Kenya yakabiliwa na kiunzi kipya cha kutuma polisi Haiti – DW – 17.05.2024

Chama cha kisiasa cha Muungano wa Thirdway Alliance Kenya na wanachama wake wawili waliwasilisha malalamishi hayo siku ya Alhamisi (16.05.2024) , wakisema kwamba serikali imepuuza amri ya mahakama iliyotolewa mwezi Januari. Mahakama ilisema hatua ya kupelekwa polisi wa Kenya nchini Haiti inakiuka katiba na ni kinyume cha sheria.

Waliowasilisha hoja hiyo mahakamani hapo Alhamisi, wamesema walikuwa na ufahamu wa uhakika kwamba huenda askari polisi wa Kenya wakatumwa kabla ya Mei 23, wiki ijayo. Hivyo uharaka wa hoja hiyo kusikilizwa.

Hali bado ni tete Haiti

Kikosi cha wanajeshi wa kimataifa, kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, kitakachoongozwa na Kenya, na kimepewa jukumu la kusaidia polisi wa Haiti wanaokabiliwa na hali ngumu kudhibiti magenge ya uhalifu.

Kwa miongo kadhaa sasa, Haiti imekumbwa na umaskini, kukosekana kwa utulivu wa kisiasa na majanga ya asili.

Hatua inayotarajiwa ya kutumwa kwa kundi la kwanza la polisi wa Kenya nchini Haiti, itaendana na ziara ya Rais William Ruto mjini Washington ambako atakutana na Rais wa Marekani Joe Biden.

Kikosi cha kwanza kupelekwa Haiti

Jeshi la polisi nchini Haiti limeelemewa na wingi wa magenge na uhalifu unaofanywa na magenge hayo
Jeshi la polisi nchini Haiti limeelemewa na wingi wa magenge na uhalifu unaofanywa na magenge hayoPicha: Ralph Tedy Erol/REUTERS

Duru kutoka nchini Haiti zilisema mapema mwezi huu kwamba kikosi cha kwanza cha polisi 200 wa Kenya kilitarajiwa kufikia mjini Port-au-Prince ifikapo Mei 23. Kwa upande wake, serikali ya Kenya haijazungumzia tarehe hiyo, lakini chanzo cha wizara ya mambo ya ndani kililiambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba wanaweza kuwasili kufikia Jumanne ijayo.

Kenya iliahidi kupeleka hadi maafisa 1,000 wa polisi nchini Haiti. Hatua ambayo ilipokelewa vyema na Marekani na mataifa mengine ambayo yalifuta uwezekano wa kupeleka vikosi vyake huko.

Lakini kupelekwa kwa kikosi hicho kumekabiliwa na changamoto za kisheria. Mnamo Januari, Mahakama Kuu ya Kenya iliamua kwamba Baraza la Usalama la Kitaifa, ambalo liliidhinisha kutumwa kwa kikosi hicho, lilikuwa na mamlaka ya kutuma wanajeshi nje ya nchi na sio maafisa wa polisi.

Jaji alisema kuwa uamuzi huo ulikuwa kinyume cha katiba kwa sehemu, kwa sababu nchi hizo hazijatia saini makubaliano ya pande mbili kuhusiana na suala hilo.

Makubaliano ya pande mbili 

Mwezi Machi, rais William Ruto na waziri Mkuu wa Haiti wakati huo Ariel Henry walishuhudia utiaji saini wa makubaliano ya pande mbili katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Lakini kesi iliowasilishwa hapo jana mahakamani imewashutumu viongozi wa Kenya kwa utendaji kwa nia mbaya kwa kupuuza maagizo ya Mahakama Kuu. Na kuongeza kwamba, Haiti haikuwa imetoa ombi lolote rasmi la kutumwa kwa polisi wa Kenya.

Related Posts