“..USHAHIDI upi mwingine unahitaji?” Hakusema mdomoni. Moyo wake ulikuwa unaongea. Asingeweza kutamka hivyo mdomoni wakati akirekodi video yake ya kuaga. Kylian Mbappe. Amewaaga PSG mapema wiki hii. Anaondoka zake PSG. Lilikuwa suala la muda tu.
Alionekana mtulivu wakati akiaga. Mara ya mwisho serikali ya Ufaransa iliingilia kati kuondoka kwake. Alipoamua kubaki ikawa sherehe kwa Wafaransa.
Labda kwa wakati huo hawakuona sababu za msingi sana kwa alama yao ya taifa kuondoka nchini kwao. Hawakunong’ona vizuri sana wakati huo.
Pengine kulikuwa na shutuma kuhusu maamuzi yake aliyoanza kuyafanya tangu msimu uliopita wakati alipoweka wazi asingesaini mkataba mpya klabuni hapo.
Kwa hasira PSG wakamuacha katika safari yao ya maandalizi ya msimu mpya waliyoifanya Marekani. Hata hivyo aliendelea na msimamo wake.
Baadaye PSG wakaamua kumrudisha kwa ajili ya kuwasukuma katika msimu mpya ambao ungekuwa wa mwisho klabuni hapo. Hata hivyo, njiani ilihisiwa huenda mambo mengi yangetokea. Huenda angebadili msimamo wake.
Wakati mwingine mambo huwa ni mengi. Unakumbuka kuna wakati alionekana anaenda Real Madrid lakini ghafla akabadili maamuzi na kubakia PSG?
Hata hivyo, safari hii hakukuwa na maamuzi hayo. Na kama ulitakiwa ushahidi wa wazi wa kutobadili maamuzi basi ni pale wiki iliyopita alipoondoka uwanjani akiwa ameinamisha kichwa chini PSG ikitolewa katika michuano ya Ligi ya mabingwa barani Ulaya. Angefanya nini zaidi?
Unatolewaje na Borussia Dortmund baada ya uwekezaji mkubwa ambao PSG wamefanya?
Lakini hapo hapo Mbappe angeiweza wapi kazi ambayo imewashinda Edinson Cavani, Zlatan Ibrahimovic, Angel Di Maria, Neymar na Lionel Messi? Ubingwa wa Ulaya umeendelea kuwa ndoto kwa PSG.
Ubingwa wa Ufaransa ni kitu kidogo cha kawaida kwa kila mchezaji ambaye anavaa jezi ya PSG katika zama hizi. Kazi kubwa ni kuipa PSG ubingwa wa Ulaya na imewashinda wengi.
Sasa Mbappe anaelekea zake Real Madrid. Ni suala la muda tu. Hii ni moja kati ya siri ambayo imefichwa vibaya katika soka.
Ni wazi Mbappe anakwenda zake katika klabu hii maarufu ambayo ni ndoto ya karibu kila mwanasoka duniani. Hauwezi kumlaumu. Ana sababu za msingi za kufanya hivyo.
Kama akizubaa sana basi Vinicius Junior anaweza kuwa mwanasoka bora wa dunia kabla yake. Mbappe analazimika kwenda Madrid kwa sababu anahitaji njia ya mkato ya kutwaa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia.
Real Madrid wanahitaji kumpa nafasi hiyo kwa urahisi tu.
Kuna kitu ambacho Madrid wanacho katika michuano hii. Ni kama tulivyoona namna ambavyo kiajabuajabu tu wamekwenda fainali baada ya kuonekana wana wakati mgumu dhidi ya Bayern Munich.
Mbappe anakihitaji hiki kitu kwa sasa ili aende kwa upepo. Vinginevyo hata Jude Bellingham anaweza kuwa mwanasoka bora wa dunia kabla yake.
Msimu uliopita Erling Haaland alikuwa mbele yake katika tuzo za mwanasoka bora wa dunia kwa sababu Manchester City walimpa taji la ubingwa wa Ulaya.
Basi tu kwa sababu Lionel Messi alikuwa ametoka kutwaa taji la kombe la dunia pale Doha. Mbappe hakuingia katika ubishi huo kwa sababu PSG haikumpa taji lolote.
Na sasa Mbappe analazimika kwenda zake Real Madrid kushindana na mwenzake ndani ya timu moja.
Achilia mbali Haaland, washindani wengine wa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia atakutana nao mazoezini na vyumba vya kubadilishia nguo pale Santiago Bernabeu.
Vinicius Junior pamoja na Jude. Mbaya zaidi zama za kujinafasi zimewadia baada ya Messi na Ronaldo kumaliza zama zao.
Lakini hii ni habari nzuri kwa La Liga. Ofisi za La Liga pale Madrid. Wamekenua mpaka gego limeonekana. Baada ya Ronaldo kuondoka kisha Messi kuondoka Ligi yao imepoteza majina makubwa yanayoisisimua dunia. Sio nzuri sana kwa biashara. Wakati huo huo Waingereza wanammiliki Haaland.
Wakati huo huo Waingereza wana ligi yenye mvuto zaidi. Fikiria kwamba ligi yao inaendelea kuamuliwa siku ya mwisho keshokutwa.
Jaribu kutazama namna ambavyo El Clasico ilivyopoteza msisimko wake kwa sasa. Hakuna majina makubwa. Waarabu waliimaliza El Clasico.
Wachezaji wenye majina makubwa kama akina Kevin De Bruyne wameishia kucheza Manchester City mpaka nyakati hizi ambazo viwango vyao vinadidimia.
Kina Mbappe wanaweza kujaribu kuifufua ingawa jirani zao Barcelona wapo hoi.
Vipi kwa PSG? Nadhani mradi wao wa kuwa na wachezaji wenye majina makubwa zaidi umekufa ghafla.
Na sasa wanalazimika kurudi katika ramani na kujenga timu yenye ushirikiano kuliko yenye majina makubwa.
Ousmane Dembele hayupo katika daraja la Messi wala Mbappe ingawa ni kipaji maridhawa.
PSG wanalazimika kuwa kama Arsenal au BayerLeverkusen. Kutengeneza timu inayocheza kitimu zaidi kuliko kutegemea uwezo wa galactico. Katika miaka ya karibuni imewezekana.
Mpira umerudi kwa makocha na mipango madhubuti. PSG licha ya kuwa na pesa nyingi lakini wanalazimika kurudi katika ramani nyingine ya vita.
Lakini hata ukiwataka hao galactico unawapata wapi? Kwa sasa unaweza kuwahesabu wanne au watatu. Unawahesabu katika kiganja chako kimoja na mkono na haumalizi.
Kwa nini wamepotea? Huu ni mjadala mgumu wa siku nyingine. Hakuna tena Ronaldinho, Zinedine Zidane, Rivaldo, Ronaldo Di Lima wala Allesandro del Piero.
Mwache Mbappe aende akaitengeneze El Clasico. Mwache pia akawanie kuchukua tuzo ya mwanasoka bora wa dunia.
Alipochukua kombe la dunia mwaka 2018 bado hakuweza kuchukua tuzo hii. Wakati wake ulikuwa bado. Lakini sasa wakati umefika na akizubaa PSG katika ligi ya wakulima Ufaransa anaweza kuozea huko bila ya taji. League one haiwezi kukupa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia.
Mashahidi tunasema mwache Mbappe aende Madrid. Itarudisha pia utamaduni wa wachezaji wakubwa kwenda timu kubwa.
Waarabu wamesumbua sana na pesa zao. Ingawa hata hivyo Mbappe atakuwa anakwenda kukatwa mshahara. Tusubiri kuona tangazo rasmi wiki chache zijazo.
Amefanya kitu kizuri kuiheshimu PSG. Amesubiri waondolewe katika Ligi ya mabingwa ndio atangaze kuondoka.