Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekamilisha utekelezaji wa mradi wa kuongeza msukumo wa maji kwenye kitongoji cha Nyakahamba Kata ya Kerege Wilaya ya Bagamoyo na kuwezesha upatikanaji wa huduma kwa wakazi takribani 250. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa Mkoa wa DAWASA Mapinga, Abraham Mwanyamaki amesema kuwa mradi huu ulihusisha ulazaji wa bomba za inch nne kwa umbali wa kilomita moja na mita 600.
Amesema mradi huu ni muhimu kwa wananchi wa kata hiyo kwakuwa wengi hawakuwa na huduma ya maji ya uhakika kwa zaidi ya miaka mitano.
“Kwenye maeneo haya huduma ya maji ilikuwa ni ya kusuasua na kusababisha kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wa Nyakahamba juu ya upatikanaji hafifu wa huduma, lakini DAWASA ilisikia kilio na kuanza utekelezaji” alisema Mwanyamaki.
Ameongezea kuwa mradi huu umetekelezwa katika bajeti ya mwaka 2023/2024 kwa gharama ya Sh 30 milioni fedha ambazo ni mapato ya ndani na mradi umekamilika Mei mwaka huu.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyakahamba, Reinhold Nyaki amelezea utekelezaji wa mradi ulivyosaidia kupunguza changamoto za huduma hususani kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji na hivyo kupunguza muda wa kufanya shughuli za maendeleo na kijamii.
“Wananchi wangu walipitia kipindi kigumu sana cha ukosefu wa maji ya uhakika, lakini baada ya maboresho haya ya DAWASA kupitia mradi huu sasa wananchi wanapata huduma muda wote,” ameeleza Nyaki.