
Mbakaji alivyojitetea kortini
Katika utetezi wake mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Morogoro, mrufani huyo alikuja na hadithi tofauti ya kukanusha kutenda kosa hilo na kuibuka na utetezi kuwa hakuwepo kabisa siku na muda wa tukio linalotajwa na Jamhuri.
Alidai Oktoba 6, 2019 ambayo ndio inatajwa tukio hilo kufanyika, aliondoka asubuhi na kwenda kanisani na baada ya kutoka alienda shuleni saa 7:00 mchana na huko alikaa hosteli hadi saa 9:00 alasiri.
Alihudhuria darasa kwa ajili ya kujifunza hadi saa 12:00 jioni aliporudi nyumbani ndipo aliulizwa na mama yake kuwa amefanya jambo gani na alisema akamjibu hajui, na akaamua kurudi tena shule Jumatatu na Jumanne.
Alieleza Jumanne alivyorudi nyumbani baada ya kufanya mitihani, baba yake alimtaka akutane naye Saa 10:00 jioni na alipokutana naye aliulizwa tena kuhusu tukio la kumbaka mtoto huyo naye alilikana.
Kuhusiana na namna alivyokamatwa, mrufani huyo alieleza kuwa alikamatwa akiwa njiani akielekea shuleni.
Alisema alikutana na watu waliojitambulisha kuwa ni askari polisi ambao walimkamata na kumpeleka kituo cha Polisi.
Baada ya Mahakama kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, ilimtia hatiani na kumuhukumu kifungo cha maisha jela na kumlipa mtoto huyo fidia ya Sh1 milioni, lakini hakuridhika akakata rufaa Mahakama Kuu ambayo nayo ilimng’ang’ania.
Bado hakuridhika na kukata rufaa Mahakama ya Rufani na katika hukumu yao waliyoitoa Mei 16, 2024, jopo la majaji hao watatu walishikilia msimamo kuwa upande wa mashitaka ulikuwa umethibitisha kosa bila kuacha mashaka.