Musoma. Mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Masaunga wilayani Bunda anayedaiwa kufanyiwa vitendo vya ukatili na mwalimu mkuu wa shule hiyo, Vicent Nkunguu, ikiwamo kubakwa, ameomba kuhamishwa kutoka shule wakati kesi ikiendelea.
Akizungumza leo Mei 17,2024, mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 16 amewaomba wadau na Serikali kumtafutia shule mbadala ili aweze kusoma vizuri kwani kuendelea kusoma Masaunga kunamwathiri kiakili na kisaikolojia.
Amesema licha ya kuwa anaendelea na masomo katika shule hiyo, lakini mazingira sio rafiki kwake jambo ambalo linaweza kumrudisha nyuma kitaaluma.
Mwanafunzi huyo ambaye anatamani kusoma hadi chuo kikuu na kuwa Waziri wa Nishati, amesema kadiri siku zinavyokwenda anaona ndoto yake hiyo inaweza isitimie, kwani anapata unyanyapaa baada ya taarifa za tukio hilo kusambaa.
“Mtihani wa mwisho nilifanya 2024 wakati tunafunga shule na nilikuwa wa 10 kati ya wanafunzi 194 lakini sasa hivi sijui kama nitaingia tena kwenye 10 bora, maana napata wakati mgumu kila nikikumbuka tukio na wenzangu wanavyonitania”amesema.
Kutokana na hali hiyo, ameomba kuhamishiwa shule ya bweni ili aweze kubadili mazingira na kuweza kusoma vizuri kwa maelezo kuwa akiwa nje ya eneo la tukio itakuwa rahisi kwake kulisahau tukio hilo aliloliita la kidhalilishaji.
Mama wa mwanafunzi huyo amesema anatamani mtoto wake apate mazingira mapya jambo litakalomsaidia katika makuzi yake kwa ujumla, lakini kutokana na uwezo wao mdogo hana namna ya kumhamishia shule nyingine.
“Tunatamani kama inawezekana apate uhamisho ili aendelee na masomo yake huko kwingine na hii haitamsaidia kwenye suala la elimu pekee bali hata katika makuzi yake kwa ujumla,”amesema mama wa mtoto huyo.
Amesema, “mfano hii wiki yote hajaenda shule kwa sababu kuna vitu nilihisi ni hatari, na ukumbuke sasa hivi wanajiandaa na mitihani ya muhula wa kwanza sijui atafanyaje hiyo mitihani.”
Kwa upande wake, baba wa mwanafunzi huyo alidai tukio hilo limemgharimu kiasi kikubwa cha fedha hadi kulazimika kuuza baadhi ya vitu vyake vya ndani ili aweze kulipia gharama za matibabu, kwani mtoto alilazwa kwa siku 10 mfululizo.
Walichokisema RPC Mara, DC Bunda
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salum Morcase alipoulizwa na gazeti hili amesema hana taarifa sahihi juu ya hali ya kesi hiyo, kwa sasa ingawa mtuhumiwa tayari alishafikishwa mahakamani na yuko nje kwa dhamana ambayo ni haki yake.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vicent Naano amesema suala la kumuhamisha mwanafunzi huyo linawezekana na kuwataka wazazi wa mtoto huyo kuwasiliana na ofisi yake au ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri kwa ajili ya kupewa utaratibu.
“Siku alipotoka hospitali nilimwambia mama yake kuwa jambo hilo la kumuhamisha mtoto linawezekana ila kuna taratibu za kufuata ikiwa ni pamoja na kushirikisha ofisi ya mkurugenzi lakini hadi sasa sijamuona tena.”
“Suala la mtoto kupata elimu ni la msingi na kwa lile tukio ni vema akabadilishiwa mazingira kwa hiyo kama wapo tayari wawasiliane na mimi moja kwa moja au mkurugenzi,”amesema Dk Naano alipozungumza na gazeti hili.
Mwanafunzi huyo anadai kubakwa na kulawitiwa kisha kunyweshwa sumu siku iliyofuata kwa kile alichodai lengo ni kupoteza ushahidi wa tukio. Matukio hayo yanadaiwa kufanywa na mtuhumiwa nyumbani kwake kati ya Machi 8 na 9,2024.