Muhimbili kujenga hosteli za kufikia ndugu wa wagonjwa

Dodoma. Hospitali ya Taifa Muhimbili, imeandaa  mpango wa uendelezaji wa eneo la hospitali (Master plan) ambapo miongoni mwa maeneo yatakayokuwepo kwenye mpango huo ni kujenga hosteli za bei nafuu ambazo ndugu wa wagonjwa watakaa.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel ameyasema hayo leo Mei 17,2024 wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu,  Hawa Mwaifunga.

Mwaifunga amehoji ni lini Serikali itatenga eneo maalumu katika hospitali za Muhimbili na Taasisi ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (Moi), kwa ajili ya watu wasio na ndugu Dar es salaam wanaopeleka wagonjwa wao kupata matibabu.

Akijibu swali hilo, Dk Mollel amesema Hospitali ya Taifa Muhimbili, tayari imeandaa mpango wa uendelezaji wa eneo la hospitali (Master plan) ambapo mojawapo ya maeneo yatakayokuwepo kwenye mpango huo ni kujenga hosteli za bei nafuu ambazo ndugu wa wagonjwa watakaa.

“Kwa mwaka wa fedha 2024/25, Hospitali ya Muhimbili  imeandaa mpango wa mashirikiano na sekta binafsi ili ndugu wasio na mahala pa kulala toka ndani na nje ya nchi waweze kupokelewa katika hosteli zilizo karibu na hospitali hiyo kwa gharama nafuu,”amesema.

Katika maswali ya nyongeza Mwaifunga amesema watu wanaokwenda kuangalia wagonjwa wanaotoka nje ya Dar es Salaam wamekuwa wakilala katika vibanda vya chipsi na majengo ya pembeni wakisubiri papambazuke waende kuona  wagonjwa wao.

“Serikali haioni umuhimu wa kufanya dharura ili angalau hawa wanaoleta wagonjwa waweze kupata mahali pa kujisitiri?”amehoji.

Akijibu maswali hayo, Dk Mollel amesema Serikali inatambua changamoto hiyo na kwa kampasi ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili pekee wagonjwa wanaoingia kwa siku ni 12,000.

Amesema endapo kila mgonjwa mmoja akisindikizwa na watu wawili maana yake ni watu 24,000.

“Kuna watu wengi wanakuja na hawana uwezo wa kulipa, kuna wagonjwa wanakuja na magonjwa mbalimbali.  Ukizungumzia wakinamama na mtoto ni Sh124 bilioni zinatumika kwa mwaka kwa ajili ya kuwahudumia,”amesema.

Amesema wanaelekeza nguvu zaidi lakini kwenye mpango kabambe (Hospitali ya Taifa ya Muhimbili) na kuwa wanaenda kujenga maeneo ya namna hiyo.

Hata hivyo, amesema wanashirikiana na sekta binafsi katika utekelezaji wa mpango huo.

Related Posts