RC Mrindoko acharuka fedha za makandarasi

Katavi. Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote tano kulipa madeni wanayodaiwa na makandarasa wanaotekeleza miradi ya maendeleo katika halmashauri zao.

Kauli hiyo ameitoa leo Ijumaa Mei 17, 2024  wakati akisikiliza kero za wananchi baada ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wakidai kutolipwa fedha kutokana na kazi walizofanya kwenye miradi ya maendeleo ya halmashauri za Mkoa wa Katavi.

Hatua ya wananchi hao kutolipwa inatokana na kile alichokisema kiongozi huyo kuwa ni huku Makandarasi  hawajalipwa fedha na halmashauri ili waweze kuwalipa.

Mwamvua  amesema malalamiko hayo yapo kila halmashauri jambo ambalo sio zuri. Amefafanua mkandarasi anapocheleweshewa malipo yake naye atachelewa pia vibarua na watoa huduma wanaohudumia mradi anaotekeleza.

“Maeneo niliyopita kusikiliza kero za wananchi  nimekutana na malalamiko ya wananchi wakidai hawajalipwa fedha zao na makandarasi katika miradi inayoendelea kwenye halmashauri zetu hii inatokana na makandarasi kucheleweshewa malipo yao.

“Naagiza wakurugenzi wote katika halmashauri zote tano lipeni madeni yote mnayodaiwa tumalize malalamiko haya na usumbufu kwa wananchi wetu na tusiwagombanishe na Serikali,” amesema.

Peter Katundu mkazi wa Wilaya ya Tanganyika amesema anafanya kazi ya kuchimba na kuponda kokoto wilayani humo, anamdai mkandarasi anayejenga shule ya sekondari fedha za kokoto baada ya kukubaliana akilipwa na halmashauri, atamlipa lakini anaona siku zinapita fedha zake halipwi.

Anasema anamdai mkandarasi huyo zaidi ya Sh9 milioni za kokoto.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Tanganyika, Shaban Juma amesema anazo taarifa za mwananchi huyo kumdai mkandarasi na anazifanyia kazi.

“Uzuri waliandikiana mkataba wa malipo na mkandarasi amekiri kudaiwa.  Yote tuliyoagizwa na mkuu wa mkoa tunayafanyia kazi ili wanaodai tuone namna ya kuwalipa stahiki zao,” amesema Juma.

Kwa upande wake, mwalimu mstaafu,  Zubeda Makambo amesema amekuwa akisumbuka kufuatilia fedha zake za kumrudisha nyumbani  pamoja na mafao yake  kila akifika halmashauri ya Manispaa ya Mpanda anamzungushwa tangu mwaka jana.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda, Sophia Kumbuli amemueleza mkuu wa mkoa kuwa fedha za mwalimu huyo tayari zimesainiwa na kilichosali ni kuziingiza benki kwenye akaunti yake.

“Ndani ya siku saba nafikiri atakuwa amepata fedha zake na yote uliyotuagiza Mkuu wa Mkoa tutayafanyia kazi,” amesema Kumbuli.

Related Posts