Kauli za Putin akiwa ziarani China, ndizo za kwanza kuhusu operesheni hiyo ya Kharkiv iliyoanza Mei 10, na kufungua uwanja mpya wa vita. Maelfu ya watu tayari wamelazimika kuyakimbia makaazi yao katika eneo hilo.
Kauli ya Putin imejiri saa kadhaa baada ya Ukrain kufanya shambulizi kubwa la droni katika rasi ya Crimea iliyonyakuliwa na Urusi, na kusababisha umeme kukatika katika mji wa Sevastopol na uharibifu nyinginezo ikiwemo ndege na hifadhi katika kambi ya jeshi la angani la Urusi.
Soma pia: Ukraine yashambulia Crimea kwa droni
Akijibu swali la mwandishi habari mjini Harbin China, Putin amesema ” nimesema hadharani kwamba ikiwa hali ya wao (Ukraine) kufyatua risasi kwenye makaazi itaendelea, tutalazimika kuunda eneo la usalama. Hicho ndicho tunayofanya kwa sasa. Lakini hakuna mpango wa kuukamata mji wa Kharkiv”.
Ameongeza kuwa vikosi vyake vinapiga hatua mbele kila siku kulingana na mpango.
Mapema Ijumaa, vikosi vya Ukraine vilikuwa vikipambana kuwazuia wanajeshi wa Urusi wasisonge mbele katika jimbo la Kharkiv.
Rais Zelensky asaini sheria ya kuwasajili wafungwa kwenye jeshi
Katika juhudi za kuongeza idadi ya wanajeshi, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amesaini sheria mbili. Moja itawaruhusu wafungwa kujiunga na jeshi na sheria nyingine ni kuongeza adhabu mara tano zaidi kwa watakaojaribu kuikwepa sheria hiyo.
Soma pia: Zelensky asema jeshi lake liko katika vita ‘vikali’ mpakani
Sheria ya wafungwa kujiunga na jeshi inaruhusu hilo kufanyika chini ya mkataba katika kipindi maalum, badala ya kutumikia vifungu vyao gerezani.
Katika tukio jingine Rais Putin amependekeza kuimarisha biashara yake ya nishati na China.
Kwenye ziara hiyo yake ya kwanza nje ya nchi tangu alipochaguliwa upya kuwa rais wa nchi yake kwa muhula wa tano, Putin alisema anaamini kwamba ushirkiano wa kimkakati katika sekta ya nishati kati ya nchi yake na China utaimarishwa zaidi.
Putin atafuta masoko mapya kwa nishati ya Urusi
Urusi imekuwa ikikabiliwa na shinikizo la kiuchumi kupata masoko mapya kwa nishati yake tangu uvamizi wake wa Ukraine mwaka 2022, ulipochochea mataifa ya Magharibi kuwekea nishati yake vikwazo.
Kulingana na kiongozi huyo wa Urusi, kwa sasa biashara kati ya nchi yake na China kwenye sekta ya nishati inakadiriwa kuwa dola bilioni 240, na amesema inaweza kuongezeka zaidi.
Urusi inapania hasa kujenga bomba la gesi kupitia Mongolia hadi China. Makubaliano kuhusu hilo yatasainiwa katika siku chache zijazo.
Soma pia: China na Urusi kuanza “enzi mpya” ya ushirikiano
Urusi pia inatumai kuimarishwa kwa ushirikiano na China katika sekta ya utengenezaji magari na kilimo. Hii ni kufuatia hatua ya kampuni za utengenezaji magari za nchi za Magharibi kuondoka kwenye mikataba nayo.
Vyanzo: APE, DPAE, EBU