Mnamo mwezi Januari, mahakama hiyo iliiagiza Israel kuhakikisha kwamba wanajeshi wake hawafanyi mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina wakati wa operesheni yake ya kijeshi na pia ilitakiwa iruhusu misaada zaidi kuingia ndani ya Ukanda wa Gaza.
Afrika Kusini imeihimiza mahakama ya juu ya Umoja wa Mataifa itoe amri ya kusitishwa kwa operesheni hiyo ya mjini Rafah na kuitaka Israel iondoe wanajeshi wake mara moja. Israel hata hivyo imesisitiza kuwa oparesheni hiyo ni muhimu katika azma yao ya kulitokomeza kabisa kundi la Hamas.
Soma pia: Israel yakosoa kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini ICJ
Leo Ijumaa, Israel imejibu tuhuma zinazoikabili serikali ya mjini Jerusalem ikiwemo mauaji ya halaiki, mateso na kuzuia kwa makusudi misaada ya kibinadamu kupelekwa ukanda wa Gaza.
Israel hata hivyo imeielezea kesi hiyo kama isiyozingatia “ukweli wa mambo” wakati Afrika Kusini ikiwataka majaji katika mahakama ya ICJ kuamuru kusitishwa mara moja kwa oparesheni hiyo ya kijeshi.
Wakili wa Israel amekwenda mbali zaidi na kuitaja kesi ya Afrika Kusini “kama dhihaka” kwa Mkataba wa mauaji wa kimbari wa Umoja wa Mataifa.
Wakili huyo Gilad Noam ameiambia mahakama hiyo ya kimataifa ya haki iliyoko mjini The Hague, kwamba Israel inafahamu kwa kina juu ya idadi kubwa ya raia waliotafuta hifadhi mjini Rafah na pia, Israel inafahamu juu ya mbinu za wapiganaji wa Hamas kuwatumia raia kama ngao.
“Sauti za ving’ora zinaendelea kusikika kote nchini wakati makombora, na mashambulizi ya droni yakielekezwa dhidi ya Israel kutoka kila upande. Mji wa Rafah hasa ni kitovu cha shughuli za kigaidi.”
Noam ameendelea kuieleza mahakama hiyo kwamba hakujakuwepo “mashambulizi makubwa” mjini Rafah na kwamba jeshi la Israel limezingatia juhudi za kuwahamisha watu na kusaidia shughuli za kibinadamu.
Afrika Kusini: Hali katika ukanda wa Gaza ni ya kutisha
Hii ni kesi ya tatu inayohusu vita kati ya Israel na kundi la wanamgambo la Hamas tangu Afrika Kusini ilipowasilisha kesi ya jinai dhidi ya Israel kwa mara ya kwanza mnamo mwezi Disemba.
Kwa upande wake, Afrika Kusini imeiambia mahakama hiyo kwamba hali katika ukanda wa Gaza imefikia hatua ya kutisha na kwamba Israel inatishia kuendelea kuwepo kwa Wapalestina.
Mahakama hiyo ya kimataifa ya haki ICJ inaendelea kutathmini iwapo vitendo vya Israel katika ukanda wa Gaza vinakiuka mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1948 kuhusu mauaji ya kimbari.
Soma pia: ICJ yataka Israel kuruhusu misaada zaidi kuingia Gaza
Jana Alhamisi, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alitilia mkazo kuwa oparesheni ya ardhini ni sehemu muhimu ya kuliangamiza kundi la Hamas na kuzuia kutokea tena mashambulizi mengine ya kigaidi kama lile lililofanyika ndani ya ardhi ya Israel mnamo Oktoba 7.
Netanyahu ameliamuru jeshi la Israel kuendelea na oparesheni hiyo licha ya tahadhari iliyotolewa na Marekani kwamba maelfu ya Wapalestina huenda wakajikuta katikati ya mashambulizi.
Kwa upande wake, Waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant aliunga mkono kauli ya Netanyahu na kueleza kuwa, oparesheni hiyo itaendelea.