Mashauri ya ndoa yaongezeka | Mwananchi

Dodoma. Mashauri yanayohusu ndoa yaliyoshughulikiwa na kupitia Baraza la Usuluhishi la Ndoa yameongezeka kwa asilimia 8.3.

 Hayo yamesemwa leo Mei 17,2024 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2024/25.

Bajeti hiyo imeomba Bunge kuwaidhinishia Sh67.90 bilioni kwa mwaka 2024/25 ikiwa ni pungufu ya bajeti ya mwaka 2023/24 ya Sh74.22 bilioni.

Amesema katika kuhakikisha kuna ustawi na utulivu wa familia, wizara kupitia maafisa Ustawi wa Jamii, imeendelea kuratibu huduma za usuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia, kupitia Baraza la Usuluhishi wa Ndoa la Kamishna wa Ustawi wa Jamii.

Amesema hadi kufikia Aprili 2024, mashauri yaliyoshughulikiwa yalikuwa 31,380 ikilinganishwa mashauri 28,773 yaliyoshughulikiwa mwaka 2022/2023.

Amesema kuwa kumekuwa na ongezeko la mashauri 2,607 sawa na asilimia 8.3.

“Natoa wito kwa viongozi wa dini zote kuendelea kutoa mafunzo kwa wanandoa, wanaofunga ndoa na kwa vijana kupitia mikusanyiko katika madhehebu yao, ili kuwaandaa kubeba majukumu ya ndoa kabla ya kuingia katika ndoa,”amesema.

Related Posts