Rudi nyuma hadi Januari 12, 2022, wakati wa mashindano ya AFCON 2021, mchezo wa hatua ya makundi kati ya Tunisia na Mali.
Mwamuzi kutoka Zambia, Janny Sikazwe, alifanya ‘blanda’ ya mwaka, dakika ya 85 akapuliza filimbi ya kumaliza mchezo huku Mali ikiongoza 1-0.
Tunisia wakalalamika sana, naye akaanzisha tena mchezo lakini akaumaliza tena dakika ya 89 na sekunde 43.
Sekunde 17, zilizobaki unaweza kuziona ni chache lakini kwenye mpira hizi ni nyingi sana na zinaweza kuleta matokeo mengine kabisa.
Hizi ndizo sekunde ambazo Real Madrid chini ya Carlo Ancelotti au Bayer Leverkusen chini ya Xabi Alonso, zimekuwa zikileta stori tofauti.
Chini ya Carlo Ancelotti, Real Madrid imekuwa na miujiza mikubwa sana ya kupindua meza katika sekunde hizi, hasa kwenye mashindano ya Ulaya.
Rejea fainali ya ligi ya mabingwa mwaka 2014, bao la kusawazisha la Sergio Ramos, sekunde ya mwisho ya mchezo.
Unaikumbuka robo fainali ya ligi ya mabingwa mwaka 2022 dhidi ya Manchester City?
Wakiwa nyuma 1-0 nyumbani Santiago Bernabeu, Real Madrid ilipata mabao mawili ya sekunde 17 za mwisho kupitia Rodygo na kubadilisha ubao.
Orodha ni ndefu sana, ikiwemo hii ya José Luis Mato ‘Joselu’ dhidi ya Bayern Munich kwenye nusu fainali ya mwaka huu.
Stori ya Real Madrid ya Carlo Ancelotti na mabao ya sekunde 17 za mwisho inaweza isiwe kubwa kama ile ya Bayer Leverkusen chini ya mwanafunzi wa Ancelotti, Xabi Alonso.
Hii timu kutoka Ujerumani imekuwa na hadithi ya kuvutia sana kwa mabao yake ya sekunde 17 za mwisho, siyo tu kwenye mashindano ya Ulaya, bali hata kwenye ligi ya nyumbani.
Usiku wa Mei 9, 2024, wamba hawa waliweka rekodi ya Ulaya ya kucheza mechi nyingi bila kupoteza.
Sare ya 2-2 dhidi ya AS Roma ya Italia kwenye nusu fainali ya Europa League, iliwafanya wafikishe mechi 49 na kuivunja rekodi ya Benfica ya Ureno iliyodumu kwa miaka 59.
Lakini sare hii nayo ilitokana na hisani ya sekunde 17 za mwisho.
Leverkusen sasa wanaitwa Neverlusen, yaani wasiopoteza, lakini yote hiyo ni kwa hisani ya sekunde 17 za mwisho.
Kwenye ligi ya ndani, Leverkusen msimu huu imefunga mabao 17 ndani ya sekunde 17 za mwisho.
Kwa kifupi Real Madrid ya Carlo Amcelotti na Bayer Leverkusen ya Xabi Alonso wamekuwa magwiji sekunde 17 za mwisho.
Timu hizi mbili ziko kwenye fainali za mashindano ya Ulaya, na zote zikifaidika na mabao ya sekunde 17 za mwisho.
Kama watashinda fainali hizo, watakutana kwenye mchezo UEFA Super Cup ambao hukutanisha mabingwa wa mashindano ya Ulaya.
Sasa hebu rejea mkasa wa Janny Sikazwe kumaliza mchezo kabla ya sekunde hizi 17 za mwisho.
Angekuwa anachezesha mechi hizi maana yake angeunyima ulimwengu wa soka fursa ya kushuhudia miujiza hii.
Real Madrid wasingekuwa fainali msimu huu na misimu mingine huko nyuma, Bayer Leverkusen isingeweka rekodi ya Ulaya kama wanavyofanya sasa.
Timu hizi mbili zimeingia fainali ya mashindano ya Ulaya na endapo zitashinda fainali zao basi zinaweza kukutana kwenye UEFA Super Cup.
Kama ikiwa hivyo, dunia inaweza kusubiri kushuhudia miujiza ya sekunde 17 za mwisho.
Lakini hiyo haitawezekana kama mwamuzi atakuwa Janny Sikazwe, maana anaweza kumaliza mchezo kabla ya mida wale na kutunyima bao la sekunde 17 za mwisho.
Hapa Tanzania pia akina Sikazwe wapo. Kwenye mchezo wa Biashara United Mara na Azam FC uliofanyika Uwanja wa Karume mjini Musoma, Novemba 30, 2020, mwamuzi Abdallah Mwinyimkuu alimaliza mchezo dakika ya 89 na sekunde 25.
Lakini baadaye akagundua kwamba alifanya makosa akilalamikia saa yake.