NBC yazindua bima ya afya kwa wakulima

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kushirikiana na kampuni ya Bima ya Assemble Insurance imezindua huduma ya Bima ya Afya kwa wakulima nchi nzima ikilenga kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa kundi hilo.
Hatua hiyo inatajwa kuwa itasaidia kuimarisha sekta ya afya ambayo ni moja ya nguzo muhimu katika ukuaji wa kilimo nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Kupitia huduma hiyo wakulima na familia zao wanaweza kupata huduma ya bima ya afya kwa malipo ya kiasi cha Sh. 450,000 kwa mwaka.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Zuwena Omary (Katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kampeni ya ‘Shinda Mechi Zako Kinamna Yako na NBC Shambani’ inayoratibiwa na benki ya NBC mahususi kwa wakulima wa zao la ufuta mkoani Lindi na wilaya za Masasi na Nanyumbu mkoa wa Mtwara. Wengine ni pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Mikakati wa Benki NBC, Msafiri Shayo (wa tatu kushoto), Meneja wa Benki ya NBC tawi la Lindi, Ivon Mapunda (wa pili kushoto), Mwenyekiti wa chama cha ushirika cha TANECU Hamis Chipola (Kulia), wakulima na maofisa wa benki hiyo.

Hafla ya uzinduzi wa huduma hiyo imefanyika leo Ijumaa mkoani Lindi ikienda sambamba na uzinduzi wa kampeni ya ‘Shinda Mechi Zako Kinamna Yako na NBC Shambani’ mahususi kwa wakulima wa zao la ufuta mkoani Lindi na wilaya za Masasi na Nanyumbu mkoa wa Mtwara.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Zuwena Omary aliongoza hafla hiyo iliyohusisha viongozi wa vyama vya msingi na ushirika mkoani Lindi na Mtwara huku Mkuu wa Kitengo cha Mikakati wa Benki NBC, Msafiri Shayo akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Theobald Sabi kwenye tukio hilo muhimu.

Akizungumzia hatua ya benki hiyo, Zuwena pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa kutoa kipaumbele kwa wakulima nchini alisema ujio wa huduma ya Bima ya Afya mahususi kwa wakulima ni ukombozi muhimu kwa kundi hilo na inaunga mkono na dhamira ya serikali ya kuhakikisha makundi yote ya wananchi yanapata huduma ya bima ya afya.

“Ujio wa huduma hii ya Afya ya NBC ni mkombozi muhimu kwa wakulima kwasababu watoa huduma wengi wa bima ya afya wameshindwa kuwa na mifumo rafiki katika kuwafikia wakulima.

“NBC wameiona changamoto hii na kwa kuwa wapo karibu na wakulipa kupitia huduma mbalimbali za kibenki wataweza kufanikisha mpango huu kwa urahisi na ufanisi zaidi. Sasa wakulima na familia zao watakuwa salama kuanzia sasa.’’ amesema Zuwena huku akitoa wito kwa wakulima kuchangamkia fursa hiyo.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Zuwena Omary (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa kampeni ya hiyo. Wengine ni pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Mikakati wa Benki NBC, Msafiri Shayo (wa saba kushoto), Viongozi wa vyama vikuu vya ushirika mikoa ya Lindi na Mtwara, wakulima na maofisa wa benki hiyo.

Akizungumzia kampeni ya ‘Shinda Mechi Zako Kinamna Yako na NBC Shambani’ Zuwena alionyesha kuridhishwa zaidi na namna kampeni hiyo ilivyohusisha suala zima la utoaji wa elimu ya fedha kwa wakulima, hatua aliyosema itasaidia zaidi kukabiliana na changamoto ya matumizi ya pesa yasiyozingatia vipumbele muhimu inayowakabili wakulima wengi mkoani humo.

“Pamoja na zawadi mbalimbali kwa wakulima ikiwemo pampu za kupulizia dawa, dawa za kuua magugu na konokono, baiskeli na pikipi ambavyo ni muhimu sana kwa wakulima, ubora wa kampeni hii upo zaidi kwenye eneo la elimu ya fedha kwa wakulima na hapa nawasihi sana washiriki wa semina hizi mzingatie zaidi,’’ amesema Zuwena ambae pia alitumia fursa hiyo kuwasisitiza viongozi hao wa vyama vya msingi na ushirika kuisaidia serikali katika kusimamia udhibiti za pembejeo za kilimo zinazotolewa bure na serikali.

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mikakati wa Benki NBC, Msafiri Shayo alisema ujio wa huduma ya Bima ya Afya kwa wakulima pamoja na uzinduzi wa kampeni ya ‘Shinda Mechi Zako Kinamna Yako na NBC Shambani’ ni muitikio wa benki hiyo katika kuunga mkono jitihada za serikali kuboresha sekta muhimu za afya na kilimo nchini kupitia mapinduzi ya huduma za kifedha.

“Kupitia program hizi mbili tulizizindua leo NBC tunakwenda kugusa maeneo muhimu kitaifa na yanayogusa watu wengi zaidi ambayo ni sekta ya afya na kilimo ambavyo kimsingi vinaingiliana sana na vinategemeana.’’

“Kwa kushirikiana na kampuni ya BIMA ya Assemble wakulima kote nchini wanafikiwa moja kwa moja na huduma ya afya kwa kiasi cha sh 450,000 tu kwa mwaka na kupitia kampeni yetu ya ‘Shinda Mechi Zako Kinamna Yako na NBC Shambani’ wakulima wa zao la ufuta mkoani Lindi na wilaya za Masasi na Nanyumbu watanufaika kupitia elimu za fedha na elimu ya kilimo cha kisasa pia wakipata huduma bora za kibenki mahususi kwao huku wakiwa kwenye nafasi ya kujishindia zawadi mbalimbali zikiwemo pikipiki, baiskeli na dawa kuua wadudu waharibifu wa mazao yao,’’ amesema.

Wakizungumza kwa niaba wakulima hao, Wenyeviti wa vyama vya ushirika vya TANECU na MAMCU, Hamis Chipola na Azam Mfaume ‘Jula jula’ msawalia, pamoja na kuishukuru na kuipongeza benki hiyo kwa program hizo muhimu walielezea namna wakulima wanavyopata wakati mgumu kutokana changamoto ya ukosefu wa huduma ya bima za afya huku wakibainisha kuwa ujio wa huduma hiyo kupitia NBC itakuwa ni msaada mkubwa kwao na familia zao.

Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo wadogo, Lariba na wakulima kutoka Benki ya NBC, Raymond Urassa akizungumza na wakulima hao na viongozi wa vyama vya msingi na ushirika mikoa ya Lindi na Mtwara.

“Hata hivyo tunaendelea kutoa wito kwa taasisi za fedha ziendelee kuwa karibu na sisi wakulima kwa kuwa nasi pia kwasasa tumeazimia kuwa karibu na taasisi zinazotujali kupitia huduma zinazotugusa kama hizi za NBC.

“Wakulima tunahitaji mikopo hususani mwanzo wa msimu ili itusaidie kuboresha uzalishaji wetu na sio waje kipindi cha msimu wa mauzo nasi tutawakataa,’’ amesema Mfaume kauli iliyoungwa mkono na mwenzie Chipola.

Related Posts