Mtindo wa maisha unavyowaweka hatarini wavuvi kupata homa ya ini

Dar/mikoani. Takwimu za Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS), zinaonyesha mikoa ya Mara na Shinyanga inaongoza kwa ugonjwa wa homa ya ini miongoni mwa wachangiaji damu kwa asilimia 9.3 na 7.4 mtawalia.

Takwimu hizo ni za mwaka 2020, ambazo NBTS ilipokea sampuli 263,119 za wachangiaji damu kwa Tanzania Bara, miongoni mwao 15,923 (asilimia 6.1) walikuwa na virusi aina ya Hepatitis B na 6,914 (asilimia 2.6) walikuwa na virusi aina Hepatitis C.

Katika mahojiano na baadhi ya wakazi wa mikoa ya Mara, Shinyanga na Mwanza, wavuvi na wachimba madini wanatajwa kuwa katika hatari zaidi ya kupata ugonjwa wa homa ya ini kutokana na mtindo wao wa maisha.

Katika fukwe za Mchangani, Gana, Kerebe, Burubi, Ikuza na Kanyara zilizoko Ziwa Victoria, ambazo Mwananchi ilizitembelea, kuna nyumba za kulala wageni zisizo rasmi (gesti bubu), miongoni mwa wahudumu hawana malipo ya mshahara, bali hutegemea fedha kutoka kwa wateja, wengi wakiwa wavuvi.

“Hatuna kiwango maalumu cha fedha tunacholipwa… inategemea bosi ataamua vipi, lakini tunapata kutoka kwa wavuvi. Wakipata chochote (fedha) baharini wakija kunywa basi mnakubaliana bei, unaenda kulala naye,” anasema Anjela Kapota, mhudumu eneo la Kerebe.

“Si wote natumia nao kondomu, inategemea alivyo na hela anayoitoa,” anasema.

Kauli ya Anjela inaungwa mkono na mvuvi Jephta Machandalo, anayesema: “Gesti unazoziona huku (maeneo ya uvuvi) ni kama madanguro, baa wahudumu hawana mishahara. Wakikaa muda mrefu eneo moja wanahama kwenda sehemu nyingine ya wavuvi na kule wanaonekana wapya.”

Machandalo, ambaye ni Katibu wa Chama cha Wavuvi Tanzania, anasema mambo yanayofanyika kwenye kambi za uvuvi ni hatarishi kwa afya.

Meckzedeck Shija, mvuvi katika Ziwa Victoria jijini Mwanza, anasema kuwa mbali na familia kwa muda mrefu husababisha kuanzisha mahusiano yanayowaweka katika hatari ya kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na homa ya ini.

Anasema wapo wenzao wameugua homa ya ini na wengine kufariki dunia lakini hawana elimu ya kutosha ya kujikingi na ugonjwa huo.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya ndani katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere mkoani Mara, Dk Augustino Makenya anasema:

“Hata kiwango cha maambukizi ya VVU kwa mkoa wetu (Mara) kipo juu. Kambi za wavuvi na migodi ya uchimbaji madini ni maeneo ambayo pamoja na mambo mengine kuna vitendo vya ngono isiyo salama.”

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na mtafiti wa Chuo Kikuu Katoliki cha Afya na Sayansi Shirikishi Bugando, mkoani Mwanza, Dk Semvua Kilonzo anasema mtindo wa maisha ya wavuvi katika Ziwa Victoria ndiyo sababu ya ukubwa wa tatizo hilo kanda ya ziwa.

“Ugonjwa wa homa ya ini nchini ni tishio. Kwa kanda ya ziwa kuna utafiti tuliufanya na wenzangu tukaona shughuli za uvuvi zinawasababisha kuwa katika hatari ya kupata homa ya ini na VVU, tumethibitisha kitaalamu kutokana na mazingira na tabia zao,” anasema Dk Kilonzo.

Miongoni mwa tabia hizo, Dk Kilonzo anasema ni kushiriki ngono na watu tofauti, na kuchangia baadhi ya vitu vyenye ncha kali.

Akithibitisha shughuli za uvuvi kuwa miongoni mwa sababu za uwapo wa homa ya ini kanda ya ziwa, Dk Kilonzo anasema hata wagonjwa wengi wanaowapokea wanatokea jamii za wavuvi.

“Kwa kiwango fulani wagonjwa tunaowapata hapa pia wanatokea katika wilaya ambazo uvuvi ni shughuli kuu, ikiwamo Sengerema, wengi wanakuja katika hatua za mwisho za homa ya ini, ikiwamo saratani ya ini.

“Tumefanya tafiti nyingi za homa ya ini, kitu kikubwa watu wengi wazima hawajapata chanjo, Watanzania wengi wapate chanjo ili tujikinge. Watu wengi wana maambukizi ya homa ya ini lakini hawajui, kwa hiyo wanakuja hospitalini wakiwa katika hatua za mwisho kabisa,” anasema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wavuvi Tanzania, Bakari Kadabi anasema wanaendelea kutoa elimu, kwani mazingira na mitindo yao ya maisha yanawaweka katika hatari a magonjwa mengi.

“Tunachokifanya ni kuwapa wavuvi elimu ya magonjwa ya maambukizi na kuwataka kuzingatia usafi katika maeneo yao ya kazi. Kimsingi maeneo wanayoishi wavuvi kuna magonjwa mengi kutokana na mazingira na mtindo wa maisha,” anasema Kadabi.

Kadabi anasema taarifa ya wao kuwa hatarini katika maambukizi ya homa ya ini hawakuijua lakini wanashuhudia magonjwa kama hayo (homa ya ini) hivyo wanaendelea kutoa elimu kwa wenzao.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Bugando kwa kushirikiana na Wizara ya Afya ulioitwa ‘Maambukizi ya virusi vya Hepatitis B, mambo yanayohusiana, ujuzi na chanjo jijini Mwanza’ uliofanyika Julai hadi Agosti 2023 ulionyesha ngono zembe ni sababu mojawapo ya maambukizi ya homa ya ini mkoani Mwanza.

“Sababu zilizogundulika kuongeza maambukizi ya homa ya ini Mwanza ni umri mkubwa, kushirikiana vitu vyenye ncha kali, na kuwa na mwenzi mmoja au zaidi wa ngono aliye na maambukizi ya homa ya ini na kutotumia kondomu wakati wa kujamiiana,” imesema sehemu ya utafiti uliochapishwa katika jarida la kimataifa la Elsevier.

Utafiti huo unaonyesha Mwanza ulichaguliwa kwa sababu ni miongoni mwa mikoa yenye maambukizi makubwa ya homa ya ini miongoni mwa makundi mbalimbali, wakiwemo wafanyakazi wa afya, wajawazito, wanawake, watoto na watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi.

Utafiti pia uligundua idadi kubwa ya wanaume katika kaya wana maambukizi ya homa ya ini, ikipendekezwa hatua za kuzuia zinapaswa kuwalenga wanaume zaidi.

Matokeo ya utafiti huo yanashabihiana na majibu ya Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP), Dk Aneth Rwebembela, anayesema njia zinazotumika kuambukiza VVU ni sawa na homa ya ini kwa kiwango kikubwa.

“Hii ni kwa sababu homa ya ini B huambukizwa kwa njia zilezile zinazoambukiza VVU,” amesema.

Dk Kilonzo anasema virusi vya homa ya ini ndivyo vinasababisha aina ya ugonjwa wa ini husika na hata takwimu za maambukizi yake hutofautiana.

“Virusi vya homa ya ini vipo vya aina nyingi kama vile A, B, C, D na E, kwa hiyo hapo ndipo huzaliwa Hepatitis A, B, C, D na E, huku C na B, hasa B ndiyo ipo sana nchini,” anafafanua Dk Kilonzo.

Kuhusu aina hizo za homa ya ini nchini, Meneja wa NASHCoP, Dk Aneth anasema utafiti unaofanyika nchini kila baada ya miaka mitano, uliofanyika mwaka 2016/2017 unaonyesha ukubwa wa tatizo nchini kwa homa ya ini B ni asilimia 4.1 na homa ya ini C ni asilimia moja.

“Katika utafiti huo tatizo lilionekana kubwa kwa baadhi ya makundi kama wajidungao (asilimia 6.3), wajawazito (asilimia 8.3) na vijana (asilimia 7.9). Kadiri ya huduma na taarifa zinavyoendelea kutolewa, takwimu zimeendelea kuonyesha ukubwa wa tatizo,” anasema Dk Aneth.

Dk Aneth anasema katika kupambana na homa ya ini, Serikali inahuisha mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wenye lengo la kutokomeza Ukimwi, magonjwa ya ngono na homa ya ini ifikapo mwaka 2030.

“Ili kufanikisha hilo Serikali kupitia Wizara ya Afya tayari imeunganisha uratibu na usimamizi wa huduma za magonjwa haya matatu chini ya programu moja. Katika mpango mkakati Serikali imejikita kwenye afua mbalimbali katika kupambana na homa ya ini,” anasema Dk Aneth.

Afua hizo anasema ni kujumuisha elimu ya homa ya ini katika programu ya kampeni za Ukimwi ili kuongeza uelewa na kutoa elimu kwa jamii kuhusu ugonjwa wa homa ya ini, namna unavyoambukizwa, chanjo na upimaji pamoja na matibabu ya homa ya ini.

Pia, Serikali inatoa huduma ya upimaji na chanjo ya homa ya ini kwa wajawazito na wanaonyonyesha, lengo ni kufikia asilimia 80 ya wajawazito wote nchini ifikapo mwaka 2025.

Huduma ya upimaji pia inatolewa kwa watu wote na makundi yaliyo katika hatari zaidi kama wanaojidunga dawa za kulevya.

Imeandaliwa kwa msaada wa Bill  & Melinda Gates

Related Posts