Iringa kutumia Sh4.4 bilioni utekelezaji miradi ya maendeleo

Iringa. Halmashauri ya Manispaa ya Iringa inatumia zaidi ya Sh4.4 bilioni kutekeleza miradi ya maendeleo.

Imeelezwa kati ya fedha hizo, Sh2.6 bilioni zinaboresha miundombinu ya jengo la kitega uchumi linalojengwa eneo la stendi ya zamani, ambako pia kunajengwa jengo la ghorofa mbili litakalotumiwa na wafanyabiashara.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Mei 17, 2024 wakati wa ziara ya kamati ya fedha na uongozi ilipokuwa ikikagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa  kipindi cha robo ya tatu ya mwaka ya kuanzia Januari mpaka Machi 2023/24.

Ofisa uwekezaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Amiry Mtamike amesema ujenzi wa jengo la maendeleo unagharimu zaidi ya Sh1.8 bilioni ikiwa ni mapato ya ndani.

Amesema katika kutekeleza miradi ya kimkakati, halmashauri hiyo pia imeingia ubia na Jeshi la Magereza ambalo linawatumia wafungwa wenye fani ya ujenzi kujenga miradi hiyo.

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada ameitaka menejimenti ya halmashauri hiyo kuongeza juhudi ya usimamizi wa miradi hiyo, ili ikamilike kwa wakati na kuleta manufaa kwa wananchi .

“Nataka kuona ujenzi unaendelea kwa kasi na vifaa vyote vinavyohitajika vinafika eneo la kazi kwa wakati, ongezeni kasi ili ujenzi ukamilike kama tulivyokubaliana kwenye mkataba,” amesema Ngwada.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Kastori Msigala amesema amepokea maelezo yote ya kamati na ameahidi kuyafanyia kazi.

Related Posts