Askofu ajinyonga chanzo kikidaiwa ni madeni

Dodoma. Askofu Mkuu wa Makanisa ya Methodist, Joseph Bundala amejinyonga ofisini kwake kwa kutumia waya wa simu, akieleza chanzo ni madeni yaliyokuwa yanamkabili.

Tukio hilo lilitokea jana Mei 16 saa moja usiku, kwenye choo cha ofisi yake, iliyoko ndani ya kanisa la Methodist, Meriwa jijini Dodoma.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Alchelaus Mutalemwa, amesema leo Mei 17, 2024 kuwa jeshi hilo linachunguza tukio hilo.

“Uchunguzi katika eneo la tukio umekuta ujumbe unaeleza sababu za kujinyonga ni madeni na mgogoro uliopo katika uendeshaji wa shule binafsi. Uchunguzi bado unaendelea,” amesema.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Meriwa, Gervas Lugunyale amesema jana saa moja usiku alipigiwa simu na mmoja wa wachungaji wa kanisa hilo akiomba aende akawasaidie, kwani wamemkuta Askofu Bundala (55) akiwa amejinyonga ndani ya ofisi.

“Nilipofika nikapiga simu kwa watu wa usalama ili waje kutusaidia, lakini nikaingia ndani (ofisini), bahati mbaya nilikuta Baba Askofu ameshajichukulia maamuzi mkononi, amejinyonga, ameshafariki dunia,” amesema.

Amesema kwenye meza iliyokuwa ofisini kwake askofu huyo, walikuta waraka ambao kwa kifupi ulikuwa umeandika madeni anayodai na anayodaiwa.

Amesema Polisi walikwenda kuchukua mwili na kuupeleka kuuhifadhi.

“Ni tukio la ajabu, kubwa na linaumiza kwa sababu huyu ni askofu wa Tanzania ambaye watu wengi wanamwamini na wanamjua, inaonekana hakuwa na watu wa kuwaambia haya yaliyomsibu, angepata watu wa kumshauri,” amesema.

Amesema mchungaji wa kanisa hilo ambaye hakumtaja jina alimweleza kuwa aliagizwa na askofu kwenda dukani kumnunulia biskuti na soda kabla ya kwenda kwenye kipindi cha maombi eneo la Makole, jijini Dodoma.

“Alifanya hivyo na kwenda Makole kwenye kipindi, akamuacha peke yake akidhani anaendelea kuratibu kazi zake za uaskofu, lakini aliporudi saa moja usiku giza likiwa limeshaingia, alishtuka kuona mlango wa ofisi ukiwa wazi na ndani kuna giza,” amesema mwenyekiti huyo.

Amesema mchungaji huyo alimweleza kuwa alishtuka kuona hadi muda huo mlango ukiwa wazi na kwamba alimuacha askofu akiwa ndani, jambo lililomfanya aingie ndani ya ofisi.

Amesema alipoingia kwenye kiti hakuona mtu, ila alipokwenda kwenye choo cha ofisi ya askofu alikuta shuka ‘la Kimasai’ akidai huenda alitaka kulitumia kujinyonga.

Alieleza, “Inaonekana alitumia waya wa simu kufunga kwenye dirisha akajinyonga. Siku zote ukiwa na jambo shirikisha rafiki zako, ndugu zako, walimu, wazee waambie changamoto zako. Ukiwaambia unaweza kupata ushauri ukaokoa maisha yako,” amesema.

Mwenyekiti huyo alipoulizwa na Mwananchi kuhusu kiasi cha fedha alichokuwa anadai na kudaiwa amesema: “Zipo fedha zimeandikwa pale, lakini kwa sababu bado wanaendelea na upelelezi tukisema sana si sehemu yake.”

Mwenyekiti wa Shina Namba 11 Mtaa wa Meriwa, Kata ya Ipagala, Jonathan Mpando amesema wameumia kumpoteza Askofu Bundala kwa kuwa alikuwa na msaada hata katika kampeni za uchaguzi.

Pia naye aliwataka watu wanapopata matatizo katika maisha wajaribu kuwashirikisha watu wengine ili kupata ushauri badala ya kuchukua uamuzi wa haraka kama aliouchukua askofu huyo.

“Yeye alikuwa kiongozi ambaye tulikuwa tukimtegemea kupata ushauri na mambo mazuri, tulikuwa tunawakimbilia viongozi kama hawa,” amesema.

Mmoja wa majirani, Steven Magawa amesema wamesikitishwa na kifo cha kiongozi huyo kwa sababu alikuwa mwalimu wa matendo ya Mungu.

Mkazi wa Area D, Dizy Hillary amesema jana asubuhi alimpeleka mtoto shuleni (katika shule iliyopo kwenye kanisa hilo) na baada ya kumfikisha alirejea nyumbani.

“Niliona viti vimepangwa nje, nikajua kuwa nimewahi sana, hivyo nilimuacha mtoto na kurudi nyumbani. Lakini baada ya muda kidogo nilipigiwa simu na mwalimu akinitaka nikamchukue mtoto kwa kuwa wana msiba,” amesema.

Amesema alirudi shuleni na kupata habari kuwa askofu amejinyonga na kuwa, amepoteza amani baada ya kusikia tukio hilo.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Pentecoste Bible Fellowship Church in Tanzania (PBFCT), Jafeth Mapogo amesema kila kanisa lina utaratibu wake wa kuwazika viongozi wao wa dini, hivyo aliitaka jamii iwaache ili wafuate waliyojiwekea.

Askofu Mapogo amesema kila dini inajua kuua ni dhambi na alichokifanya askofu huyo ni kujihukumu kwa kukatisha uhai wake.

Yapo baadhi ya madhehebu ambayo hayatoi huduma kwa mtu aliyejiua.

Amesema amefanya hivyo kama binadamu na kuwataka watu kutoingilia majukumu ya Mungu ya kuhukumu bali wamwachie mwenyewe.

“Ila anastahili kuzikwa kama ilivyo kwa binadamu yeyote anayemaliza mwendo wake, awe na dini au asiwe nayo, awe askofu au muumini asiye na cheo ni lazima azikwe kwa heshima zote kwa sababu anastahili,” amesema.

Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu amesema kitendo cha kujiua ni sawa na kuua mtu mwingine yeyote, jambo ambalo ni kosa mbele za Mungu.

“Kwa sababu alikuwa ni mkuu wa dini ni haki yake kama ilivyo kwa binadamu yeyote, hawawezi kumtupa kama mzoga, ni lazima ahifadhiwe kwa heshima zote,” amesema Sheikh Rajabu.

Related Posts