Rais Mwinyi aahidi ushirikiano kukuza utalii Arusha

Arusha. Zanzibar imeeleza nia ya kushirikiana na Mkoa wa Arusha kuimarisha uwekezaji katika sekta ya utalii ambayo imekuwa ikiimarika na kuleta mchango mkubwa wa kiuchumi visiwani humo.

Akizungumza katika semina ya wanahisa wa Benki ya CRDB leo Mei 17, 2024, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema kuna uhusiano wa karibu kati ya yanayoendelea Zanzibar na Arusha katika masuala ya utalii, hivyo kuhitajika ushirikiano wa karibu kati ya pande hizo.

“Watalii wanaanzia Zanzibar ambako wanafurahia utalii wa ufukweni kabla ya kuja Arusha kwa ajili ya utalii wa mbuga au kinyume chake. Kwa hivyo, kuna haja ya ushirikiano,” amesema.

Amesema kwa sasa wawekezaji wanamiminika Zanzibar ambako hoteli nyingi zinajengwa. Kinyume chake, Arusha, ambayo ni mji mkuu wa utalii Tanzania, unakabiliwa na uhaba wa vyumba katika hoteli ili kuhudumia idadi ya watalii inayoongezeka.

Rais Mwinyi amesema hayo akijibu ombi la Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda aliyesema kuongezeka kwa vitega uchumi katika utalii wa Zanzibar hasa katika ujenzi wa hoteli ni ujumbe tosha kwamba Serikali inaweza kuvutia wawekezaji pia kuzingatia kuwekeza Arusha.

Katika hatua nyingine, Dk Mwinyi ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuendelea kutengeneza faida kubwa inayoiwezesha kutoa gawio kwa wanahisa.

“Nadhani sitakuwa nimekosea nikisema ongezeko la faida baada ya kodi, ambayo CRDB imepata mwaka jana kufikia Sh424 bilioni kulinganisha na Sh351 bilioni mwaka 2022, ni ukuaji mkubwa wa faida kupata kutokea,” amesema Rais Mwinyi.

Amesema CRDB imeendelea kudhihirisha kwa vitendo kuwa ‘benki kiongozi’ nchini kwani kila mwaka imekuwa ikiendelea kutoa faida ya uwekezaji kwa wanahisa, huku akizitaka taasisi nyingine za umma na binafsi kuiga mfano.

“Nimefurahishwa pia kusikia mwaka huu bodi ya wakurugenzi imekuja na pendekezo la ongezeko la asilimia 11 la gawio kwa hisa. Wanahisa wa Benki ya CRDB mnastahili kutembea kifua mbele kwa ongezeko hili,” amesema.

Rais Mwinyi pia amesisitiza umuhimu wa sekta ya fedha katika maendeleo ya Taifa, akitambua mchango wa benki katika kuimarisha uchumi wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Ameeleza jinsi CRDB ilivyo mshirika muhimu katika kuendeleza dhana ya uchumi wa buluu, kupitia programu kama vile ‘Inuka na uchumi wa buluu’, ambazo zimechangia katika sekta za utalii, kilimo, ufugaji, uvuvi, mafuta, biashara, na ujasiriamali.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB, Dk Ally Laay amesema ikiwa benki ya kizalendo inayomilikiwa na Watanzania kwa zaidi ya asilimia 80, CRDB inajivunia kuendelea kukuza thamani ya uwekezaji wa wanahisa, ikiwemo Serikali, ambayo inamiliki asilimia 36 ya hisa katika benki hiyo.

Dk Laay amewakaribisha Watanzania wengine kuwekeza ndani ya Benki ya CRDB ili nao waanze kunufaika na gawio ambalo limekuwa likitolewa.

Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Abdulmajid Nsekela amesema malengo ya semina hiyo ni kuwajengea uwezo wanahisa na Watanzania wengine ili kujenga uwajibikaji wa kifedha na kuongeza ushiriki katika fursa za uwekezaji, hususani katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.

Katika semina hiyo, mada mbalimbali zilijadiliwa, ikiwa ni pamoja na ujumuishi wa kifedha, uwekezaji katika hisa, hatifungani ya kijani, wosia na mirathi, na kinga dhidi ya majanga.

Semina iliyofanyika jana ni sehemu ya maandalizi kuelekea Mkutano Mkuu wa 29 wa Benki ya CRDB utakaofanyika kesho katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).

Related Posts